Dola yachunguza sms za uchochezi
• Watakaonaswa kuchukuliwa hatua za kisheria
na Betty Kangonga
TAASISI za dola zinazosimamia ulinzi na usalama wa taifa zimeanza kuwasaka watu wanaojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa ujumbe wa maneno wa simu za mkononi wenye maneno ya uchochezi na yanayoweza kuhatarisha amani.
Hatua ya vyombo hivyo vya dola ilitangazwa jijini Dar es Salaam jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, wakati akizungumza kwenye mkutano wa wazi uliowakutanisha viongozi wa taasisi za dola, dini na vyombo vya habari kujadili mwenendo wa kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
IGP Mwema alisema taasisi hizo za dola zimeamua kuchukua uamuzi huo kutokana na kutambua kwamba matumizi mabaya na yasiyofaa ya teknolojia ya mawasiliano kama zilivyo simu za mkononi, yanaweza yakawa ni chanzo cha kuvunjika kwa amani na utulivu uliopo.
Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano, upo uwezekano wa mtu aliye hapa nchini akaandika ujumbe wa maneno kupitia simu yake ya mkononi na kuutuma ukionekana kutoka nje ya nchi.
“Kutokana na kukua kwa teknolojia, mtu anaweza kuwa hapa nchini akatengeneza meseji inayoonekana inatoka nje ya nchi ambayo inaweza kuwa nzuri au mbaya. Tusipokuwa makini kuna uwezekano wa kusababisha vurugu,” alisema Mwema.
Pasipo kufafanua, IGP Mwema alisema uchunguzi walioanza kuufanya kuhusu ujumbe huo wa maandishi ambao katika siku za hivi karibuni umezua mtafaruku katika jamii umeshafikia katika hatua nzuri.
Pamoja na kuahidi kutoa taarifa kuhusu vitendo hivyo, IGP Mwema alizungumzia pia tamko lililosomwa kwa niaba ya vikosi vya ulinzi na usalama na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo.
IGP Mwema alisema tamko hilo halikuwa na lengo la kuwatisha wananchi bali lilitolewa baada ya kufanyika kwa kikao cha pamoja kilichokuwa kimezishirikisha taasisi mbalimbali za ulinzi na usalama za dola.
Alisema katika dunia ya sasa ambayo uhalifu umekua, ni kawaida kwa taasisi za ulinzi na usalama kukutana kujadili mambo na kwa hapa nchini vikao vya namna hiyo hukaa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.
Mwema alisema ni jambo la kusikitisha kwamba tamko hilo lililosomwa na Shimbo lilipokewa ndivyo sivyo na wananchi mbalimbali ambao kwao waliona kuwa lililokuwa na lengo la kutoa vitisho.
“Si nia ya vyombo vya dola kutaka kupendelea serikali, bali mafunzo tuliyopewa ambayo yanatutaka kuhakikisha tunaheshimu maamuzi yanayofanywa na wananchi ambao huwaweka viongozi madarakani na sisi tupo tayari kushirikiana na serikali itakayokuja,” alisema Mwema.
Akichangia mjadala huo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC), Anthony Makunde, alisema vikosi vya ulinzi vinapaswa kuhakikisha kunakuwapo na mawasiliano ya haraka kwa wakati huu ili kuweza kuvuka salama katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Naye mdau aliyetambulika kwa jina moja la Chase, aliitaka serikali iwaamini viongozi wa dini na kuachana na upotoshaji na kutafsiri vibaya pindi wanapotoa elimu kwa waumini wao kuhusiana na viongozi wa aina ipi wanaohitajika kuwekwa madarakani.
Kwa upande wake, Abdulsalim Mashoto, alisema amani na utulivu si wimbo wa sasa bali umeanza kuimbwa toka enzi ya chama kimoja, hivyo wanapaswa waamini kuwa wimbo huo ni wa wananchi wote na si Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee.
“Siamini kuwa vyama vya upinzani vina nia ya kutaka kumwaga damu, ni siasa na propaganda za kizamani ambazo zinashikiliwa na CCM. Hiyo ni dalili ya kutojiamini,” alisema.
Akichangia mjadala huo, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajab Kiravu, alisema NEC haiwezi kufanya marekebisho tena ya daftari la uandikishaji kwa wakati huu ili kutoa fursa kwa wanafunzi walioandikishwa vyuoni kupiga kura, kwani hilo linaweza kusababisha kutokea kwa vurugu kubwa ambayo haitaweza kutatuliwa.
Kiravu alieleza kusikitishwa na namna taarifa zinazohusu wanafunzi waliojiandikisha vyuoni ambao sasa wako likizo zinavyofanywa kisiasa.
Alisema hakuna mtu aliyejiandikisha akaonewa au akanyimwa haki ya kupiga kura, bali wote waliojiandikisha watashiriki na hata katika idadi iliyoandikishwa hakuna kituo kinachozidi zaidi ya wapiga kura mia tano, hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu ya kuibiwa kura.
Katika hatua nyingine, IGP Mwema ameunda kikosi maalumu kwa ajili ya kufuatilia madai mazito yaliyotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuwa kulikuwa na njama chafu zilizohusisha askari polisi, ambazo zilikuwa zikilenga kumbambikizia mwanae dawa za kulevya.
IGP Mwema aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa timu hiyo ya maofisa wa polisi inaongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.
Hatua ya IGP Mwema kuunda timu hiyo imetokana na madai yaliyotolewa na Mengi juzi, kuwatuhumu wazi wazi kwa kuwataja majina maofisa wa jeshi hilo aliodai walihusika na sakata hilo.
Kutokana na hali hiyo, IGP Mwema alisema DCI Manumba na timu yake wametakiwa kukusanya vielelezo vyote kuhusiana na tuhuma hizo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika, ingawa hakutaja itafanya kazi hiyo kwa siku ngapi.
“Hapa ninapoongea nanyi, hammuoni DCI Manumba, nimelazimika kumtuma kufuatilia suala hilo ili tuweze kupata ufumbuzi wa kina. Tunaamini yeye na kikosi chake watafanya kazi ambayo majibu yake tutawaeleza Watanzania.
0 comments:
Post a Comment