Monday, October 11, 2010

Tafiti za kama wa REDET ziangaliwe kwa macho mawili

Saturday, 09 October 2010 21:00
0diggsdigg

Dk Benson Bana

Yahya Charahani

ALHAMISI iliyopita, Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet), ulitoa taarifa ya matokeo ya utafiti kuhusu maoni ya wananchi kuhusu uUchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Matokeo ya utafiti huo yalionyesha mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete anaongoza kwa asilimia 71.2 dhidi ya wagombea wa vyama vingine.

Mbali ya matokeo hayo ya Kikwete, Redet ilisema matokeo ya jumla yanaonyesha CCM inaongoza katika nafasi zote yaani urais, ubunge na udiwani. Matokeo hayo ni kwa utafiti wa mwezi uliopita.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti mwenza wa Redet, Dk Benson Bana alisema katika utafiti huo, Kikwete aliungwa mkono kwa asilimia 71.2 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Dk Willbrod Slaa asilimia 12.3 na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akipata asilimia 10.1.

Katika utafiti huo, mfumo wa sampuli nasibu unaelezwa kuwa ulitumika kwa kuzingatia idadi ya watu waishio mijini na vijijini ili kupata matokeo ya uhakika.

Utafiti huo ulihusisha mambo mengi kama vile, maoni ya watu kuhusu vyama vya siasa na wagombea, maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi wa rais na wabunge, maoni ya watu kuhusu mgombea urais, sifa za mgombea urais wanayemtaka n.k.

Kwa kuwa si rahisi kuzungumzia kila kitu kilichojitokeza katika matokeo ya utafiti huo, nichukue fursa hii kuzungumzia matokeo ya utafiti huo kwa upande wa kitaalama zaidi.

Nimeshawishika kujadili kipengere hicho kutokana na ukweli kwamba, matokeo ya utafiti huo kwa upande huo yanatisha, yameibua zogo.

Bila shaka yamewashangaza watu wengi kiasi kwamba, baadhi ya watu wakiwamo wagombea wenyewe mpaka sasa hawaamini kama kilichotangazwa na Redet ni cha kweli na baadhi wanathubutu kusema kuwa imehongwa.

Mashaka ya usahihi wa utafiti huo unatokana na takwimu zilizokusanya kutoa majibu tofauti na hali halisi ilivyo katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, Pemba ambako inajulikana wazi kuwa ni ngome ya CUF miaka yote tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi ulipofanyika mwaka 1995, taarifa ya utafiti huo inaonyesha CCM inaongoza!

Najua kuwa utafiti huo ulifanyika kisayansi na unatakiwa kupingwa kisayansi, lakini zinapotolewa takwimu zinazokinzana na hali halisi, lazima kuwa na mashaka! Lazima mtu atajiuliza kwamba, hivi katika kipindi hiki kifupi yametokea mabadiliko makubwa kiasi hicho? Sipingi matokeo ya utafiti huo, lakini mashaka yangu yanaweza kuelekea kwa waliohusika kukusanya taarifa kwamba huenda hawakufanya kazi vizuri kwa makusudi, au maelekezo ya kutimiza lengo fulani.

Kwa mtaalamu yeyote anayejua maana ya utafiti ataelewa moja kwa moja kwamba utafiti wa Redet una maana gani. Maana hiyo ataipata baada ya kuingia ndani zaidi ya kile kinachoelezwa hadharani.

Nafahamu lengo la utafiti ni kujaribu kuelezea hali halisi ya wahusika kwa kutumia wawakilishi ndani ya wahusika hao, Ingawa kuna mambo lazima yazingatiwe.

Kwanza, msingi mkuu wa utafiti na ukusanyaji wa maoni huwa watu waliopo katika mazingira sawa sawa na tabia ya kufuata mkondo sawa wa fikra.

Uwezekano huu huwa sawa na kwa maana hiyo, badala ya kuuliza kila mtu kama anaunga mkono fulani. Huwa rahisi kutafuta watu wachache katika mazingira hayo ili kupunguza uwezekano wa kuchukua watu wanaoamua kujitenga kutoka kwa maoni ya watu wengi na njia hutumia hii kama mwongozo.

Pili, tumeelezwa lengo la wazi la utafiti huu, lakini hatujajua lengo lililojificha la utafiti ambalo kikawaida anayelijua ni mtafiti mwenyewe au mteja anayempa kazi ili aweze kuufanyia kazi.

Jambo jingine ni kwamba, tutambue kuwa huu ni utafiti wa kisayansi na hatuwezi kusema kuwa haukuwa halali na ili kuweza kujibu mapengo yaliyojitokeza tunatakiwa kufanya utafiti mwingine.

Jingine ni ukweli ulio wazi kwamba, popote pale, ukiwa madarakani kama unafanya kazi lazima uzalishe wasioridhika, hasa wakati ukisimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali.

Kwa muktadha huo huo, upande wa pili lazima watu wakiwa wamekata tamaa lazima watafute tumaini, au mahali ambapo patawapa faraja na faraja hiyo wataipata upinzani.

La mwisho ni kwamba, utafiti wowote wapaswa kufanywa kwa kufuata kanuni ambazo mwishowe yanapatikana matokeo yanayoonyesha ukweli. Ukweli wa utafiti huu hatuwezi kuuzungumzia sababu hatuna kipimo kingine kilichopima kisayansi joto la uchaguzi mkuu.

Yahya Charahani ni mchambuzi wa masuala ya jamii, siasa na utawala.
Anapatikana kwa email: charahani@yahoo.com This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it
Blogu charaz.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment