Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akitoa salamu za chama hicho kwa Familia ya Mwalimu Nyerere, wakati vongozi mbali mbali na wabunge wa chama hicho, walipomtembela Mama Maria Nyerere (katikati) nyumbani kwake Butiama jana. Kulia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilibrod Slaa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, akiweka shada la maua kwenye kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati viongozi mbalimbali wa chama hicho walipomtembelea Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Butiama hii leo.
Mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), akiweka shada la maua katika kaburi la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati viongozi na baadhi ya wabunge wa chama hicho, walipomtembelea Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Butiama leo. (Picha na Joseph Senga)
Mama Maria Nyerere akiteta jambo na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, wakati viongozi wa Chama hicho na baadhi ya wabunge, walipomtembelea nyumbani kwake Butiama
Monday, February 28, 2011
CHADEMA WATEMBELEA BUTIAMA
Uthibitisho wa Mhe. Lema kuhusu Pinda kuongea uongo Bungeni
Maelezo ya uthibitisho ya Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema (mbunge) juu ya kauli ya uwongo iliyotolewa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo P.K. Pinda (mbunge) wakati akijibu maswali kwa Waziri Mkuu katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 10 Februari, 2011
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, nilikuomba “kupata ufafanuzi kwamba Mbunge anaweza akachukua hatua gani kama anaona mtu mwenye nafasi kubwa katika nchi kama Waziri Mkuu analidanganya taifa na kulidanganya Bunge.” Badala ya kunipatia ufafanuzi niliouomba, Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ifuatayo, kwa mujibu wa Hansard hiyo: “Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili lazima liwe na adabu inayostahili. Kwa hiyo kama tutafanya Bunge letu hili ikawa ni mahali, sasa unataka kusema Waziri Mkuu kwa ahadi aliyoweka ndani ya Bunge hili anadanganya? Kama anadanganya naomba ukaiandike vizuri kabisa kuhusu kudanganya kwake, halafu nitakuambia tufanye nini.”
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelekezo hayo ya awali, ulitoa maelekezo ya ziada kwamba “nampa mpaka tarehe 14 asubuhi alete maandiko ya kuthibitisha maneno aliyoyasema…. Kwa hiyo tarehe 14 kipindi cha asubuhi atoe maelezo ya kwamba Waziri Mkuu amesema uongo. Maana yake alichosema kwamba Waziri Mkuu amesema uongo sasa anataka tumpe Mwongozo wa namna ya kufanya na akasema aandike. Sasa kifungu hiki cha 64 kinamdai alete maelezo hayo mpaka tarehe 14.”
Mheshimiwa Spika,
Maneno yote ya Hansard niliyoyanukuu hapo juu yanathibitisha kwamba mimi sikusema Waziri Mkuu amesema uongo, bali niliomba mwongozo wa Spika kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Mbunge endapo kiongozi wa ngazi za juu kama Waziri Mkuu atasema uongo au kulidanganya Bunge. Hata hivyo, kwa vile umenielekeza nitoe maelezo uthibitisho kwamba Waziri Mkuu alisema uongo au kulidanganya Bunge, na kwa kutimiza maelekezo yako, naomba sasa nithibitishe kwamba kauli ya Waziri Mkuu kuhusu matukio yaliyopelekea mauaji ya wananchi wa Arusha na Mbarali yalikuwa ya uongo na kwamba Waziri Mkuu alilidanganya Bunge.
1. UONGO WA KWANZA
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu amenukuliwa kwenye Hansard ya tarehe 10 Februari 2011 akidai kwamba “… tumepoteza maisha ya Watanzania watatu bila sababu.” Huu ni uongo wa kwanza wa Waziri Mkuu Bungeni. Ukweli ni kwamba waliopoteza maisha ni Watanzania wawili – Dennis Michael Shirima na Ismail Omari – na Mkenya mmoja aliyejulikana kwa jina la Paul Njuguna.
2. UONGO WA PILI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, Waziri Mkuu alitamka maneno yafuatayo kuhusu suala la maandamano ya Arusha: “Mliomba wenyewe mfanye maandamano, hatukukataa, mkakaa na askari pale mkaelewana vizuri. Mkakubaliana kwamba sisi tunafikiri ili tuweze kuwadhibiti vizuri na kuwalinda vizuri, tutumie route moja tu. Wenzangu nyie mkakataa.” Kauli mbili za mwisho kwamba zina maana kwamba Jeshi la Polisi lilipendekeza kwamba njia moja ya maandamano ndiyo itumike na kwamba viongozi wa CHADEMA walikataa pendekezo hilo. Kauli hiyo, Mheshimiwa Spika, ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kulidanganya Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Ukweli wa jambo hili ni kwamba tarehe 31 Desemba 2010, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini alitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20/10 yenye kichwa cha habari: “TAARIFA YA MAANDAMANO NA MKUTANO WA HADHARA TAREHE 5 JANUARI 2011.” Sehemu ya barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwamba “… CHADEMA (Wilaya ya Arusha Mjini) tutakuwa na maandamano ya amani tarehe 5 Januari 2011 yatakayohitimishwa na mkutano wa hadhara katika viwanja wa NMC – unga Ltd.” Aidha, barua hiyo ilipendekeza njia ifuatayo ya maandamano hayo: “Maandamano hayo yataanzia maeneo ya Phillips saa NNE asubuhi, kuelekea Sanawari, Mianzini, Stand Kuu kuelekea Mnara wa Azimio, kupitia Polisi – Manispaa – Clock Tower kushukia Sokoine Road, kasha Friends’ Corner na kuingia viwanja vya NMC.” Nakala ya taarifa hiyo ya CHADEMA kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha Mjini imeambatanishwa katika maelezo haya kama Kielelezo ‘A.’
Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 2 Januari 2011, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini alimwandikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini barua nyingine yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20.1/11 ambapo alimjulisha kwamba “msafara wetu utabaki kama tulivyoainisha kwenye barua (ya tarehe 31 Desemba 2010.)” Vile vile barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya juu ya “… vituo maalumu vya wananchi kukutana ili baada ya hapo waweze kujiunga na maandamano (msafara mkuu).” Nakala ya barua ya tarehe 2 Januari 2011 nayo imeambatanishwa kama Kielelezo ‘B’ kwenye maelezo haya.
Kwa ushahidi huu wa maandishi, ni wazi kwa hiyo kwamba kauli ya Waziri Mkuu kwamba Jeshi la Polisi la Wilaya ya Arusha Mjini ndio waliopendekeza njia ya maandamano ilikuwa ni ya uongo na/au ililenga kulidanganya Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Mnamo tarehe 3 Januari 2011 viongozi wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini walikutana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha ili kujadili masuala mbali mbali yanayohusu maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 5 Januari. Moja ya mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ndani ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa ilikuwa ni kuchagua njia muafaka zaidi ya maandamano hayo. Kufuatia mazungumzo hayo, mnamo tarehe 4 Januari 2011 Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha SSP Zuberi Mwombeji alimwandikia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini kumjulisha kwamba “kimsingi mmekubaliwa kufanya maandamano na mkutano wenu wa hadhara tarehe 5 Januari 2011….”
Katika barua hiyo, Mkuu wa Polisi aliitaka CHADEMA ichague moja kati ya njia mbili za maandamano ambazo zilijadiliwa na kukubaliwa katika mkutano wa tarehe 3 Januari, yaani njia ya “kuanzia Phillips, Sanawari Mataa, kushuka na barabara ya AICC, Goliondoi, Sokoine Road, Friends Corner na kuingia uwanja wa NMC”; au “kuanzia Phillips, sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stand, CRDB Bank, Friends’ Corner hadi uwanja wa NMC.” Nakala ya barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya yenye kumb. Na. AR/B.5/VOL.II/63 imeambatanishwa kama Kielelezo ‘C’ kwenye maelezo haya. Siku hiyo hiyo ya tarehe 4 Januari 2011 Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya alimtaarifu Mkuu wa Polisi Wilaya kwamba maandamano yangepitia njia ya Phillips, Sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stendi Kuu ya Mabasi, CRDB Bank, Friends’ Corner na kuingia viwanja wa NMC – Unga Ltd.
Kufuatana na mtiririko huu wa matukio, sio kweli kwamba Polisi ndio waliopendekeza njia ya maandamano na wala sio kweli kwamba CHADEMA walikataa njia hiyo iliyopendekezwa na Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba Polisi walipendekeza njia ya maandamano na CHADEMA wakaikataa ilikuwa ni kauli ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge.
3. UONGO WA TATU
Mheshimiwa Spika,
Aya ya tatu ya kauli ya Waziri Mkuu inadai kwamba Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA kihalali lakini CHADEMA wakaamua “… kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe.” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kudanganya Bunge. Kwanza kabisa, utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga marufuku maandamano ulikuwa ni ukiukaji wa sheria husika za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi, mara baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, njia pekee halali ya kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Sheria hiyo inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano wa hadhara hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo “isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.”
Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma katika eneo husika.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa ni lazima itolewe na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na ni lazima iwe ni ya maandishi. CHADEMA haijawahi kupokea wala kuonyeshwa amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ya kupiga marufuku maandamano ambayo Mkuu huyo huyo wa Polisi wa Wilaya alikuwa ameyaruhusu kwa maandishi! Aidha, tumeona taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011 ambayo imedai kwamba CHADEMA iliandikiwa barua yenye kumb. Na. ARR/B.5/1/VOL.VIII/24 ya tarehe 4 Januari 2011 iliyoandikwa na “Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa mujibu wa sheria … kusitisha maandamano hayo ya CHADEMA….” Madai hayo hayana ukweli wala msingi wowote kisheria kwa sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote kisheria ya kusitisha au kupiga marufuku maandamano au mikutano ya hadhara. Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni ‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!
Aidha, tuna taarifa kwamba jioni ya tarehe 4 Januari 2011 Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na hautambuliwi kabisa na sheria hizo!
Mheshimiwa Spika,
Hata kama ‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza kuchukuliwa kisheria na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye amani na utulivu.’ Swali la kumuuliza Waziri Mkuu hapa ni kwamba kama kweli kulikuwa na ‘taarifa za kiintelijensia’ za uwezekano wa uvunjifu wa amani, kwa nini Jeshi la Polisi lililokuwa na taarifa hizo halikutoa ulinzi wa kutosha kwa waandamanaji?
Mheshimiwa Spika,
Hata kama maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Aidha, kwa mujibu ibara ya 64(5) ya Katiba, “… Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka mashrti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.” Hii ina maana kwamba hata kama Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu Jeshi la Polisi kukataza na/au kusitisha maandamano, Sheria hizo zitakuwa ni batili kwa kiasi cha ukiukwaji wao wa masharti ya ibara ya 20(1) ya Katiba inayotoa uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.
4. UONGO WA NNE
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa nne aliousema Waziri Mkuu unahusu sababu ya kusitishwa kwa maandamano ya amani ya tarehe 5 Januari 2011. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka: “Sasa mkaamua kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe. Mheshimiwa Spika, sasa kilichotokea pale ni namna ya kuzuia hayo maandamano....” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo kwa sababu inapingana moja kwa moja na taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Jeshi la Polisi lilichukua hatua ya kuwaamuru waandamanaji kusitisha maandamano hayo mara moja baada ya kuona kwamba yataleta uvunjifu wa amani kutokana na jazba ya waandamanaji hao.” Wakati Waziri Mkuu – ambaye hakuwepo Arusha - anadai Bungeni kwamba maandamano yalisitishwa kwa sababu yalikiuka utaratibu, Jeshi la Polisi – lililokuwa na mamia ya askari polisi kwenye eneo la tukio – linasema kwenye taarifa rasmi kwamba maandamano hayo yalisitishwa kwa sababu ya jazba ya waandamanaji!. Taarifa ya IGP kama kielelezo “D”
5. UONGO WA TANO
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa tano wa Waziri Mkuu unahusu kauli yake juu ya umbali kati ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha na mahali walipouawa waandamanaji watatu na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka yafuatayo kuhusu jambo hili: “Mpaka mmekaribia mita 50 muweze kuingia kituo cha Polisi. Police was left with no option kwa kujua tu kwamba kama mkiingia hatujui litakalotokea ni kitu gani. Katika purukushani ile, masikini wale marehemu wale watatu wakapoteza maisha.”
Kwa mara nyingine tena kauli ya Waziri Mkuu Bungeni inapingana na kauli ya Jeshi la Polisi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi hilo, “walipokaribia kituo Kikuu cha Polisi cha Kati umbali wa kama mita 50 huku wakirusha mawe, chupa, fimbo, nondo, mapanga na visu, amri halali na tahadhari za msingi zilizotolewa kuwataka watawanyike mara moja. Wafuasi hao walikaidi amri na kuzidi kukaribia kituo kwa lengo la kutimiza azma yao ya kukivamia.” Hapa maana ni kwamba waandamanaji walishapita huo umbali wa mita 50! Baada ya hapo, kufuatana na taarifa ya Jeshi la Polisi, hatua zifuatazo zilichukuliwa:
(i) Hatua ya kwanza, yalipigwa mabomu ya machozi, onyo ambalo lilipuuzwa na wakaendelea kusonga mbele;
(ii) Hatua ya pili, zilitumika risasi za baridi na mabomu ya vishindo bado walikaidi na kuzidi kukaribia kituo cha Polisi;
(iii) Hatua ya tatu, zilipigwa risasi juu za onyo bado wakaendelea kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya hatua zote hizo kushindikana kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, “kilichofuatia ni mapambano ya ana kwa ana kati ya askari na waandamanaji waliokuwa wakisonga mbele kuvamia kituo. Katika mazingira hayo risasi za moto ililazimika kutumika. Matokeo ya tafrani hiyo, watu 14 walijeruhiwa na kufikishwa hospitalini ambapo watatu kati yao walifariki dunia wakipatiwa matibabu.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ni kweli hatua zote zilizoelezwa hapo juu zilichukuliwa na Jeshi la Polisi basi ni wazi kwamba watu waliouawa au kujeruhiwa waliuawa au kujeruhiwa kwenye uzio au mlango wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha! Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa kauli ya Waziri Mkuu, taarifa ya Jeshi la Polisi vile vile ni ya uongo mtupu. Kwa ushahidi wa picha za video tulio nao, marehemu mmoja aliuawa kwenye eneo la Mianzini ambalo liko zaidi ya kilometa tatu kutoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha. Aidha, marehemu wa pili alipigiwa risasi katika eneo la Kaloleni ambalo nalo liko zaidi ya kilometa moja kutoka kituo hicho. Ushahidi wa video unaungwa mkono na ushahidi wa watu walioshuhudia mauaji hayo wenyewe.
6. UONGO WA SITA
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa sita wa Waziri Mkuu unatokana na kauli yake kwamba “... kama Mheshimiwa Mbowe na chama chako mngeliamua kushirikiana na Serikali hii mkafanya ule mkutano kama tulivyokubaliana haya yote yasingetokea.” Ukweli ni kwamba mkutano wenyewe uliohutubiwa na Dr. Wilbrod Slaa na Mheshimiwa Philemon Ndesamburo ulishambuliwa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwashawasha na kutawanywa kabla ya makundi ya watu kurudi kwenye mkutano na Dr. Slaa na Mheshimiwa Ndesamburo kuendelea kuhutubia!
Aidha, ushahidi wa maandishi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha unaonyesha wazi kwamba CHADEMA walikubaliana na matakwa ya Jeshi la Polisi kwa kuchagua njia moja ya maandamano. Hata viongozi waliokamatwa wakati wa maandamano hayo walikamatiwa kati ya eneo la Sanawari na Mianzini wakiandamana kwa kutumia moja ya njia zilizopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya! Na gari iliyokuwa imewabeba Mheshimiwa Lucy Owenya na mke wa Dr. Slaa ilishambuliwa na kuvunjwa vioo na Mheshimiwa Owenya na Mama Slaa kuumizwa na askari polisi katika eneo la Sanawari Mataa wakati wakiwa katika njia ya maandamano iliyopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba, waliovunja makubaliano juu ya maandamano na mkutano wa hadhara walikuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Thobias Andengenye na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema walioamua kuingilia maamuzi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha na kuyapiga marufuku maandamano hayo.
7. UONGO WA SABA
Mheshimiwa Spika,
Katika jibu lake kwa swali la Mheshimiwa Martha Umbulla, Waziri Mkuu alidai kwamba mkutano wa Baraza la Madiwani wa kumchagua Meya, Naibu Meya na Wenyeviti wa Kamati ulianza “wajumbe wote 31 wakiwepo....” Hii ni kauli ya uongo. Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Mikutano na Shughuli za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha za 2003, “kila mjumbe anayehudhuria mkutano wa Halmashauri au Kamati yoyote ya Halmashauri ambamo yeye ni mjumbe ataweka sahihi yake kwenye Rejesta ya mahudhurio inayotunzwa na Mkurugenzi kwa ajili hiyo.” Kwa kufuatana na orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 17 Desemba, walikuwepo madiwani 16 wote wakiwa madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM)!
Kwa Waziri Mkuu kusimama na kuliambia Bunge kwamba wajumbe wote 31 wa Halmashauri ya Jiji la Arusha walikuwepo tarehe 17 Desemba 2010 wakati Rejesta ya mahudhurio inaonyesha kwamba ni wajumbe 16 tu ndio walioweka sahihi zao kwenye Rejesta hiyo ni uongo wa wazi. Angalia Kielelezo “E”
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu alitoa kauli ya uongo tena pale aliposema kwamba mgombea wa CCM alishinda kura za meya “walikuwa wanashindana mmoja wa CHADEMA, mmoja wa CCM.” Kwa mujibu wa orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 18 Desemba 2010 uliomchagua Meya, waliokuwepo ni madiwani 17 ambao kati yao, 16 walikuwa wa CCM na mmoja alitoka chama cha TLP. Hakukuwepo na mjumbe hata mmoja wa CHADEMA. Na hii haishangazi kwa sababu ratiba ya mkutano huo inaonyesha kwamba siku ya tarehe 18 Desemba 2010 ilitakiwa kuwa siku ya mafunzo ya Madiwani yaliyokuwa yafanyike Olasiti Garden. Madiwani wa CHADEMA ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa tarehe 17 Desemba wasingeweza kujua kwamba ratiba ya mafunzo ilikuwa imebadilishwa na kuwa ratiba ya uchaguzi wa Meya! Ratiba ya shughuli za tarehe 18.12.2010 kielelezo “F”
8. UONGO WA NANE
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa nane wa Waziri Mkuu ni kauli yake kwamba “... utaratibu uliofuatwa ulikuwa sahihi kabisa, haukukosewa kitu chochote. Meya ni halali kabisa, alipatikana kihalali kabisa.” Huu ni uongo mtupu. Chini ya kanuni ya 8(3) ya Kanuni za Halmashauri, “akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na mkutano wa kwanza wa Halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri.” Kwa kusoma kanuni ya 8(3) pamoja na kanuni ya 9, ni wazi kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wanatakiwa kuchaguliwa na mkutano wa kwanza wa Halmashauri. Ili kukidhi matakwa ya kanuni hizi, mkutano wa uchaguzi wa Meya na Makamu Meya wa Arusha ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri hiyo. Kwa maana hiyo, mkutano wa tarehe 18 Desemba haukuwa mkutano halali na viongozi wa Halmashauri waliochaguliwa na mkutano huo hawawezi kuwa halali!
9. UONGO WA TISA
Mheshimiwa Spika,
Uongo wa tisa aliousema Waziri Mkuu Bungeni uko kwenye kauli ifuatayo: “Mheshimiwa Spika, yaani hata kwa hesabu tu za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza hakuna namna ambavyo kwa hali ilivyokuwa kwamba mna CHADEMA wajumbe 14, una CCM 16 utashindaje?” Hapa Waziri Mkuu alitaka kuaminisha Bunge kwamba hata kama wajumbe wa CHADEMA wangehudhuria kwenye mkutano huo bado wasingeshinda kwa sababu wajumbe wa CCM walikuwa wengi zaidi ya wajumbe wa CHADEMA. Lakini kwenye hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu alitoa kauli ifuatayo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha: “Wakaingia awamu ya pili ya kumtafuta Naibu Meya, wakapiga kura, Mjumbe wa kutoka TLP akashinda, CCM alishindwa hakupata kura hata moja, CHADEMA hawakupata kura hata moja...”!
Mheshimiwa Spika,
Kwa akili za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza kama iliwezekana kwa mgombea wa TLP ambaye yuko peke yake katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupata kura za wajumbe wote wa CCM na kumshinda mgombea wa CCM ambaye – kwa kauli ya Waziri Mkuu – hakupata kura hata moja, je, ingeshindikanaje kwa mgombea wa CHADEMA yenye wajumbe 14 kushinda? Swali ni muhimu hasa hasa kwa vile chini ya kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha inasema kwamba kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wake itakuwa ni ya siri! Na kama inavyofahamika, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeshinda pamoja na kwamba CCM ina wajumbe wengi zaidi katika Halmashauri hiyo!
10. UONGO WA KUMI
Mheshimiwa Spika,
Waziri Mkuu aliulizwa swali la nyongeza na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kama Serikali iko tayari kuunda tume ya uchunguzi ya kimahakama kutafuta ukweli wa matukio ya Arusha na “... vile vile kuchukua hatua kwa wale wanaohusika.” Swali hilo liliulizwa pia na Mheshimiwa Martha J. Umbulla aliyetaka kujua kama Serikali itachukua hatua kuwaadhibu CHADEMA kwa kile alichokiita kuhusika na vurugu za Arusha “... ili tukio kama hilo lisirudie katika chaguzi za nchi yetu?” Waziri Mkuu alijibu: “Mimi nadhani hili ... wala si suala pengine la kusema ichukue hatua dhidi ya CHADEMA hapana.” Waziri Mkuu alitilia mkazo kwamba Serikali haina mpango wa kuwachukulia hatua CHADEMA kwa kusema: “Nataka niwaombe sana, hili hatuwezi kama Serikali tukasema tutaichukulia hatua CHADEMA....”. Angalia hansard ya tarehe 10-02-2011 kielelezo “G”
Mheshimiwa Spika,
Watanzania wawili na raia wa nchi jirani na yenye uhusiano mzuri na nchi yetu waliuawa wakati wa vurugu za Arusha. Watu wengine wengi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, mabomu, virungu na mabuti ya polisi. Kama taarifa za Jeshi la Polisi na kauli ya Waziri Mkuu ni za kweli, vurugu hizo zilihusisha pia mashambulizi na uharibifu wa mali za Serikali kama vile vituo vya Polisi na mali za watu binafsi na za vyama vya siasa hususan CCM. Aidha, kama kauli ya Jeshi la Polisi nay a Waziri Mkuu ni za kuaminiwa, madhara yote haya yalitokana na uchochezi uliofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA na ambao wametajwa kwa majina.
Mheshimiwa Spika,
Kama yote haya ni ya kweli na sio porojo za kisiasa, Watanzania wanapaswa kuambiwa ni kwa nini Serikali hii haiko tayari kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na matukio haya? Kwa nini Serikali imeamua kwamba ni busara kuwafungulia mashtaka ya kosa dogo la kufanya maandamano kinyume cha sheria badala ya kuwashtaki kwa makosa makubwa kama kusababisha mauaji, au uchochezi, au kujaribu kuchoma majengo moto au makosa ya aina hiyo ambayo yana adhabu kubwa zaidi ya kosa waliloshtakiwa nalo? Kukataa kuchukua hatua stahili kuna tafsiri moja tu: CHADEMA hawakuhusika katika vurugu za Arusha na kwa hiyo kauli ya Waziri Mkuu Bungeni ni ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge!
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kanuni ya 63(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, inasema “… ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu.” Hii pia ni msingi wa kanuni ya 64(1)(a) ya Kanuni za Bunge.
Kama nilivyothibitisha katika maelezo haya, Waziri Mkuu amesema uongo na/au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli Bungeni. Kanuni ya 63(5) inaelekeza cha kufanya inapothibitika kuwa Mbunge amesema uongo Bungeni: “Spika au Mbunge mwingine yeyote, baada ya kutoa maelezo mafupi ya ushahidi unaotilia mashaka ya dhahiri kuhusu ukweli wa kauli au usemi au maelezo juu ya jambo au suala ambalo Mbunge amelisema Bungeni, anaweza kumdai Mbunge huyo atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo.” Naomba kuchukua nafasi hii kumtaka Waziri Mkuu atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake Bungeni siku ya tarehe 10 Februari 2011 na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo na kutubu kwa Mungu!
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha!
Godbless Jonathan Lema
Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini
Sunday, February 27, 2011
CHADEMA Kuzuru Kaburi la Baba wa Taifa
Vikosi leo vitaelekea Tarime, Rorya, Bunda, Serengeti, Mwibara na Musoma Vijijini.
Hauna Kulala Mpaka Kieleweke.
Thursday, February 24, 2011
Wednesday, February 23, 2011
Tuesday, February 22, 2011
Mrejesho kuhusu Uwakilishi Wangu katika Mkutano wa pili wa Bunge
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2) Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi ya kuishauri na kuisimamia serikali. Katika kutimiza wajibu huu kwa nafasi yangu ya ubunge wa Jimbo la Ubungo niliwawakilisha wananchi wenzangu kwenye Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi ulioanza tarehe 8 Februari na kuahirishwa tarehe 18 Februari 2011. Naomba nitoe mrejesho kwa muktasari kuhusu ushiriki wangu katika vikao vya mkutano husika wa bunge.
Katika kikao cha kwanza tarehe 8 Februari wakati wa mjadala juu ya Azimio la kufanya Mabadiliko katika Kanuni za Bunge toleo la 2007 niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni 68 (7) kuhusu haja ya kiongozi wa kampi rasmi ya upinzani kupewa nafasi ya kuzungumza na nikatoa hoja kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (b) kwamba mjadala uahirishwe mpaka kwanza kiongozi wa upinzani apewe nafasi ya kuzungumza kama zilivyo mila na desturi za uendeshaji wa Bunge. Spika alilazimika kumpa kiongozi wa upinzani nafasi ya kuzungumza pamoja na kuwa tayari alikuwa amefunga orodha ya wachangiaji hapo awali bila kumpa nafasi. Baada ya hotuba ya kiongozi wa upinzani nilishiriki kutoka bungeni ili kutoshiriki maamuzi ambayo yalilenga kuminya demokrasia ya kambi rasmi ya upinzani bungeni na pia kutoa fursa kwa wabunge wa chama tawala kuchagua wenyeviti wanaowataka kuwakilisha kambi rasmi ya upinzani kwenye kamati za muhimu za usimamizi wa fedha za umma kinyume na misingi ya utawala bora.
Katika kikao cha tatu tarehe 10 Februari mara baada ya maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu niliomba muongozo wa Spika kwa kurejea kanuni ya 68 (7) kutokana na kauli ya Spika ya kumtaka Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kuthibitisha papo kwa papo bungeni juu ya uongo wa Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni 63 (3) (4) na 68 (1). Nilimueleza Spika kwamba Lema hakutumia kanuni 68 (1) ya ‘kuhusu utaratibu’ kama Spika alivyodai bali alitumia kanuni 68 (7) ya kuomba muongozo wa Spika wa hatua gani za kuchukua iwapo kiongozi mkubwa kama Waziri Mkuu analidanganya bunge. Aidha nilimkumbusha Spika kuwa alishatoa muongozo kuwa alete taarifa hivyo hakupaswa kutoa ushahidi wa papo kwa papo. Kauli yangu ilimfanya Spika atoe mwongozo mwingine wa kumtaka Lema awasilishe maelezo yake tarehe 14 Februari katika kikao cha asubuhi.
Katika kikao cha nne tarehe 11 Februari nilitoa mchango wangu wa papo kwa papo bungeni wakati wa hoja ya kujadili Hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge jipya. Katika hotuba hiyo niliwashukuru wananchi na kuzungumzia suala la viongozi kuepuka kupandikiza mbegu ya udini, haja ya kukabaliana na mfumuko wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha, suala la kufufua viwanda na jitihada za kukabiliana na matatizo ya maji katika jimbo la Ubungo. Nilianza hotuba hiyo kwa kuweka katika kumbukumbu za historia namna tulivyoshinda Ubungo kwa nguvu ya umma ya wazee, wanawake na vijana pamoja na vikwazo vya kikatiba na kisheria. Katika hotuba hiyo nimetaka vyombo vya ulinzi na usalama vimshauri Rais na viongozi wengine kuacha kutoa kauli za mara kwa mara ambazo kimsingi ndizo zinazopandikiza udini. Aidha nimeitaka serikali kuwasilisha taarifa ya hali halisi kuhusu mfumuko wa bei na hatua ambazo inapendekeza zichukuliwe ili kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha ambapo kunaweza kuleta migogoro katika taifa. Nilidokeza kuhusu mwelekeo wa kufa kwa kiwanda cha Urafiki Ubungo na kueleza kusudio la kuwasilisha maelezo binafsi kuhusu suala husika. Nilieleza Bunge kuhusu Kongamano la Maji Ubungo na kueleza dhamira yangu ya kuendelea kushirikiana na Wizara katika kutatua kero husika. Sikuendelea zaidi kwa kutokana na muda wa dakika kumi kuisha hata hivyo niliwasilisha mchango wa ziada wa maandishi kuhusu ufisadi hususani kuhusu Dowans na Kagoda na michezo ikiwemo suala la kurudishwa kwa viwanja vya umma ambavyo vimehodhiwa na chama kimoja baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi ( Bonyeza hapa kusoma hotuba husika: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/hotuba-yangu-bungeni-katika-mkutano-wa.html )
Katika kikao cha tano tarehe 14 Februari mara baada ya kipindi cha maswali na kauli za mawaziri Spika aliruhusu moja kwa moja Hoja ya Kujadili Hotuba ya Rais ya kufungua bunge kuendelea. Nilitaka muongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni 68 (7) na 63 (6) ambayo inatoa fursa ya mbunge kutoa uthibitisho wa ukweli bungeni ili Lema apewe nafasi ya kuwasilisha maelezo yake bungeni katika kipindi hicho cha asubuhi kama alivyoelekeza Spika mwenyewe katika kikao cha tatu. Hata hivyo, Spika alitoa muongozo mpya kuwa Lema awasilishe maelezo na ushahidi wake kwa maandishi ofisini kwake. Katika kikao hicho pia niliuliza swali la nyongeza baada ya majibu ya Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa Swali namba 65 ambapo nilihoji kwa kuwa waraka wa kutengua utaratibu wa wahitimu wenye stashahada wenye kupaswa kurudia mitihani michache kufanya hivyo wakiwa kazini ulisambazwa ukiwa umechelewa huku wakitakiwa kulipia ada ya mitihani na kujiandaa je serikali iko tayari kutoa muda wa nyongeza zaidi ya uliotangazwa wa mwezi Aprili? Katika majibu yake naibu waziri alieleza kwamba serikali itatoa muda mwingine wa walimu hao kufanya mitihani yao ikiwa wakishindwa kufanya mwezi Aprili hata hivyo serikali iliwahimiza wafanye hivyo wakati huu ili kuepuka ushindani wa nafasi za ajira utakaokuwepo kipindi kijacho.
Katika kikao cha sita tarehe 15 Februari mara baada ya kauli za Mawaziri ambapo Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli ya serikali kuhusu hali ya umeme nchini na utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi kifupi na cha kati nilitoa hoja ya dharura kwa mujibu wa kanuni 55 (3) (e) na kanuni ya 47 ili bunge lijadili jambo la dharura la mgawo wa umeme unaolikumba taifa. Nilitaka jambo hilo lijadiliwe kwa kutoa maelezo ya namna linavyowathiri maisha ya wananchi waliowengi na pia kuathiri uchumi wa taifa. Pia, nilieleza kwamba katika kauli yake Waziri ameeleza hatua za dharura zinazotaka kuchukuliwa na serikali ambazo nyingine kimsingi sio za dharura na pia zinahusisha matumizi makubwa ya fedha za wananchi ambazo nilizikadiria kuwa ni zaidi ya bilioni 300 nje ya bajeti ya serikali hivyo ni muhimu bunge likajadili. Spika wa Bunge akaikataa hoja hiyo pamoja na kuwa iliungwa mkono na idadi ya wabunge inayohitajika badala yake akanitaka kama Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nikazungumzie mambo hayo kwenye kikao cha kamati husika hapo baadaye. Kimsingi nilitaka suala hilo lijadiliwe kwa sababu katika maelezo yake Waziri alitaja kuwa serikali inakusudia kukodi mitambo ya dharura ya MW 260 (hii ni mitambo ambayo gharama yake ni kubwa sana, na inaweza kuchelewa isije wakati wa dharura kama ilivyokuwa kwenye sakata la Richmond), pia Waziri hakuzungumzia kabisa kuhusu mitambo ya Dowans ambayo asubuhi ya siku hiyo nilizungumza LIVE na TBC1 na kutaka serikali iitaifishe mitambo husika kwa kutumia sheria ya uhujumu uchumi na sheria nyinginezo ili iiwashe kwa dharura na kupunguza pengo la MW 120 wakati taifa likiendelea kufanya maamuzi ya namna ya kufidia kiwango kitachobaki. Aidha mjadala huo ungewezesha pia kutaka waziri awajibike kwa kutochukua hatua za mapema za kukabiliana na kinachoitwa dharura ambacho kilishafahamika toka mwaka 2006, 2008 na 2009 na maamuzi ya kuondokana na hali hiyo yakafanyika lakini hayakutekelezwa kwa wakati ( Bonyeza hapa kwa kauli ya awali kuhusu Dowans na mgawo wa umeme: http://mnyika.blogspot.com/2011/02/mitambo-ya-dowans-itaifishwe-waziri.html)
Katika kikao cha saba tarehe 18 Februari niliuliza Swali la Nyongeza kutokana na majibu ya Swali namba 85 kwa Wizara ya Maji. Kwenye swali langu la Nyongeza kwanza nilimkosoa Naibu Waziri kwa kutaja majina ya miradi ya maji ambayo iko Kigamboni na kueleza kwamba ni ya Ukonga na kumweleza Naibu Waziri kuwa pamoja na uwekezaji wa fedha za miradi ya maji za Benki ya Dunia na Wadau wengine wa maendeleo kwenye Ruvu Juu na Ruvu chini ikiwemo kuweka mtandao mpya wa mabomba ya maji maarufu kama mabomba ya wachina; bado maji kwenye kata za Kwembe, Kibamba, Msigani, Mbezi, Saranga, Kimara nk maji hayatoki kwa pamoja na mambo mengine upotevu wa maji na wafanyabiashara wanauza maji bei juu kujiunganishia kinyemela; je Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa? Naibu Waziri alijibu kwa kunipongeza kwa kuweka kipaumbele cha kwanza suala la maji katika kazi zangu na kuahidi kutembelea miundombinu husika kwa kushirikiana nami. Pia, niliuza Swali namba 91 kwa niaba ya Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi kwa Wizara ya Fedha kuhusu kero za upatikanaji wa mafao ya wastaafu na mirathi kwa watumishi waliokufa kazini. Baada ya majibu ya Waziri kueleza kwamba sababu ni matatizo ya mawasiliano ukiwemo udhaifu katika mfumo wa kumbukumbu kwa upande wa watumishi wanaohudumiwa na mifuko; niliuliza maswali mawili ya nyongeza, moja kuhusu namna ambavyo serikali imepanga kuondokana na matatizo hayo ya mawasiliano na kumbukumbu hasa kwa kuwa wapo wastaafu na marehemu ambao kumbukumbu zao zote zimekamilika lakini bado kuna kero nyingi katika kupata mafao na mirathi. Pili, niliuliza swali la kutaka tamko la serikali kuhusu wastaafu wengine ambao hawahudumiwi na mifuko kama wale wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki ambao mpaka sasa wanahangaika kuhusu mafao yao. Serikali ilijibu kuwa haina tamko la kutoa kwa sasa kwa kuwa inasubiri kwamba suala la Wastaafu wa Afrika Mashariki lipangiwe jaji mwingine katika mahakama ya rufaa kama walivyoomba.
Kwa muktasari huo ni mrejesho kuhusu ushiriki wangu ndani ya vikao vya mkutano wa pili wa bunge la kumi. Hata hivyo, kuna masuala mengine yanayohusu ushiriki wangu katika shughuli nyingine za kibunge nje ya vikao kwa nafasi zangu zingine kama Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CHADEMA, Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam, Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo, Msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani-Nishati na Madini na nafasi nyinginezo ambayo sijayaeleza katika taarifa hii. Nawashukuru sana wote walitoa maoni kwenye Mikutano ya Mbunge kuwasikiliza na kuzungumza na Wananchi tuliyoifanya Mbezi mwisho na Manzese Bakhresa siku chache kabla ya kuanza kwa mkutano wa pili wa bunge, sehemu ya masuala mliyonituma nimeyawasilisha. Hata hivyo yako mengine kutokana na ufinyu wa muda na kubanwa na kanuni sikupata wasaa wa kuyawasilisha ikiwemo suala la hoja ya mchakato wa katiba mpya ambalo nililitolea kauli ya tahadhari baada ya serikali kukubaliana nami mchakato husika kuanzia bungeni kwa kutungwa kwa sheria (Rejea kauli yangu ifuatayo: JOHN MNYIKA: Tahadhari kuhusu serikali kupeleka muswada wa katiba mpya bungeni). Nawashukuru kwa kuniunga mkono.
Tuendelee kuwasiliana, kushauriana na kushirikiana.
Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika (MB)
Monday, February 21, 2011
Dk Wilbrod Slaa Ashiriki Kwenye Misa Ya Watu wa Tatu Wa Familia Moja Waliofariji Kwa Ajali ya Mabomu Gongo la Mboto
Waziri Mkuu Mizengo Pinda(kulia) na Mbunge wa Singida Mashariki-Chadema Mheshimiwa Tundu Lissu
Thursday, February 17, 2011
Tamko la CHADEMA kuhusu Mabomu ya Gongo la Mboto
TAARIFA KWA UMMA
DODOMA, FEBRUARI 17, 2011
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) imeeleza kushtushwa na kusikitishwa na taarifa za
milipuko ya mabomu katika Ghala la Kuhifadhi Silaha la Kambi ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam
jana jioni.
Aidha, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewapa pole ndugu, jamaa, marafiki
na wananchi wote wa Tanzania kwa sababu ya maafa haya. Pia Kambi hiyo
imezitaka mamlaka zote za umma zinazohusika kuchukua hatua za haraka
kuhakikisha wananchi wote walioathirika na maafa haya wanapatiwa huduma zote
wanazohitaji katika kipindi hiki cha msiba huu. Hii ni pamoja na kuwapatia
huduma za maziko wale wote waliofariki, matibabu kwa waliojeruhiwa na
hifadhi kwa wale waliopoteza makazi yao. Aidha, ni muhimu kwa vyombo vya
usalama kuhakikisha ulinzi wa mali za wananchi katika maeneo yote
yaliyoathirika na ambazo zitakuwa hazina ulinzi baada ya wananchi kukimbia
maeneo yao.
Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeeleza kwamba tukio hili ni la
kushtusha na kusikitisha hasa kwa kuzingatia kwamba haijapita miaka miwili
tangu tukio la aina hiyo hiyo litokee katika Ghala ya Silaha ya Kambi
nyingine ya JWTZ katika eneo la Mbagala, Dar es Salaam, ambalo lilisababisha
vifo vya zaidi ya watu thelathini na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za
wananchi binafsi. Aidha, milipuko ya Mbagala ilipelekea Serikali kutumia
mabilioni ya fedha za umma kwa ajili ya malipo ya fidia kutokana na vifo,
majeruhi na uharibifu wa mali binafsi za wananchi.
Akielezea tukio la milipuko ya Gongo la Mboto, Msemaji wa Ulinzi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Joseph Selasini alisema: “Milipuko ya Gongo
la Mboto inaonyesha dhahiri kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) haijajifunza lolote kutokana na maafa yaliyotokea Mbagala
mwaka juzi. Maana kama Serikali ingejifunza kutokana na maafa hayo
ingeshachukua hatua za dharura na za haraka kuhakikisha kwamba maafa ya aina
hii hayatokei tena.” Mh. Selasini alizitaja baadhi ya hatua hizo kama ni
pamoja na kuhamisha maghala yote ya silaha na mabomu yaliyo karibu na maeneo
wanayoishi raia na kuyapeleka katika Kambi za JWTZ zilizoko mbali kabisa na
maeneo ya raia. “Haiwezekani kwa Serikali kuendelea kuweka maghala ya silaha
katika Kambi za Jeshi zilizo karibu na wananchi na hivyo kuhatarisha maisha
yao namna hii”, alisema Mh. Selasini.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewataka Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali
Davis Mwamunyange kujiuzulu mara moja ili kuwajibika kisiasa kutokana na
maafa ya Gongo la Mboto na ili kupisha uchunguzi huru na wa kina wa chanzo
na/au sababu za milipuko hiyo. Mh. Selasini alisema: “Dr. Hussein Mwinyi
alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa ya Mbagala; na Jenerali Mwamunyange
alikuwa Mkuu wa Majeshi. Maafa ya Mbagala yalitokea chini ya dhamana na/au
usimamizi wao. Na mara baada ya maafa hayo, Waziri Mwinyi na Jenerali
Mwamunyange waliliahidi taifa kwamba maafa ya aina hii hayatatokea tena.
Sasa yametokea. Inaelekea, kwa hiyo, kwamba ahadi yao ilikuwa sio ya kweli
na/au hawakuhakikisha kwamba inafanyiwa kazi ili iwe ya kweli. Viongozi hawa
hawana budi kuwajibika kwa hiari yao wenyewe au kuwajibishwa kama
itahitajika.”
Mh. Selasini aliongeza kusema kwamba hadi leo hakuna taarifa yoyote rasmi
iliyowahi kutolewa hadharani kwa wananchi na/au kwa wawakilishi wao Bungeni
ya chanzo na/au sababu za maafa hayo. “Hadi leo hii wananchi na/au
wawakilishi wao Bungeni hawajaambiwa kama kulikuwa na makosa ya makusudi
na/au ya uzembe na/au kama hatua zozote za kinidhamu na/au za kisheria
zilizochukuliwa dhidi ya mtu yeyote kutokana na kusababisha na/au kuwajibika
kwa maafa hayo. Jana maafa mengine ya aina hiyo hiyo yametokea tena na kwa
kadri ya taarifa rasmi ya Serikali watu wengi wameuawa na wengi wengine
kujeruhiwa na mali nyingi kuharibiwa. Kwa sababu hizo, huu ni wakati muafaka
kwa Dr. Mwinyi na Jenerali Mwamunyange kuonyesha uadilifu wao kwa kujiuzulu
nafasi zao ili kuwajibika kwa maafa haya.”
Uchunguzi na/au Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili
kuchunguza kwa kina chanzo, sababu na madhara yote yaliyosababishwa na
milipuko ya Gongo la Mboto. “Kwa kuzingatia historia ya uchunguzi wa
milipuko iliyotokea Mbagala mwezi Aprili 2009, Tume Huru na/au Kamati Teule
ya Bunge lazima itoe taarifa yake hadharani kwa kupitia Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania”, alishauri Mh. Selasini.
Mheshimiwa Zitto kabwe na Lucy Owenya
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA Mhe. Tundu Lissu
Tuesday, February 15, 2011
UZINDUZI WA TAWI LA CHADEMA CHUO CHA MIPANGO DODOMA
HOTUBA YA ZITTO KABWE BUNGENI
MHE. KABWE Z. ZITTO:
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kwanza, kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa kunichagua tena kuwa Mbunge wao kwa kipindi cha pili. Kitu pekee ambacho napenda kuwaahidi ni kuwatumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kuhakikisha kwamba tunafanya mabadiliko. Wao wanafahamu kwamba miaka mitano iliyopita tuliitumia kwa ajili ya kuimarisha miundombinu. Tumejenga barabara na kufungua maeneo ambayo yalikuwa hayafikiki. Miaka mitano ijayo tutaielekeza kwenye kuhakikisha kwamba vijiji vyetu tunapata nishati, rural electrification ili na watu wa Kigoma nao wajione ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika na napenda kuwapongeza Wabunge wote kwa umoja wetu bila kujali vyama vyetu kwa kuweza kufika hapa Bungeni na kuwa Wabunge wa Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye kipaumbele namba 2 katika hotuba ya Rais, kipaumbele cha ukuzaji wa uchumi. Na nikipata muda nitagusia kidogo kipaumbele namba 3. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi wa Taifa letu umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7. Lakini, takwimu zinaonyesha kwamba katika kipindi hicho hicho hali ya umaskini wa wananchi wetu imepungua kwa asilimia 2.5 tu. Wenzetu Uganda ambao uchumi wao umekuwa ukikua kwa asilimia 6 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, wapepunguza umaskini kwa asilimia 25. Nchi za South East Asia kama Malaysia ambao miaka ya 1970 tulikuwa nao sawa, ambapo zaidi ya asilimia 56 ya watu wao walikuwa ni maskini, leo ni asilimia 3 tu ya wananchi wao ni maskini. Tanzania asilimia 37 ya wananchi ni maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo kubwa sana la kutoweza kutatua issue ya inequality katika nchi yetu. Tumejikuta tunatengeneza mataifa mawili; taifa la matajiri na taifa la maskini. Na mgawanyiko huu umetanuka mpaka kwenye huduma. Leo kuna shule za maskini na shule za matajiri. Crisis tunayoizungumza leo ya watoto wa kidato cha nne kufeli sana au wa darasa la saba kufeli sana, siyo watoto wa Wabunge, siyo watoto wa watu wenye uwezo, ni watoto wa maskini kabisa. Watoto wa watu wenye uwezo wako kwenye shule za academies n.k.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya hali ni hiyo hiyo. wakati zamani ilikuwa huduma ya afya ya msingi ni ya kila raia kuipata, leo wenye uwezo wa fedha wana hospitali zao, maskini wana hospitali zao. huduma za usafiri hivyo hivyo na kila kitu. Kwa sababu tumeshindwa kuhakikisha ukuaji wa uchumi wa Taifa letu una-address hali nzima ya inequality (kutokuwa na usawa). Na hilo hatulizungumzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapata investment nyingi sana, nimesikia kule Mchuchuma na Liganga wanakuja watu, ten billion dollars investment. Lakini, haita-penetrate chini. Hatujawa na sera mahsusi za kuhakikisha tunakuza watu wa chini, na njia pekee, na aliniambia Mahatri Mohammed juzi nilipokuwa Malaysia, hatujengi mikakati ya klu-crate jobs. Vijana wengi sana hawana ajira, na hii ni time bomb, we don’t address this.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, katika kipaumbele chake cha tatu anazungumzia kujenga middle class. Sina problem na hiyo, mimi ni mjamaa, naamini katika ujamaa. Kwa hiyo, ningepaswa kutokuamini katika kuwa na middle class. Lakini, unajengaje middle class bado hatujaweza ku-address tatizo la watu wa vijijini ambao ndio maskini zaidi! Na reason is very clear, taarifa za Serikali zote zote, Waziri wa fedha yuko hapa, taarifa zote za MKUKUTA, mipango yetu yote inaonyesha kwamba ili tuweze kuwavuta
watu maskini, tuwaondoe, tuwapandishe, ni lazima sekta ya kilimo ikue kati ya asilimia 6 na 8 miaka mitatu mfurulizo. For the last 5 years tumekua kwa asilimia 3.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya uwekezaji yanazidi kuwa mabaya siku hadi siku, na we a very happy, some of us ni creators wa hayo mazingira, kwa sababu ni lazima tukiri. Na kama wawekezaji kwa maana ya internal na external hawaji kuwekeza, where will people get jobs! Kama private sector haipati mazingira mazuri ya kufungua viwanda, ya kufungua mashamba n.k. where will people get jobs! And this is not addressed. Tutapigana vijembe vya kisiasa tu, lakini tukumbuke hatima yake Watanzania watatuuliza mmekaa miaka mitano, mmefanya nini? Ni lazima sote (both sides of the houses) sisi Kambi ya Upinzani na watu wa Chama cha Mapinduzi tukubaliane tuhakikishe kwamba ni wapi tunataka kulipeleka hili Taifa. Tuweke pembeni kabisa hizi tofauti zetu, otherwise tutaenda kupata matatizo makubwa sana. Na nisingependa niishi katika umri wangu uliobakia nione nchi inasambaratika. Ningependa nione Tanzania inakuwa imara zaidi na zaidi.
Mheshimikwa Naibu Spika, la pili, la energy: Rais amezungumza kuongeza access to electricity mpaka asilimia 30. Sasa hivi Tanzania asilimia 14 tu. Katika kila nyumba 100 Tanzania, ni nyumba 14 tu zina umeme, 50 years after independence. Lakini uzalishaji wetu wa umeme bado ni mdogo na Waziri wa Nishati na Madini kila siku anatutajia miradi humu Bungeni na nje kwenye ma-press conference. Hatuambii ni mradi gani utatekelezwa l
ini! Lazima tukubaliane kama Bunge, tuseme tuchague basi angalau mradi mmoja, tunapofika tarehe 9 Desemba, tunasherekea miaka 50 ya uhuru, tunasema sasa angalau tumevuka 1000MW za umeme zinazozalishwa kwa uhakika. Otherwise we can’t go anywhere, we can’t. Sasa hivi nchi hii ina deficit ya umeme 2000MW, yaani umeme ambao unapaswa uwe umezalishwa hauzalishwi. Haiwezekani na hatuwezi kuendelea. 1992 sisi na Malaysia wote tulikuwa tuna power cut, wote, 1992. Wenzetu leo wana surplus 7000MW, sisi tuna deficit 200MW – 300MW. Lazima tukae tukubaliane ni namna gani ambavyo tunataka kui-transform nchi hii, vinginevyo tutaishia kuwa nchi ya maneno, tutaishia kuwa nchi ya kurushiana vijembe, tutaishia kuwa nchi ya kuzungumza tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naamini, mimi na vijana wenzangu ambao tuko humu Bungeni, hatutakubali. Na naomba vijana wenzangu wa pande zote mbili tukae, maana hii ndiyo nchi yetu sisi. Sisi ndio tutakaoishi muda mrefu zaidi kama Mungu akipenda. Akina Mzee Cheyo hawa sasa hivi tayari ni Alasiri. Ndio ukweli huo. Tukae, tuone ni namna gani ambavyo tutavuka mbele zaidi. Energy na growth ni very important. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
ZITTO KABWE Kutoka BUNGENI: Swali La Kwanza
MHE. KABWE ZUBERI ZITTO Aliuliza:-
Serikali katika Bunge la tisa ilitangaza kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira na kuuchukua mgodi huo ili kuumiliki na kuzalisha umeme.
a) Je, kwa nini Serikali haijawalipa wafanyakazi hao mpaka sasa?
b) Kwa kuwa Shirika NSSF limeleta kwa maandishi Serikalini nia ya kununua madeni yote ya mgodi wa Kiwira.Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya suala hili?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto,Mbunge wa Kigoma Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:
a) Mheshimiwa Spika, suala la mgodi wa Kiwira ni suala ambalo Serikali imekuwa ikilitolea maelezo kila mara hapa Bungeni,hususan,suala la wafanyakazi wa mgodi huo. Aidha, ni kweli Serikali ilitangaza kupitia Bunge la tisa kuwa italipa wafanyakazi wa mgodi huo mishahara yao.
Baada ya tangazo hilo Serikali imefanya malipo ya malimbikizo ya mishahara yao ya miezi 15 kwa awamu mbili kama ifuatavyo:
1. Awamu ya kwanza ilifanyika katika kituo cha Kiwira kwa madai yanayoishia mwezi Julai,2010; na
2. Awamu ya pili imefanyika mwezi wa Januari 2011 kwa madai ya malimbikizo ya kuanzia mwezi Agosti, 2010 hadi Januari 2011.
Malipo yamelipwa hadi kufikia Januari kwa mategemeo kuwa baada ya hapo wahusika watakuwa wanalipwa kwa utaratibu wa kawaida kwa sababu tumeshawaingiza katika bajeti yetu inayoendelea sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba, 2010 mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliwasilisha maombi Serikalini kwa ajili ya kuendeleza mgodi huo. Kufuatia maombi hayo,Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Uchumi na Shirika la Consolidated Holding Corporation ambalo lipo chini ya Wizara ya Fedha,tumeanza mchakato wa awali kutathmini ombi hilo,ili kujiridhisha kama NSSF wanaweza kuendesha shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme kabla ya kutoa mgodi huo kawo. Hivyo,baada ya mchakato (tathmini) hiyo kukamilika,Serikali itaweka bayana suala hili na endapo atakuwa amekidhi masharti atamilikishwa mgodi huo.
MHE. KABWE Z. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Serikali ilitangaza hapa Bungeni kwamba itachukua mgodi wa Kiwra na kuumiliki, lakini mpaka tunavyozungumza hivi sasa, haijafanyika tathmini yeyote ya mali na amdeni ya mgodi kwa ajili ya Serikali kuweza kuuchua. Na tayari mmoja wa wakopeshaji kupitia benki ya CRDB wametangaza kuufilisi mgodi na hivyo kuhatarisha mali na uwekezaji mkubwa ambao Serikali uliufanya katika mgodi huu, Serikali haioni haja ya kuharakisha zoezi na kuumiliki mgodi huu na kuupa kwa taasisi ya NSSF ambayo tayari wameonyesha nia ya kuweza kuhakikisha kwamba wanalipa madeni yote ambayo ni ya mgodi huu ili waweze kuzalisha umeme?
Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kusubiri mchakato uendelee Wizara ya Fedha hayaonyeshi udharura, uharaka au upo mkakati wa mgodi wa Kiwira katika kumaliza tatizo la umeme nchini, na jana takriban masaa mawili nchi nzima ilikuwa haina umeme na TANESCO wametangaza zaidi ya megawati 230 zimeondoka katika gridi ya Taifa. Waziri wa Nishati na Madini analiambia nini Taifa kuhusu Taifa hili? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu Mheshimiwa Spika na Watanzania kwa ujumla kwamba dhamira ya Serikali ya kufanikisha uendelezaji wa mgodi wa Kiwira iko pale pale na kinachoendelea sasa hivi tangu tutangaze hapa Bungeni ni masuala ya kiutalaam ambayo ni lazima tuyafanye kwa utaratibu unaoeleweka ili kuhakikisha kwamba tunapokwenda kuwekeza na kuendeleza mradi ule pasiwe na mashaka yoyote katika mradi huo.
Kwa hiyo muda wote Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya kazi yake kwa utaratibu na umakini kuhakikisha kwamba mradi ule unaendelezwa. Kwa hiyo mchakato unaendelea ni kwa taratibu za kawaida na ndiyo maana vikao kadhaa tumekuwa tukishiriki ambavyo nina hakika Mheshimiwa Zitto anafahamu pia kwa sababu kwa kiasi kikubwa taasisi ambazo zinashirikishwa katika eneo hili ikiwemo NSSF yenyewe ni taasisi ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha. Mikutano inaendelea vizuri na masuala yanayojadiliwa ni kwa maslahi ya Taifa.
kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni NA Mbunge wa HAI- chadema Freeman Mbowe(kushoto)akisalimiana na Mbunge wa Wawi Hamad Rashid
Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Wilbroud Slaa akisalimiana na Naibu kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Zitto Kabwe
Katibu Mkuu wa Chadema Dr.Wilbrod Slaa
Sunday, February 13, 2011
Wabunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA
Wabunge wa CHADEMA Wazindua Matawi vyuo Vikuu
Wabunge waliowakilisha Chama ni
1. Prof Kahigi- Bukombe
2.Halima Mdee- Kawe
3.John Mnyika-Ubungo
4.Godbless Lema-Arusha Mjini
5.Rebecca Mgodo-Viti Maalum Arusha
6.Regia Mtema- Vitimaalum Kilombero
Wanafunzi zaidi ya 200 wa Chuo Cha Mt John wamejiunga na CHADEMA sambamba na ufunguzi wa ofisi ya tawi hilo.
Zaidi ya wanafunzi 1000 wa Vyuo vya Mipango na UDOM wamejiunga na CHADEMA Sambamba na ufunguzi wa Tawi.
Wabunge hawa walipokelewa kwa nderemo na vifijo na wanafunzi hao.
Mapambano yanaendelea,Hakuna Kulala Mpaka Kieleweke.
Friday, February 11, 2011
Upotoshaji wa Kauli ya Mhe FreeMan Mbowe Bungeni
REGIA MTEMA
Mbunge wa Singida Mjini Mohammed Dewji (kulia) na Mbunge wa Hai Freeman Mbowe
Wednesday, February 9, 2011
CHADEMA NA VIONGOZI WAKITOKA NJE
Tuesday, February 8, 2011
Wabunge wakitafakari kuhusu muhtasari uliotolewa
Monday, February 7, 2011
MH FREEMAN MBOWE AKISALIMIANA NA MHE JAKAYA KIKWETE
Tuesday, February 1, 2011
TAMKO LA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHADEMA KUHUSU HALI YA TAIFA
Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika tarehe 29-30 Januari 2011 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe (Mb), pamoja na mambo mengine, imepokea, kujadili na kutolea maazimio Taarifa ya Hali ya Siasa na Taifa kwa ujumla. Maazimio haya yapo katika maeneo matano yafuatayo.
1. Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya.
Kamati Kuu imezingatia na kupongeza juhudi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wadau mbalimbali wa demokrasia nchini za kudai Katiba Mpya. Aidha, Kamati Kuu imejadili na kutafakari kwa kina maoni ya wadau mbalimbali juu ya mchakato unaofaa katika kupata Katiba Mpya, na kuzingatia kuwa njia sahihi ni ile itakayowashirikisha wananchi kikamilifu na kwa dhati bila kujali tofaui zao za kisiasa, dini, umri, elimu, kabila wala jinsia zao. Kamati Kuu imezingatia pia kwamba Tume ya Rais sio njia sahihi itakayowezesha upatikanaji wa Katiba Mpya yenye kuzingatia utashi, matakwa na mahitaji ya wananchi wa Tanzania. Hivyo basi:
- Kamati Kuu imepinga utaratibu wa kuunda Tume ya Rais katika uundaji wa Katiba Mpya
- Kamati Kuu imeunga mkono utaratibu wa kutumia Bunge katika kutengeneza na kusimamia mchakato utakaoletekeza upatikanaji wa Katiba Mpya
- Kamati Kuu imeipongeza Sekretariati yake kwa kumwagiza Mheshimiwa John Mnyika kuandaa na kuwakilisha Hoja Binafsi inayolitaka Bunge kuandaa sheria itakayoweka utaratibu na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya
- Kamati Kuu imewahimiza na kuwaomba wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunga mkono Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mnyika kwa maslahi ya Taifa.
2. Mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Jijini Arusha
Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya wananchi watatu wasio na hatia kwa kupigwa Risasi na askari wa Jeshi la Polisi kufuatia vurugu zilizosababishwa na Jeshi hilo katika harakati zao za kuzuia maandamano halali na yenye Baraka zote za Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilayani Arusha. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na uvurugwaji wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha kulikofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa maelekezo ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Katika maazimio yake:
- Kamati Kuu imewapa pole ndugu wa wafiwa wa vurugu za Arusha pamoja na wananchi wa Arusha na watanzania kwa ujumla
- Kamati Kuu imewapongeza Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mhe Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Peter Slaa, Mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema na viongozi wengine wa CHADEMA kwa juhudi zao kubwa za kuepusha shari na kutoa uongozi wa kisiasa pale ambapo wananchi wa Arusha walitelekezwa na viongozi wa Serikali ya CCM katika kipindi chote cha matatizo ya Arusha
- Kamati Kuu imeiagiza sekretariati ya CHADEMA kuendelea na harakati za kudai haki za wananchi wa Jiji la Arusha kwa njia za kisiasa.
- Kamati Kuu imewaagiza madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuingia katika vikao vya Baraza la Halmahauri hiyo na kuwawakilisha wananchi waliowachagua kikamilifu na wahakikishe kuwa wanatumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa Meya.
3. Matatizo ya Nishati ya Umeme na Gesi na Malipo kwa Kampuni Hewa ya Dowans
Kamati Kuu imesikitishwa na kupanda holela kwa bei za nishati muhimu za umeme na gesi, pamoja na kushindwa kwa serikali ya CCM katika kuwekeza kikamilifu katika sekta ya nishati hapa nchini. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na kufadhaishwa sana na uamuzi wa CCM na serikali yake kuridhia kuilipa Kampuni hewa ya Dowans fedha za walipa kodi wa Tanzania zipatazo Shilingi bilioni 94, pamoja na kwamba Kampuni hii ilikwishaharamishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi.
Kamati Kuu imetambua kuwa sakata la Dowans ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi ndani ya CCM na serikali yake ambavyo vimeligharimu taifa hili kwa miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:
- Kamati Kuu imewahimiza wana CHADEMA, wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kupinga kwa nguvu zote malipo ya Dowans
- Kamati Kuu imewaelekeza viongozi pamoja na wabunge wa CHADEMA kuendelea kuwahamasisha wananchi kupinga kwa njia mbalimbali za kisiasa na kisheria malipo ya Dowans na ufisadi mwingine hapa nchini
- Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wanaharakati wa taasisi za kiraia kwa ujasiri na moyo wao wa kizalendo kwa uamuzi wao wa kufungua kesi mahakamani ya kupinga malipo ya Dowans
- Kamati Kuu imeiasa Serikali ya CCM kutokuona aibu kutekeleza sera za CHADEMA zilizofanyiwa utafiti kuhusu namna ya kujenga na kuimarisha sekta ya nishati ya umeme na gesi hapa nchini ili nchi yetu iondokane na tatizo la kudumu la umeme.
- Kamati Kuu imeiagiza Secretariat yake kuanza maandalizi ya maandamano ya nchi nzima ya kupinga ongezeko la bei ya umeme, gesi na kuilipa Dowans. Na tarehe 24/02/2011 itakuwa siku ya kuanza maandamano kwenye Jiji la Mwanza na miji mingine kadiri ratiba itakavyotolewa.
4. Matokeo ya Kidato cha Nne
Kamati Kuu imeyapokea kwa masikitiko makubwa matokeo ya Kidato cha Nne yanayoonyesha kuwa nusu ya watahaniwa wote wamefeli Mtihani huo. Aidha, Kamati Kuu imezingatia na kusikitishwa na taarifa kuwa ni asilimia 11.5 tu ya watahiniwa ndio waliopata daraja la I hadi la III. Ndio kusema kuwa karibu asilimia 90 ya vijana wote waliomaliza kidato cha nne mwaka 2010 hawawezi kuendelea na elimu yeyote ya juu na itakuwa ni vigumu sana kwa vijana hawa kupata aina yeyote ya ajira ya uhakika.
Aidha, Kamati Kuu imezingatia kuwa matokeo mabaya ya Kidato cha Nne yamesababishwa na sera dhaifu za serikali ya CCM zenye kulenga kughilibu wananchi kwa ajili ya mafanikio ya kisiasa kwa kukazania wingi wa majengo ya shule badala ya ubora wa walimu na ubora wa shule. Kutokana na hali hii:
- Kamati Kuu imeyatangaza matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2010 kuwa ni Janga la Kitaifa
- Kamati Kuu imeitaka Serikali ya CCM isione aibu kutekeleza sera za elimu za CHADEMA zilizoanishwa katika ilani yake ya mwaka 2010, ikiwemo sera ya kutoa elimu bure na kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya walimu ambazo zilielezwa na wataalamu wa elimu kwamba ndio sera sahihi za kufufua ubora wa elimu ya nchi yetu
- Kamati Kuu imeunda timu maalumu ya wataalamu wa elimu kwa ajili ya kutafiti kwa kina sababu za matokeo mabaya ya Kidato cha Nne na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu katika kikao chake kitakachofanyika kabla ya Mwezi Mei 2011.
5. Kuhusu propaganda za udini hapa nchini
Kamati Kuu imesikitishwa na propaganda zinaendelezwa na viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi, hususani Rais Kikwete, kuhusu kuwepo kwa mfarakano wa kidini hapa nchini. Kamati Kuu imezingatia kuwa wananchi wa Tanzania wameendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano mkubwa bila kujali tofauti zao za kidini. Kamati Kuu imezingatia kuwa Viongozi wa juu wa CCM, na hasa Rais Kikwete, ameamua kuficha udhaifu wake wa kiuongozi chini ya zulia la udini ili wananchi waache kujadili mambo ya msingi ya Taifa hili, ikiwemo kushindwa kwa CCM kutekeleza ahadi ambazo imekuwa ikizitoa katika miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:
- Kamati Kuu imewahimiza wananchi wa dini zote hapa nchini kuendelea kuishi kwa amani na mshikamano na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii bila kujali tofauti zao za dini, ukabila wala itikadi ya siasa
- Kamati Kuu imewataka viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete kuacha kuchochea mgawanyiko wa dini hapa nchini kama njia ya kuficha udhaifu wake wa uongozi
- Kamati Kuu imewahimiza viongozi wa dini zote hapa nchini kuendelea kukemea maovu yeyote katika jamii bila woga wala upendeleo kwani hilo ni jukumu lao la msingi.
6. Kuhusu Ushirikiano wa Vyama vya Siasa vya Upinzani
Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja Kitaifa Zanzibar, na kwa kuwa Sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za Muungano, na kwa kuwa vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge wamo katika ushirikiano na CUF, Kamati Kuu imeona kuwa CHADEMA haiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo. Hivyo basi Kamati Kuu imemwagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kuunda Baraza la Kivuli kwa kuhusisha wabunge wa CHADEMA pekee.
7. Kuhusu mpango mkakati wa chama 2011-2016.
Kamati Kuu ilijadili na kupitisha mapendekezo ya mpango kazi wa chama kwenye Baraza kuu la chama .Pia ilijadili na kupitisha mpango kazi wa mwaka 2011-2012.
Tamko hili limetolewa leo tarehe 31/01/2011.
Dk Willibrod Peter Slaa
Katibu Mkuu