Slaa: Nitafanya maamuzi magumu
• Asema lengo ni kurudisha umoja
na Janet Josiah, Bukoba
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema taifa linahitaji kiongozi anayeweza kufanya maamuzi magumu bila kujali lawama, kama alivyofanya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake.
Akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba kwenye Uwanja wa Mashujaa jana, Dk. Slaa alisema bila kuwa na kiongozi mwenye maamuzi magumu, taifa litaendelea kupoteza mwelekeo kama ilivyotokea miaka ya hivi karibuni.
“Taifa hili lilipofika sasa, linahitaji kuwa na kiongozi ambaye anaweza kuchukua maamuzi magumu, kama vile Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alivyofanya enzi za uhai wake… Watanzania nichagueni ili nirejeshe tunu za kitaifa alizozijenga Mwalimu, lakini zimemomonyolewa na utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM),” alisema Dk. Slaa.
Akitoa mfano, alisema Mwalimu Nyerere alipotaifisha shule za madhehebu ya dini kuwa za umma, alilenga kuwawezesha wananchi wote kupata elimu na kuua matabaka.
Alisema mwanzoni baadhi ya watu, akiwamo yeye walimlaumu Nyerere bila kuelewa, lakini sasa wakiangalia nyuma wanaona alifanya kazi ya kujenga taifa, kwa kujenga shule zilizosaidia kuchochea muungano wa watoto wa Kitanzania na kuwafunza uzalendo.
Alisema viongozi waliomrithi wamebomoa misingi ya utaifa, uaminifu, uadilifu na uzalendo vitu vilivyosimika dira ya taifa.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Bukoba, waliojipamba na rangi za bendera ya CHADEMA, wengi wao wakisisitiza kwamba kwao jana haikuwa siku ya Nyerere, bali ya Slaa.
“Pamoja na kwamba leo ni siku ya Nyerere, kwetu sisi leo watu wa Bukoba ni Slaa Day,” alisikika mmoja wa watu waliokuwa kwenye mkutano huo.
Kabla ya kuwahutubia wakazi hao, Dk. Slaa aliingia na maandamano yaliyoanzia katika maeneo ya Ijuganyondo na kupita katika barabara kuu itokayo Dar es Salaam hadi viwanja vya Uhuru.
Huku akisisitiza umuhimu wa serikali kutoa elimu bure kwa wananchi, alisema viongozi wa CCM wanadai haiwezekani kwa sababu wamefikia mwisho wa kufikiri, na hawana uchungu na taifa kwa kuwa wanang’ang’ania anasa.
“Elimu bure inawezekana, kama Rais Jakaya Kikwete anadhani urais ni kula mayai tu Ikulu, niko tayari kula mihogo ili niokoe pesa za wananchi nisomeshe watoto hawa,” alisema Dk. Slaa.
Kuingia kwake mjini hapa, kulisababisha karibu shughuli zote kusimama kutokana na watu kuacha kazi zao huku mbwembwe, shangwe, shamrashamra na milio ya vuvuzela na maandamano ya baiskeli, pikipiki, magari na watembea kwa miguu yakiongozwa na helikopta.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, ukubwa na mabonde yaliyoko Tanzania ni zaidi ya nchi nzima ya Japan ambayo imekuwa inatupa chakula cha msaada kila mara.
Alisema kwa sababu ya kukosa vipaumbele, Kikwete aligawa mabilioni kwa watu wachache na baadaye akagawa trilioni 1.3 kwa makampuni aliyodai anataka kuyanusuru kutokana na ukali wa kiuchumi, lakini imekuja kugundulika kuwa baadhi ya makampuni yaliyofaidi mabilioni hayo ni ya rafiki zake.
Kama ambavyo amekuwa akisisitiza katika mikutano yake, Dk. Slaa aliwataka wananchi kufanya kampeni na kupiga kura kwa amani, lakini akimlaumu Rais Kikwete na CCM kwamba wanahatarisha amani ya nchi kwa kuwafunza vijana wao kupiga watu.
0 comments:
Post a Comment