Saturday, October 2, 2010

Dk Slaa: Nimeisikia sauti ya Mungu ndiyo maana ninagombea urais


DK WILBROD SLAA

WAKATI kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea, vyama vya siasa vimeshatoa ilani zao kwa ajili ya kuzinadi kwa wapiga kura.Chadema ambacho kimemsimamisha Dk Willbroad Slaa kugombea urais kimeweka vipaumbele kadhaa katika utawala wake kama kitashika serikali.Katika mahojiano na waandishi wetu HAWRA SHAMTE na ELIAS MSUYA, Dk Slaa anafafanua.

Swali: Ilikuwaje ukaamua kuingia katika kinyang’anyiro cha urais dakika za mwisho?

Jibu: Ukweli ni kwamba sikuwa na ndoto ya kugombea nafasi hii. Ilikuwa ni siku ya pili tangu nichukue fomu ya kugombea ubunge wa jimbo la Karatu, lakini nikaitwa kwenye vikao vya chama nikapendekezwa kugombea urais. Kwa kweli niliugua siku mbili kwa sababu nafahamu uzito wa nafasi hii. Unajua hata Mwalimu Nyerere alishasema kuwa Ikulu ni mzigo. Hata hivyo ilinibidi kuukubali uamuzi wa viongozi wenzangu.

Licha ya kamati kuu ya chama kuamua hivyo kulikuwa na ushawishi kutoka kwa watu mbalimbali walionishauri nigombee urais; Kuna wanafunzi zaidi ya 400 waliotia saini zao wakipendekeza mimi nigombee urais. Kwa hiyo hao pia walinitia moyo.

Pamoja na kuwa chama chetu tuna utaratibu wa kupata wadhamini 25 kwa mgombea urais, mimi niliwashauri wenzangu tuzunguke mikoani ili kuona kama kweli nakubalika huko.

Tumezunguka mikoa 19 ukiwamo mmoja wa Zanzibar, kwa kweli watu wametupokea…. Kuna baadhi ya mikoa zile fomu za udhamini walikuwa wakizigombea. Wengine walikuwa wakizisaini hadi usiku na ilitubidi kuwasha taa za gari ili wasaini. Kwa hiyo nikaona kuwa kuna sauti ya Mungu.

Swali: Pamoja na kusikia kilio cha wengi waliokutaka ugombee urais, wewe binafsi kitu gani cha ziada kilikusukuma?
Jibu: Nchi yetu ina matatizo makubwa. Ufisadi na wizi ndiyo uliotawala katika serikali ya CCM. Hata chakula cha wafungwa magerezani kinaporwa na askari. Fedha za miradi ya maendeleo zinahamishiwa kwa watu binafsi. Watanzania tunapewa pipi badala ya kilo ya nyama. Hayo ndiyo tunaambiwa maendeleo maana kila siku wanatulisha pipi, kwa kweli ni gharama kubwa kuiacha CCM iendelee kututawala.

Licha ya Mwalimu Nyerere kutaja maadui wakubwa watatu ambao ni Ujinga, umasikini na maradhi, CCM imeongeza adui wa nne ambaye ni ufisadi.
Tatizo jingine ni umasikini uliokithiri ambapo tangu mwaka 2001 hadi 2008 Watanzania ambao ni masikini wa kutupwa wameongezeka kutoka 11.4 milioni hadi 12.9 milioni.

Kwa kweli hapa inaonyesha wazi kwamba Tanzania tunahitaji uongozi utakaoweza kubadilisha haya. Fedha za EPA zingeweza kujenga shule zaidi ya 1000.
Tulipobadilisha Azimio la Arusha na kuunda Azimio la Zanzibar ambalo hadi leo hakuna kumbukumbu zozote zilizoandikwa na kuwekwa bayana zilizotokana na Azimio lile, lakini pale ndipo tulipopoteza msingi mkubwa wa uadilifu na hapo ndipo ulipoanza ufisadi.

Tatizo jingine ni mfumo mbovu wa uendeshaji wa serikali unaosababishwa na Katiba mbovu.
Kwa ujumla tumeona kuwa tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa uongozi.

Tanzania ya sasa inahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kuongoza, anayekubalika, mwadilifu na chama chenye sera zenye kuweza kuleta mabadiliko.
Swali: Nini vipaumbele vyako kama utafanikiwa kuwa rais wa Tanzania?

Jibu: Kwanza nitajenga mfumo mpya wa serikali kwa kubadilisha Katiba. Katiba ya sasa inampa mamlaka makubwa mno rais. Rais anachagua kila kitu mpaka mkurugenzi wa shirika la kulala na kunywa pombe. Mtu analiangusha shirika moja anahamishwa na kupelekwa katika shirika jingine.

Katiba tuliyonayo inaweka hatima ya watu zaidi ya milioni 40 mikononi mwa mtu mmoja. Rais ndiye anayeamua ni wizara ngapi ziwepo.

Wenzetu Marekani wako zaidi ya milioni 200 lakini wana mawaziri 14 tu. Uingereza wako 75 milioni lakini baraza lao lina mawaziri 20. Lakini Watanzania tuko 40 milioni tunakuwa na baraza la lenye mawaziri hadi 47au 67.

Kazi kubwa ya Manaibu waziri waliopo sasa ni kujibu maswali Bungeni ambayo hata hivyo huyajibu juu juu tu.

Wote hao wahudumiwe mashangigi ya Sh 200 milioni na mahitaji mengineyo. Bado hapo unazungumzia makatibu wakuu na watumishi wengine. Mkuregenzi anabadilishiwa fenicha kila mwaka.


Mzigo wote huu wanatwishwa walipa kodi. Badala ya kodi ya maendeleo kuleta maendeleo ina kazi ya kuhudumia viongozi wa serikali tu.


Nikifanikiwa kuingia madarakani nitabadilisha Katiba ili tuwe na mawaziri 20 tu au hata 15. Nitawapa madaraka wananchi katika maamuzi ya serikali tofauti na sasa ambapo wananchi wenyewe hawakushirikishwa kuiunda Katiba yao.

Katiba iliyopo Ibara ya 8 inasema kuwa mamlaka yote ya serikali yanatokana na wananchi, lakini kihalisia hivyo sivyo inavyofanyika. Hivyo tunaona kuwa ipo haja ya kufanya mabadiliko makubwa ya katiba na hayo ndiyo yatakayoleta mabadiliko katika mfumo mzima wa serikali.

Kipaumbele kingine ni huduma za jamii, tutaboresha elimu. Elimu kwa sasa imeshuka sana. Wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na kisomo cha manufaa ambapo Tanzania ilisifiwa na Unesco kwa kufikia kiwango cha asilimia 70, lakini sasa imeshuka hadi asilimia 40.

Takwimu za Mpango wa maendeleo ya sekondari inaonyesha kuwa, serikali ilitakiwa kujenga shule 22,000 lakini hadi sasa imejenga shule 300 tu.

Ahadi kwenye bajeti zipo, lakini hazitekelezwi. Fedha za kashfa ya EPA tu zinaweza kujenga shule bila kuchangisha mtu.Kwetu sisi elimu ya lazima itakuwa ni kidato cha sita.

Kipaumbele kingine ni huduma bora za afya ambapo tutaimarisha afya ya msingi na kuipa kipaumbele katika bajeti.
Huduma nyingine ni maji, leo Watanzania wengi hawapati huduma ya maji licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji.

Niliwahi kwenda Mtwara ambako nilikutana na wananchi wa huko. Baadaye nikaletewa maji ya kunywa, nilidhani ni pombe nikataka kuijaribu, nikaambiwa hayo ndiyo maji ya kunywa. Ilibidi twende umbali wa kilometa 15 nikayaone maji wanayochota. Hali ni mbaya.

Kwa upande wa kilimo, nako hatufanyi vizuri. Tumekuwa tukiomba chakula kila mwaka wakati nchi yetu inaweza kuzalisha chakula kingi, hii ni aibu! Tatizo ni ufisadi, kuna taarifa katika Mpango wa Maendeleo wa sekta ya kilimo (ASDP) asilimia 80 ya bajeti yake imepotea kutokana na wizi na semina za kujitengenezea posho.


Hii ni aibu kabisa, Kila mwaka tunaomba msaada wa chakula kutoka nje. Ni mwaka huu kwa sababu tu mvua zimenyesha sana. Lakini Rais Kikwete anasema kuwa mafanikio yamepatikana kutokana na mkakati wa kilimo kwanza wakati mkakati wenyewe una mwaka mmoja tu tangu uanzishwe. Kazi ya serikali ni kutoa kauli mbiu tu kila mwaka, kaulimbiu hazizalishi!

Bilioni 21 zilizochezewa, zikaitwa za Kikwete hatujui zimekwenda kwa nani.
Kama tungekuwa na mikakati mizuri ya kilimo Tanzania inao uweza kulisha nchi nyingine za Afrika.


Kuhusu miundombinu , Tanzania inapaswa kuwa na treni inayotumia umeme na siyo kuendeleza treni zinazotumia dizeli tangu wakati wa ukoloni. Usafirishaji kwa njia ya malori unaotumika sasa una hasara kubwa kwa serikali ukilinganisha na usafirishaji kwa njia ya reli.

Ni gharama kubwa kuendelea kuvumilia kutawaliwa na CCM. Hakuna utashi wa kisiasa, hakuna anayechukua maamuzi na wala hakuna utawala wa sheria. Nchi ina ‘double standard’ katika kuchukua maamuzi ya kisheria; anayeiba kuku au Sh500 anafungwa lakini anayeiba mabilioni anaachiwa huru na hata anaambiwa kuwa akirudisha atasamehewa.
Swali: Ni vipi utalishughulikia suala la rushwa?

Jibu: Serikali yangu haitakuwa na msalie Mtume na wala rushwa, ni ‘zero tolerance’ kwa ufisadi. Rasilimali zilizotumika vibaya zitarejeshwa serikalini.

Swali: Je, unadhani Chademaina ubavu wa kuiondoa CCM madarakani?
Jibu: Tunaweza kuwaondoa endapo haki itatendeka.

Tatizo ni kuwa hakuna ‘level ground’ ya siasa hapa nchini.

Lakini kwa kuwa wananchi wamechoka na wanasema kuwa safari hii hawakubali tena kudanganywa, tuna imani kwamba Chadema ndicho chama mbadala. Amani wanayoiimba CCM ni amani ya hofu, hakuna amani kwa mtu anayekula mlo mmoja kwa siku.

Swali: Katika uchaguzi kuna kushina na kushindwa, je nini itakuwa hatima yako kisiasa endapo utashindwa?
Jibu: Kwanza sijutii kugombea nafasi hii na ikiwa sikubahatika kuipata basi naweza kuwa Spika wa Bunge kwani nafasi hiyo inaweza kushikwa na hata mtu asiye mbunge.

Kadhalika hata kama hilo halitawezekana sitajuta kwa sababu nina imani kwamba nitaendelea kuwatumikia Watanzania.

0 comments:

Post a Comment