Tuesday, October 12, 2010

Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki amesema, kwa hakika hazitaki,
Mbona mna muandama, kwa kisa kile na hiki,
Kikwete mtu mzima, na wala msihamaki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Pendo kitu cha hiari, hakina lazima katu,
Ni vema kujihadhari, msizidi kuthubutu,
Si kwa kero nazo shari, mumwache mwana wa watu,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mapenzi kweli maua, huweza ota popote,
Bali huhitaji nia, kuyahudumia yote,
Bila maji kumwagia, Hunyauka kwa vyovyote,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Wafanyakazi hataki, mwataka nini zaidi?
Msitumie mikiki, hali mu watu weledi,
Binadamu ana haki, kupima na kukaidi,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mbona hamna simile, huria kumuachia,
Mmeng'ang'ana na lile, hamtaki kusikia,
M-bembeleze milele, hataki kawaambia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mmejawa na hiana, kwa jibu alilotoa,
Kawaeleza bayana, wazi amewaambia,
Mwalitafuta laana, msilolitarajia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Kwa uvumba na ubani, kesha sema hazitaki,
Zaidi mwataka nini, awaeleze rafiki?
Tulia mkae chini, muwaze na kuhakiki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki kakataa, kura zenu kasusia,
Japo mlete gitaa, na nyimbo kumuimbia,
Mumtembeze mitaa, kwa manoti mia mia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki si ajabu, kura zisizo na soko,
Msiitafute tabu, kujipendekeza mwiko,
Bure mwajipa aibu, kwa kumpa mialiko,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.


Kaditamati shairi, kura zenu hazitaki,
Kila kitu ni hiari, shuruti haina haki,
Kuchagua ni fahari, lazima haipendeki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

0 comments:

Post a Comment