Thursday, October 7, 2010

Dk Slaa avuta umati wa watu mkoani kwa Pinda

Waandishi Wetu Dar na Rukwa
SHUGHULI nyingi za kiuchumi jana zilisimama kwa muda mjini Sumbawanga kufuatia ujio wa mgombea urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa huku akiahidi kutafuta soko la uhakika la mazao yanayozalishwa mkoani Rukwa.

Maeneo ya katikati ya mji huo jana yalianza kudorora kutokana na wakazi wengi kulazimika kwenda katika Viwanja vya Shule ya Msingi Chaji vilivyopo umbali wa takribani kilomita tatu nje ya mji.

Wakazi hao walifika viwanjani hapo kwa kutumia usafiri wa pikipiki, magari ya kukodi pamoja na baiskeli huku wakisherehesha mkutano huo kwa kupiga mavuvuzela.

Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Rukwa kubadilika kifikra kwa kufanya uchaguzi sahihi hapo Oktoba 31 mwaka huu ili kuweza kupata maendeleo ya kweli. Waziri Mkuu Mizengo Pinda anatokea mkoani hapa.

Dk Slaa alisema maendeleo ya kweli huletwa na viongozi waadilifu na hivyo kuwaomba wakazi hao wa Sumbawanga kukipa ridhaa Chadema ili waweze kuwa na maisha bora.

Katika mkutano huo, aliwaomba wananchi ridhaa ya kuweza kumchagua yeye pamoja na mgombea ubunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini, Norbeth Yamsebo pamoja na madiwani wote wa jimbo hilo.

Dk Slaa alisema kuwa "Nimepita maeneo mengi ya Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine ambayo ipo katika the 'big four' nimejionea mwenyewe mlundikano wa mahindi katika nyumba za wakazi wa mkoa huo hivyo naahidi kuwa mara mtakaponichagua mimi na kushika madaraka mtakuwa na soko la uhakika la mazao yenu."

Alisema Serikali yake atakayoiunda itaondoa vikwazo vyote vya uuzaji wa mazao nje ya nchi na hivyo kuwapa wakulima soko la uhakika.

Alisema kuwa sehemu kubwa aliyopita ameona nyumba za wakazi wa mkoa huo zikiwa duni hivyo kuahidi kwamba kama atachaguliwa mfuko wa sementi utakuwa chini ya Sh5000.

Akizungumzia suala la elimu, Dk Slaa alisema kuwa atahakikisha elimu ya msingi na sekondari inatolewa bure na kuwataka jamii ya wafugaji kutomlaumu kwa hilo na kuwataka kuwatoa watoto wao wapatiwe elimu na kuacha kuchunga ng'ombe pasipokuwa na elimu. Kwa sasa ada ya mwanafunzi ni Sh20,000 kwa wale wanaosoma katika shule za serikali.

Katika hatua nyingine, mgombea urais wa TLP, Muttamwega Mugahywa amesema kuwa ataingia Ikulu bila kutegemea fedha za wananchi masikini na mafisadi kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika jana, Karume jijini Dar es Salaam, Mugahywa alijigamba kuwa kamwe hawezi kutegemea fedha ili kuingia Ikulu na badala yake atahakikisha kuwa anakuwa rais wa awamu ya tano kwa jasho lake mwenyewe.Alisema kuwa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania alitumia baiskeli na punda kwa ajili ya kuwazungukia wananchi na kueleza sera zake za ukombozi wa Tanganyika.

Mgombea huyo alijifananisha na kiongozi huyo huku akidai kuwa atazunguka mikoani kufanya kampeni kwa nguvu zake mwenyewe kama ilivyokuwa kwa Nyerere.

"Kila mtu ana haki ya kuwa rais wa nchi hii, mimi nataka kuwa rais, lakini nawaelezeni kuwa sitategemea fedha za wananchi masikini wala mafisadi, sizitaki kwa sababu nataka kuwa rais ili niwasaidie Watanzania masikini," alisema Mugahywa.

Aliongeza: "Nikiwa kijana mdogo mwanzoni mwa miaka ya 90 nilikuwa na maisha ya taabu sana, niliamua kuwa machinga na nilitengeneza fedha zangu mimi mwenyewe hivyo siwezi kutegemea fedha ya mtu yeyote, mimi sio fisadi na nikiingia Ikulu nitakachokifanya kitawashangaza wengi,".

Alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kuichagua TLP na kuachana na CCM ambao wanatoa ahadi ya ajira milioni moja wakati wanaua viwanda.

chanzo: Dk Slaa avuta umati wa watu mkoani kwa Pinda

0 comments:

Post a Comment