Saturday, October 9, 2010

Gharama ya kura yangu

Ndugu Watanzania. Mwaka huu wa-Tanzania tumepata tena nafasi ya kufanya maamuzi magumu nchini mwetu, maamuzi ya kuchagua viongozi watakaokuwa na majukumu ya kutuendeleza kama Taifa.

Ninaamini swala la uchaguzi ni zito na muhimu sana na kila mmoja wetu ana wajibu mkubwa wa kuwa makini kwa sababu uzembe katika kupiga kura huzaa uongozi wa kibabaishaji na ni ndoto za alinacha kutegemea viongozi wabovu, wapenda rushwa na wasio na sifa kuleta mabadiliko yoyote.

Natambua kila mmoja wetu ana vigezo vyake vya nani atakayempa kura zake, nimeona niwaeleze vigezo vyangu ili tuweze kubadilishana mawazo.

Urais:
Anayekubali midahalo; Ninaamini Rais anayenifaa ni yule amabaye anaelewa matatizo ya kitaifa na mwenye upeo wa kuelewa nini kifanyike katika kukabiliana na matatizo hayo. Ili niweze kumtathmini na kumpima na wagombea wengine lazima awe tayari kuingia kwenye midahalo ili nikiwa kama mpiga kura nipate nafasi ya kumhoji. Siko tayari kumpigia kura mgombea anayefanya kampeni kama tape recorder, yaani anakuja jukwaani kusema anayotaka yeye tu na kuondoka.

Elimu ya Bure; hakuna taifa linaloweza kuwa na mategemeo ya maendeleo bila ya kuwaelimisha wananchi wake. Tanzania ya leo inakabiliwa na tatizo la masikini kuendelea kuwa masikini na matajiri wanazifi kuwa matajiri, njia muhimu ya kuwakomboa walio wengi ni kuwapa elimu yenye manufaa wananchi wote. Siko tayari kukubali hoja ya kwamba haiwezekani, nataka kiongozi ambaye anathubutu kubana matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali kama magari ya fahari ili elimu ipatikane.

Uwajibikaji kifedha; Nataka Rais ambaye hawachekei wahalifu wenye tabia ya kudokoadokoa fedha za umma. Fedha za umma zitumike kwa kile kilichokusudiwa tu na kwa kufuata taratibu zilizopo . Nimechoka kusikia ripoti za kitaalamu zinazothibitisha wizi na Rais hawaagizi wasaidizi wake kuwapeleka wahusika kwenye vyombo vya sheria. Matatizo yetu mengi yangeweza kupungua endapo matumizi ya fedha za umma yangeboreshwa.

Serikali iliyo wazi; nimechoshwa na tabia ya kuendesha kazi za Kiserikali kisiri kama kibaka anayekwenda kuiba usiku wa manane. Nakataka Rais atakayetuletea Sheria inayogusa maswala ya Open Records ambayo inamruhusu kila Mtanzania kupata taarifa zinazohusu maamuzi ya Serikali. Kama Serikali imetoa zabuni kwa kampuni yoyote basi tuwe na nafasi ya kujua undani kama vile makampuni mangapi yaliomba tenda, vigezo gani vilitumika, etc. Kwa mikataba ambayo inaweza kuwa ya siri kama ya kiusalama nayo iwe monitored na kamati ya uchumi ya Bunge ili angalau tuwe na wabunge watakaotuwasilisha kudhitibi utoaji wa zabuni.

Uchumi na Biashara; Kabla ya uhuru tulikuwa ni wazalishaji wa malighafi kwa ajili ya mataifa makubwa, leo hii baada ya karibu miaka 50 bado tunafanya hayohayo. Nataka rais mwenye jibu ya kubadilisha Tanzania kutoka nchi inayozalisha malighafi na kuwa taifa linalozalisha bidhaa za viwango vya juu zilizokamilika.

Serikali na Bunge; Kuna haja ya kuwa na mapinduzi ya katiba. Katiba ina matatizo kadhaa, moja wapo ni hili ya wabunge kuwa mwaziri. Kwa mtizamo wangu hii ni conflict of interest kwa sababu haiwezekani wabunge wajidhibitu wenyewe, tunahitaji clear separation ya hizi nguzo mbili za dola. Mfumo wa sasa hauthamini fedha za walipa kodi, mfano sasa hivi mawaziri wako majimboni kwenye kampeni lakini Serikali inawalipa mamilioni ya mishahara. Wakirudi maofisini Serikalini hawaonekani majimboni mpaka wakati wa uchaguzi ujao wakati wanalipwa fedha kama wabunge. Hawa wanatafuna fedha za bure kwa kuwa haiwezekani wafanye kazi mbili zinazohitaji muda mwingi. Mfumo huu unatumaliza.

Kuimarisha mahakama; leo hii mahakama zetu zinakabiliwa na matatizo ya kdaji kutokana na ukata. Nataka Rais ambaye atahakikisha mahakama zetu zinapata bajeti ya kutosha ili wananchi wapate haki zao katika kipindi muafaka.

Katika nafasi ya Ubunge halikadhalika kura yangu itakwenda kwa Mbunge anayeunga mkono matakwa haya.

Je, wewe una masharti gani kwa anayetaka kura yako?

By US Blogger
Usblogger11@gmail.com

0 comments:

Post a Comment