Tuesday, February 22, 2011

Mrejesho kuhusu Uwakilishi Wangu katika Mkutano wa pili wa Bunge

Wakati wa kuomba kura nilikuja kwenu katika ukumbi huu kuwaomba mniunge mkono, kati ya ahadi nilizotoa wakati huo ni kuchukua maoni yenu na kuyawasilisha bungeni. Naomba kwa leo niwape mrejesho kuhusu uwakilishi wangu katika mkutano wa pili wa bunge kwa ajili ya kupata maoni ya kuzingatia katika mikutano ijayo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2) Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi ya kuishauri na kuisimamia serikali. Katika kutimiza wajibu huu kwa nafasi yangu ya ubunge wa Jimbo la Ubungo niliwawakilisha wananchi wenzangu kwenye Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi ulioanza tarehe 8 Februari na kuahirishwa tarehe 18 Februari 2011. Naomba nitoe mrejesho kwa muktasari kuhusu ushiriki wangu katika vikao vya mkutano husika wa bunge.

Katika kikao cha kwanza tarehe 8 Februari wakati wa mjadala juu ya Azimio la kufanya Mabadiliko katika Kanuni za Bunge toleo la 2007 niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni 68 (7) kuhusu haja ya kiongozi wa kampi rasmi ya upinzani kupewa nafasi ya kuzungumza na nikatoa hoja kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (b) kwamba mjadala uahirishwe mpaka kwanza kiongozi wa upinzani apewe nafasi ya kuzungumza kama zilivyo mila na desturi za uendeshaji wa Bunge. Spika alilazimika kumpa kiongozi wa upinzani nafasi ya kuzungumza pamoja na kuwa tayari alikuwa amefunga orodha ya wachangiaji hapo awali bila kumpa nafasi. Baada ya hotuba ya kiongozi wa upinzani nilishiriki kutoka bungeni ili kutoshiriki maamuzi ambayo yalilenga kuminya demokrasia ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na pia kutoa fursa kwa wabunge wa chama tawala kuchagua wenyeviti wanaowataka kuwakilisha kambi rasmi ya upinzani kwenye kamati za muhimu za usimamizi wa fedha za umma kinyume na misingi ya utawala bora.

Katika kikao cha tatu tarehe 10 Februari mara baada ya maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni ya 68 (7) kutokana na kauli ya Spika ya kumtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuthibitisha papo kwa papo bungeni juu ya uongo wa Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni 63 (3) (4) na 68 (1). Nilimueleza Spika kwamba Lema hakutumia kanuni 68 (1) ya ‘kuhusu utaratibu’ kama Spika alivyodai bali alitumia kanuni 68 (7) ya kuomba muongozo wa Spika wa hatua gani za kuchukua iwapo kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu analidanganya bunge. Aidha nilimkumbusha Spika kuwa alishatoa muongozo kuwa alete taarifa hivyo hakupaswa kutoa ushahidi wa papo kwa papo. Kauli yangu ilimfanya Spika atoe mwongozo mwingine wa kumtaka Lema awasilishe maelezo yake tarehe 14 Februari katika kikao cha asubuhi.

Katika kikao cha nne tarehe 11 Februari nilitoa mchango wangu wa papo kwa papo bungeni wakati wa hoja ya kujadili Hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge jipya. Katika hotuba hiyo niliwashukuru wananchi na kuzungumzia suala la viongozi kuepuka kupandikiza mbegu ya udini, haja ya kukabaliana na mfumuko wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha, suala la kufufua viwanda na jitihada za kukabiliana na matatizo ya maji katika jimbo la Ubungo. Nilianza hotuba hiyo kwa kuweka katika kumbukumbu za historia namna tulivyoshinda Ubungo kwa nguvu ya umma ya wazee, wanawake na vijana pamoja na vikwazo vya kikatiba na kisheria. Katika hotuba hiyo nimetaka vyombo vya ulinzi na usalama vimshauri Rais na viongozi wengine kuacha kutoa kauli za mara kwa mara ambazo kimsingi ndizo zinazopandikiza udini. Aidha nimeitaka serikali kuwasilisha taarifa ya hali halisi kuhusu mfumuko wa bei na hatua ambazo inapendekeza zichukuliwe ili kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha ambapo kunaweza kuleta migogoro katika taifa. Nilidokeza kuhusu mwelekeo wa kufa kwa kiwanda cha Urafiki Ubungo na kueleza kusudio la kuwasilisha maelezo binafsi kuhusu suala husika. Nilieleza Bunge kuhusu Kongamano la Maji Ubungo na kueleza dhamira yangu ya kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutatua kero husika. Sikuendelea zaidi kwa kutokana na muda wa dakika kumi kuisha hata hivyo niliwasilisha mchango wa ziada wa maandishi kuhusu ufisadi hususani kuhusu Dowans na Kagoda na michezo ikiwemo suala la kurudishwa kwa viwanja vya umma ambavyo vimehodhiwa na chama kimoja baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi ( Bonyeza hapa kusoma hotuba husika: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/hotuba-yangu-bungeni-katika-mkutano-wa.html )

Katika kikao cha tano tarehe 14 Februari mara baada ya kipindi cha maswali na kauli za mawaziri Spika aliruhusu moja kwa moja Hoja ya Kujadili Hotuba ya Rais ya kufungua bunge kuendelea. Nilitaka muongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni 68 (7) na 63 (6) ambayo inatoa fursa ya mbunge kutoa uthibitisho wa ukweli bungeni ili Lema apewe nafasi ya kuwasilisha maelezo yake bungeni katika kipindi hicho cha asubuhi kama alivyoelekeza Spika mwenyewe katika kikao cha tatu. Hata hivyo, Spika alitoa muongozo mpya kuwa Lema awasilishe maelezo na ushahidi wake kwa maandishi ofisini kwake. Katika kikao hicho pia niliuliza swali la nyongeza baada ya majibu ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa Swali namba 65 ambapo nilihoji kwa kuwa waraka wa kutengua utaratibu wa wahitimu wenye stashahada wenye kupaswa kurudia mitihani michache kufanya hivyo wakiwa kazini ulisambazwa ukiwa umechelewa huku wakitakiwa kulipia ada ya mitihani na kujiandaa je serikali iko tayari kutoa muda wa nyongeza zaidi ya uliotangazwa wa mwezi Aprili? Katika majibu yake naibu waziri alieleza kwamba serikali itatoa muda mwingine wa walimu hao kufanya mitihani yao ikiwa wakishindwa kufanya mwezi Aprili hata hivyo serikali iliwahimiza wafanye hivyo wakati huu ili kuepuka ushindani wa nafasi za ajira utakaokuwepo kipindi kijacho.

Katika kikao cha sita tarehe 15 Februari mara baada ya kauli za Mawaziri ambapo Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya umeme nchini na utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi kifupi na cha kati nilitoa hoja ya dharura kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (e) na kanuni ya 47 ili bunge lijadili jambo la dharura la mgawo wa umeme unaolikumba taifa. Nilitaka jambo hilo lijadiliwe kwa kutoa maelezo ya namna linavyowathiri maisha ya wananchi waliowengi na pia kuathiri uchumi wa taifa. Pia, nilieleza kwamba katika kauli yake Waziri ameeleza hatua za dharura zinazotaka kuchukuliwa na serikali ambazo nyingine kimsingi sio za dharura na pia zinahusisha matumizi makubwa ya fedha za wananchi ambazo nilizikadiria kuwa ni zaidi ya bilioni 300 nje ya bajeti ya serikali hivyo ni muhimu bunge likajadili. Spika wa Bunge akaikataa hoja hiyo pamoja na kuwa iliungwa mkono na idadi ya wabunge inayohitajika badala yake akanitaka kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nikazungumzie mambo hayo kwenye kikao cha kamati husika hapo baadaye. Kimsingi nilitaka suala hilo lijadiliwe kwa sababu katika maelezo yake Waziri alitaja kuwa serikali inakusudia kukodi mitambo ya dharura ya MW 260 (hii ni mitambo ambayo gharama yake ni kubwa sana, na inaweza kuchelewa isije wakati wa dharura kama ilivyokuwa kwenye sakata la Richmond), pia Waziri hakuzungumzia kabisa kuhusu mitambo ya Dowans ambayo asubuhi ya siku hiyo nilizungumza LIVE na TBC1 na kutaka serikali iitaifishe mitambo husika kwa kutumia sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo ili iiwashe kwa dharura na kupunguza pengo la MW 120 wakati taifa likiendelea kufanya maamuzi ya namna ya kufidia kiwango kitachobaki. Aidha mjadala huo ungewezesha pia kutaka waziri awajibike kwa kutochukua hatua za mapema za kukabiliana na kinachoitwa dharura ambacho kilishafahamika toka mwaka 2006, 2008 na 2009 na maamuzi ya kuondokana na hali hiyo yakafanyika lakini hayakutekelezwa kwa wakati ( Bonyeza hapa kwa kauli ya awali kuhusu Dowans na mgawo wa umeme: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/mitambo-ya-dowans-itaifishwe-waziri.html)

Katika kikao cha saba tarehe 18 Februari niliuliza Swali la Nyongeza kutokana na majibu ya Swali namba 85 kwa Wizara ya Maji. Kwenye swali langu la Nyongeza kwanza nilimkosoa Naibu Waziri kwa kutaja majina ya miradi ya maji ambayo iko Kigamboni na kueleza kwamba ni ya Ukonga na kumweleza Naibu Waziri kuwa pamoja na uwekezaji wa fedha za miradi ya maji za Benki ya Dunia na Wadau wengine wa maendeleo kwenye Ruvu Juu na Ruvu chini ikiwemo kuweka mtandao mpya wa mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya wachina; bado maji kwenye kata za Kwembe, Kibamba, Msigani, Mbezi, Saranga, Kimara nk maji hayatoki kwa pamoja na mambo mengine upotevu wa maji na wafanyabiashara wanauza maji bei juu kujiunganishia kinyemela; je Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa? Naibu Waziri alijibu kwa kunipongeza kwa kuweka kipaumbele cha kwanza suala la maji katika kazi zangu na kuahidi kutembelea miundombinu husika kwa kushirikiana nami. Pia, niliuza Swali namba 91 kwa niaba ya Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi kwa Wizara ya Fedha kuhusu kero za upatikanaji wa mafao ya wastaafu na mirathi kwa watumishi waliokufa kazini. Baada ya majibu ya Waziri kueleza kwamba sababu ni matatizo ya mawasiliano ukiwemo udhaifu katika mfumo wa kumbukumbu kwa upande wa watumishi wanaohudumiwa na mifuko; niliuliza maswali mawili ya nyongeza, moja kuhusu namna ambavyo serikali imepanga kuondokana na matatizo hayo ya mawasiliano na kumbukumbu hasa kwa kuwa wapo wastaafu na marehemu ambao kumbukumbu zao zote zimekamilika lakini bado kuna kero nyingi katika kupata mafao na mirathi. Pili, niliuliza swali la kutaka tamko la serikali kuhusu wastaafu wengine ambao hawahudumiwi na mifuko kama wale wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki ambao mpaka sasa wanahangaika kuhusu mafao yao. Serikali ilijibu kuwa haina tamko la kutoa kwa sasa kwa kuwa inasubiri kwamba suala la Wastaafu wa Afrika Mashariki lipangiwe jaji mwingine katika mahakama ya rufaa kama walivyoomba.

Kwa muktasari huo ni mrejesho kuhusu ushiriki wangu ndani ya vikao vya mkutano wa pili wa bunge la kumi. Hata hivyo, kuna masuala mengine yanayohusu ushiriki wangu katika shughuli nyingine za kibunge nje ya vikao kwa nafasi zangu zingine kama Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA, Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam, Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo, Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani-Nishati na Madini na nafasi nyinginezo ambayo sijayaeleza katika taarifa hii. Nawashukuru sana wote walitoa maoni kwenye Mikutano ya Mbunge kuwasikiliza na kuzungumza na Wananchi tuliyoifanya Mbezi mwisho na Manzese Bakhresa siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano wa pili wa bunge, sehemu ya masuala mliyonituma nimeyawasilisha. Hata hivyo yako mengine kutokana na ufinyu wa muda na kubanwa na kanuni sikupata wasaa wa kuyawasilisha ikiwemo suala la hoja ya mchakato wa katiba mpya ambalo nililitolea kauli ya tahadhari baada ya serikali kukubaliana nami mchakato husika kuanzia bungeni kwa kutungwa kwa sheria (Rejea kauli yangu ifuatayo: JOHN MNYIKA: Tahadhari kuhusu serikali kupeleka muswada wa katiba mpya bungeni). Nawashukuru kwa kuniunga mkono.

Tuendelee kuwasiliana, kushauriana na kushirikiana.



Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (MB)

0 comments:

Post a Comment