Saturday, October 30, 2010

Amri kumi za Uchaguzi

1. Tambua kwamba kura ni silaha takatifu inayokuwezesha kumchagua yule
unayeamini kwamba unaweza kumkabidhi sehemu ya maisha yako na ukawa salama.
Tumia busara.

2. Jua kwamba ni usaliti kwako mwenyewe na kwa wananchi wengine iwapo
utapiga kura kwa misingi ya rushwa. Anayekununua hakuthamini. Kwake wewe ni
bidhaa tu, kama maharage.

3. Usiruhusu hisia za ubaguzi wa kabila, rangi, dini, jinsia, au ubaguzi wa
aina yoyote nyingine ili utawale uamuzi wako katika kupiga kura.

4. Tenda haki kwa wengine, na pia dai haki yako kutoka kwa wengine.
Usimwonee yeyote na wala usimruhusu yeyote akuonee.

5. Watetee na walinde wanyonge na wasiojiweza. Wasaidie ili waweze kutumia
haki yao ya kupiga kura.

6. Imarisha uhuru wako na uhuru wa nchi yako kwa kuhakikisha kwamba uchaguzi
unakuwa na maana, na kwamba kila kura inayopigwa ina maana.

7. Epuka vurugu, vitisho na ugomvi. Kura ni jambo la raha, si karaha.

8. Kumbuka kwamba amani ni mwana wa haki. Penye haki, aliyeshindwa akubali
kushindwa, na aliyeshinda bado atende haki kwa aliyeshindwa.

9. Tambua kwamba uchaguzi unakuja na kwisha, viongozi huja na kuondoka,
lakini Taifa na watu wake hudumu milele. Tuliza hamasa, epuka chuki, uwe na
ustahimilivu.

10. Hii ni fursa adhimu; ifurahie.

JENERALI ULIMWENGU

0 comments:

Post a Comment