Ndugu wana JamiiForums, Mtandao wa IssaMichuzi, wana FaceBook na mitandao mingine na Watanzania wenzangu wote kwa ujumla mtakaosoma ujumbe huu, Salaam toka Mbeya Vijijini, ndio tumeanza mikutano midogo ya kufunga kazi asubuhi hii na tutahitimisha baadaye.
Ninashukuru sana kwa maneno ya heri kwa siku yangu ya kuzaliwa hapo jana na ningekuwa sina shukrani kama ningeacha ipite bila kusema asante kwa maneno mema mliyonipatia humu na kwenye facebook na hata waliopata nafasi kwa njia ya simu. Ninawashukuru vile vile kwa mashauri mbalimbali, na pia kwa sala na dua zenu.
Ninashukuru sana na ninaona fahari kuwa ni mwanachama mwenzenu.
Kampeni zote zinaisha leo na kesho ni siku ya Uchaguzi Mkuu kama mnavyofahamu. Kwa upande wangu nimetembelea karibu maeneo yote ya nchi yetu kubwa, nimekutana na watu mbalimbali na nimeona mengi. Nimeona mengi yenye kutia matumaini na faraja na nimena mengine ya kuhuzunisha na kukatisha tamaa. Yote kwa ujumla yake yamenipa picha ya kuelewa zaidi Taifa letu hasa kuhusu mafanikio tuliyoyapata mpaka hivi sasa na changamoto tulizonazo.
Ninaelewa vizuri zaidi sasa kupitia mang’amuzi binafsi hali ya Taifa letu ilivyo na ya kwamba ni lazima tubadili mwendo na huko tunakokwenda maana tutafika mahali ambapo tutashindwa hata kujiuliza tulifikaje. Watu makini hawawezi kuendelea na njia ambayo wanajua wamepotea. Kuendelea kung’ang’ania kwenda wakati mnajua mmeshapotea ni kutukuza kiburi cha kujiona. Taifa letu limepotea njia na hata kama tukijitahidi kwa nyimbo na masimulizi mbalimbali kuhalalisha huko tunakokwenda bado tutakuwa tumepotea.
Ni kwa sababu hiyo nilipoombwa kugombea Urais nilitambua uzito wa mzigo huu mkubwa kwani utahusiana moja kwa moja na kubadilisha mwelekeo wa taifa letu na kuanza kutengeneza pale palihorabiwa, kuinua kilichoanguka na kumwagilia kilichoanza kunyauka. Hili linahitaji mawazo mapya, uthubutu wa kiuongozi na mtazamo mpya wa nini Taifa letu linahitaji. Ndugu zangu, Taifa letu linahitaji mabadiliko makubwa ili tuweze kujipa sisi wenyewe na watoto wetu nafasi ya kuweza kufanikiwa huko mbeleni.
Mabadiliko haya siyo mabadiliko ya mapambo yaani kuhamimisha maua na vitambaa sebuleni wakati nyumba inanuka na nichafu. Wote mliosikiliza au kumwangalia mgombea mwenzangu jana ni wazi hana ahadi ya mabadiliko yoyote makubwa isipokuwa mwendelezo wa yale yale yaliyotufikisha hapa. Ni kutokana na hilo natambua kuwa kura ya kesho siyo kura ya kawaida; siyo kura kama ya 2005 au ya miaka kabla yake.
Kura ya kesho ni kura ya kuchagua kuendelea na vile tulivyo kwa miaka mitano ijayo au kubadilika ili tuanze upya kwa njia sahihi na kwenda ambako sote tunakujua tunataka kwenda. Ninaamini tunachohitaji ni mabadiliko yatakayoanzisha mwamko wa kuanza kulijenga upya taifa letu. Hili ndilo lililonifanya nikubali pale Chama changu kiliponiomba ninyanyue bendera ya Chadema kwenye uchaguzi huu katika nafasi ya Urais.
Naweza kuwaahidi mengi na kwa maneno matamu ya kila aina. Hata hivyo ninawaahidi kitu kimoja kwa uhakika wa asilimia 100. Mkinichagua kuwa Rais wenu na mkiwashawishi ndugu, jamaa na marafiki zenu kufanya hivyo nami nikachaguliwa, nitawapatia uongozi ambao utaifanya miaka 49 iliyopita kuwa ni ya masimulizi ya njozi za jinamizi kwani nitaongoza timu ya watu ambao watakuwa wamejitokea muda, elimu, ujuzi na vipya vyao katika kujenga taifa letu upya. Katika miaka mitano ijayo tutafanya mambo ambayo CCM na utawala wake imeshindwa kufanya kwa karibu miaka hamsini.
Tutawapa nafasi Watanzania hatimaye nao wafurahia matunda ya uhuru wao na vile vile kuweza kuanza kujenga Taifa la kisasa ambalo litakuwa ni tamanio nakinara cha mabadiliko ya kiutawala, kiuchumi na kiutendaji katika Bara letu. Tuna uwezo, tuna sababu na tuko tayari kuwatumikia.
Naomba sana kura zenu hapo kesho ili niwe Rais wenu katika awamu ya tano. Kura yako ina nguvu ya kubadilisha mwelekeo wa taifa letu. Usiuze, usiache kuitumia na pale utakapoitumia itumie kwangu, kwa wagombea Ubunge Chadema na wagombea wetu wa Udiwani ili tuweze kuhakikisha yote tuliyowaahidi tutayatimiza na zaidi.
Msiwe na shaka, hata toka Ikulu nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa mitandao hii na kuwapa taarifa mbalimbali moja kwa moja na kujibu maswali mtakayokuwa nayo kuhusu serikali yenu pale inaponipasa mimi kutolea kauli. Asanteni!!
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
1 comments:
Umma wa Watanzania upo nyuma yako ndio maana wanaweweseka. Tunakuombea Mungu akupe afya njema na amani, sisi tutafanya kweli hiyo kesho. No way back
Post a Comment