Hii ndio hotuba iliyotolewa na Naibu Katibu MKuu wa CHADEMA, Mh Zitto Kabwe . Tarehe ya Mei 09, 2009 baada ya maandamano makubwa yaliyotanguliwa na Bango lenye ujumbe “ Karibu Zitto Kabwe, Karibu Obama wa Tanzania, Mwongoze Magessa Bungeni, huku mbele yake wakiwa vijana waliobeba jeneza lililozungushwa kitambaa cha kijani katika kata ya Katoro ambayo ndio kata yenye wapiga kura wengi takribani asilimia thelathini ya wapiga kura wote wa jimbo la Busanda.
“ Leo ni furaha isiyo kifani kwa maandamano na mahudhurio makubwa kiasi hiki. Umati huu mkubwa unanikumbusha Mkutano wangu mkubwa wa kwanza kuwahi kufanya, Mkutano wa Jangwani niliofanya viwanja vya Jangwani baada ya maandamano marefu ambapo watu takribani laki mbili waliandamana na kukusanyika viwanja vya Jangwani mwezi Agosti 2007 wakipinga uamuzi wa wabunge wa chama cha mafisadi-CCM, kunisimamisha ubunge baada ya kuwashinda kwa hoja, katika mjadala uliohusu mkataba mbovu na wakifisadi wa Buzwagi.
Ni imani yangu mahudhurio haya tafsiri yake ni imani yenu kwa mgombea wetu Finnias Maggesa. Ni imani yangu kuwa Busanda na Katoro hamtatuangusha. Viongozi wenzangu waliotangulia kuhutubia wamezungumzia matatizo mengi yanayolikumbuka taifa letu, matatizo ambayo kwa miaka 48 utawala wa CCM umeshindwa kuyatatua.
Mtakumbuka matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 kwa kura halali na zisizo halali yalikipa CCM ushindi wa wabunge 274 na CHADEMA wabunge 11.Lakini kwa kipindi cha miaka mitatu, wabunge 11 wa CHADEMA tumeweza kuhakikisha masuala mengi muhimu kuhusu mwenendo wa Taifa letu yanajulikana kwa Umma. Bila CHADEMA watanzania wasingejua ufisadi wa Buzwagi, EPA wala ufisadi wa Richmond uliosababisha serikali ya awamu ya nne kuanguka. Nasema kuanguka kwasababu kikatiba waziri mkuu ndio mwenye serikali. Kwahiyo serikali hii ni ya awamu ya nne na nusu.
Wananchi wa Busanda, Ingawa tupo wabunge 11, lakini CHADEMA tupo makini kukabiliana na utawala huu mbovu chini ya uongozi mahiri wa Naibu Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dr Willibrod Slaa. Hii ndio sababu kwanini tunaomba mtuongezee mpiganaji wa 12, ambaye si mwingine bali kijana wenu, msomi wetu, mwenye sababu za kutosha kwa mapambano haya, Finias Magessa.
Ndugu zangu wa Busanda, Uchaguzi huu sio uchaguzi wa Ilani za vyama. Uchaguzi wa Ilani za vyama ulikuwa mwaka 2005, ndipo vyama viliomba kura kwa Ilani , na CCM ikapata asilimia 86 ya wabunge pamoja na Urais. Mwenendo wa serikali ya CCM wote mmeouna. Wanasikitisha na kukatisha tama wananchi. Ndio maana ninawaambia, Ilani ya CCM ni ileile, kama kwa kuwapa wabunge zaidi ya 200 pamoja na Urais wameshindwa kuwatumikia, mnadhani mkichagua mbunge huyu mmoja wa CCM atabadilisha kitu? Ataongeza nini kama wenzake zaidi ya 200 wameshindwa ? Jamani CCM hawana nyongeza ya Ilani! Ni hivi hivi! Ndio maana ninawaambia kwamba uchaguzi huu ni muhimu sana sio tu kwa nyie wakati wa Busanda, bali watanzania kwa ujumla. Ni kipimo. Ni kura ya maoni ambayo katika nchi nzima nyie watu wa Busanda ndio mmepata fursa hii ya kujibu. Mmepata fursa ya kuwaambia watawala tarehe 24, Mei mwaka huu kama mnakubaliana na mwenendo huu wa watala au hamkubaliani. Mnaridhika au hamridhiki.
Ukipigia kura mgombea wa CCM Mei 24, tafsiri yake ni kwamba unaridhika na mwenendo wa utawala wa CCM, na ukipigia kura CHADEMA maana yake ni kwamba ni unatuma ‘signal’ kwa watawala wetu kuwa hauridhiki na mambo yanavyokwenda katika nchi yako.
Ndugu zangu wa Busanda, labda nyie hamkumbuki CCM inatupeleka awamu mmoja hadi nyingine. Kwa mujibu wa taarifa ya Hali ya Umasikini na Maendeleo nchini, Mwaka 2005, Tanzania ilikuwa na wananchi ambao ni fkara milioni 11, yaani hawa wanaishi chini ya dola moja kwa siku. Yaani mapato yao ni chini ya ya shilingi 1300 kwa siku.
Rais Jakaya Kikwete alipokuwa kwenye kampeni aliahidi maisha bora kwa kila mtanzania. Na CCM ikaahidi kwenye ilani yake kwamba itapunguza idadi ya watu hawa masikini kabisa kwa asilimia 50%. Leo mwaka 2009, mwaka mmoja kabla ya mwaka wa uchaguzi 2010, Taarifa ya Hali ya umasikini inaonesha kuwa idadi ya watanzania wanaoishi chini ya kipato cha dola moja(shilingi 1300) kwa siku wameongezeka badala ya kupungua, na sasa wamefikia milioni12.7. Umasikini unapungua, au unaongezeka?
Hili ndilo Busanda mnalo Mei 24. Ukipigia kura CCM maana yake unakubaliana na mwenendo wa serikali ya CCM uliosababisha idadi ya masikini kuongezeka mwaka hadi mwaka. Leo mwaka 2009 masikini kabisa wameongezeka kufikia milioni 12.7 kutoka milioni11 mwaka 2005. Maana yake katika miaka 3 CCM imeongeza idadi ya watu masikini kabisa milioni moja na laki saba.. Kwa mwenendo huu, Je kufikia kipindi cha uchaguzi wa 2010 watanazania wangapi watadumbukia kwenye shimo hilo la masikini kabisa? Milioni3? 5?.
Hii ndio maana ya uchaguzi huu. Ni uchaguzi wenu wakazi wa Busanda. Sisi tumekuja kuwawezesha tu. Tumekuja kuwaunga mkono mfanye maamuzi sahihi kwa niaba ya watanzania wengine ambao hawakupata fursa hii. Mkichagua CCM mtakuwa mmewaangusha watanzania. Watanzania wana imani kubwa na nyie mliochaguliwa na Mungu kupiga kura hii ya maoni!
Hebu fikiria wewe Baba na Mama wa Busanda. Mwaka 2005, katika kila wanawake 100,000, wanawake 520 walifariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito, Leo mwaka 2009, wanawake 527 wanafariki kutokana na matatizo ya ujauzito, matatizo ambayo msingi wake ni huduma duni za afya. Takwimu hizi maana yake nini? Maana yake katika kila lisaa limoja la Tanzania chini ya utawala wa CCM mwanamke mmoja anafariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito yanayosababishwa na serikali kutojali wanawake wan chi hii, na zaidi wanawake wa vijijini kama Busanda.
Hebu fikirieni ninyi wazazi na wakazi wananchi kwa ujumla. Mwaka 2005, katika kila watoto 1000, watoto 114 walipoteza maisha kwasababu ya matatizo ya uzazi, leo mwaka 2009, watoto 112 wanafariki dunia kwa matatizo hay ohayo. Tarehe 24 Mei unapokwenda kupiga kura maana yake unakwenda kujibu swali hilo. Ukimpigia kura Magessa wa CHADEMA maana yake unapinga watoto wasio na hatia kuendelea kufriki dunia kwasababu zinazotibika kabisa. Na ukipigia kura CCM maana yake unakubaliana na mwenendo wa vifo vya watoto wasio na hatia kama hivi.
Sisi CHADEMA tunaomba utupigie kura katika uchaguzi huu ili watawala washituke, wajirekebishe. Wajue kwamba watanzania haturidhiki na mwenendo huu wa umasikini na vifo. Wewe mwananchi ukiipigia CCM kura hawatajua kama kuna tatizo, hawatajua kama wananchi wanaumia. Hawatajirekebisha.
Hali ya Taifa hili ni mbaya sana. Na tusipoangalia, Taifa hili tutalipeleka shimoni kabisa. Tangu mwaka 2007, Asilimia 38% ya watanzania wamedumaa akili kutokana na lishe duni. Maana yake nini? Maana yake katika kila watanzania 100, watanzania 38 wamedumaa akili, hawafikiri vizuri kutokana na lishe duni. Lishe duni ni ‘indicator’ ya ufukara. Kama madiwani wa CCM ni watanzania wa kawaida, basi katika kila madiwani 10, madiwani 4 wamedumaa akili. Au katika kila wabunge 10( wa CCM lakini), wabunge 4 wamedumaa akili kama wanatoka familia za kawaida. Hivyo hivyo kwa mawaziri wa serikali ya CCM, kwamba inawezekana katika kila mawaziri 10, mawaziri 4 wamedumaa akili. Pengine ndio sababu wamekuwa wanasaini mikataba mibovu ya kifisadi.
Kwahiyo tarehe 24, Mei, Ukichagua CCM, maana yake ni kwamba unaunga mkono mwenendo wa serikali ya CCM kusababisha watanzania 4, katika kila watanzania 10 wawe waendelee kudumaa akili. Na ukimpigia kura Magessa wa CHADEMA, maana yake ni kwamba, unapinga , unakasirishwa na mwenendo huu. Jamani taarifa hizi hatuzitungi sisi! Wala hatuziandai sisi. Ni taarifa za serikali. Ukisoma taarifa ya serikali ya Hali ya Umasikini na Maendeleo nchini (Pverty & Human Development 2007).
Haya ndio maswali CCM wakija muwaulize, ingawa sidhani kama watafanya mikutano ya hadhara mana nimesikia wanaogopa sana kuzomewa kwa uzembe na ufisadi wa serikali yao.
Nimesikia hapa mji mdogo wa Katoro, ambayo ni makao makuu ya jimbo hamna umeme. Hamna tofauti na Kasulu wala Kibondo mkoani Kigoma. Madhara ya kukosa umeme sio tu kwa wenye uwezo wa kuwa na umeme kukosa umeme, hali hii inasababisha gharama za maisha kuwa juu, kwasababu gharama za uzalishaji zinakuwa juu.Tulifanya utafiti Dar es Salaam kwa vijana vinyozi. Umeme ukikatika wakawasha jenereta wanatumia shilingi 68,000. Lakini wakitumia umeme wa TANESCO wanalipia shilingi 8000 tu. Maana yake kwa kutumia umeme wa jenereta wanapata hasara ya ziada ya shilingi elfu sitini. Hii ni tafiti ilifanywa na Kamati ya bunge. Kwaiyo sio Katoro tu. Nchi nzima ni tatizo.
Nilazima watanzania tutafakari kama tunakokwenda ni sahihi au la! Na tufanye maamuzi. Wakati tunapata uhuru, Asilimia 15 ya watanzania walikuwa na Umeme.Leo ikiwa ni miaka 48 ya Uhuru, watanzania wanaopata huduma ya umeme hawazidi asilimia 12. Maana yake katika nchi hii yenye umri wa miaka 48 ya uhuru, katika kila nyumba 100, ni nyumba 12 tu ndizo zenye umeme, ilhali wakati wa uhuru, katika kila nyumba 100, nyumba 15 zilikuwa na umeme.
Kwahiyo ukienda kupiga kura tarehe 24, Mei, unapaswa kujiuliza kama unakubaliana au hukubaliana na mwenendo huu. Ukichagua CCM maana yake unaridhika kuona kwamba wakati miaka 48 iliyopita watanzania walikuwa na huduma ya umeme ilikuwa 15, ni sawa, na sio tatizo kwa leo Tanzania huduma ya umeme kuwa asilimia 12.Naukiipigia kura CHADEMA mana yake unatma ujumbe kwa watawala kwamba unaumizwa na hali hii. Haukubaliani na hali hii.
Njia pekee yaw ewe mkazi masikini kukataa hali hii ni kukataa kuipigia kura CCM. Ni kuipigia kura CHADEMA. Ni muhimu uone kama nafasi hii adimu kuwa muhimu sana kwako. Maana uchaguzi huu umefanyika kwasababu ya mipango ya Mungu. Na tunao amini katika Mungu, tunaamini kwamba mipango ya Mungu haina makosa. Na kila mpango una busara yake. Msituangushe kwakupewa fursa hii kabla ya miaka5 kukamilika.
Hali ni mbaya ndugu zangu. Tanzania nzima ina majimbo 232. Lakini ni ninyi watu wa Busanda mliopewa fursa ya kuchagua tena kabla ya miaka 5. Nimesikia viongozi wa CCM wakipita na kuahidi eti CCM ikishinda uchaguzi huu italeta umeme Busanda. Waulizeni walikuwa wapi miaka 48 yote hii. Kama wameshindwa kuleta ndani ya miaka 48, watawezaje ndani ya mwaka 1?
Ndio maana sisi CHADEMA tunawaambia watanzania kwamba uchaguzi huu ni kura ya maoni , Tunaamini mtachagua CHADEMA ili kuonyesha kwamba hamkubaliani. Kuna matatizo mengi sana wilaya hii ya Geita. Kwa mujibu wa taarifa za uchumi za mwaka 2006, Geita ni miongoni mwa wilaya tatu masikini kabisa Tanzania, ikiwa pamoja na Bunda na Musoma vijijini.
Ninyi wilaya yenu ya Geita, unaozalisha takribani wakia laki tatu na nusu kwa mwaka, ambazo ni sawa na bilioni 211 kwa bei ya sasa. Lakini utajiri huo hauna tafsiri yoyote kwa maisha yenu. Sisi kwenye Kamati ya Bomani iliteuliwa kupitia upya mikataba ya madini nchini tulipendekeza kanuni ya kukokotoa mrabaha kwanza ibadilishwe kutoka asilimia tatu hadi 5, lakini zaidi hesabu hizo zikokotolewe kutokana na gharama zote za uzalishaji, na sio mwekezaji azalishe kasha aondoe gharama zote za uzalishaji kasha ndio atupe watanzania asilimia 3 tu ya hilo salio. Kwasababu CCM haina dhamira ya kuwasaidia, bado imeendelea kupiga danadana utekelezaji wa Kamati yetu.
Baada ya vuguvugu la kupinga mikataba mibovu liliasisiwa na CHADEMA tangu sekeseke la Buzwagi, Leo Geita mnapata dola laki 2 kutoka mgodi wa dhahabu wa Geita( Geita Gold Mining-GGM). Kule Tarime, Halmashauri ile chini ya Uongozi wa CHADEMA, kwa kuamini kuwa wawekezaji wanatunyonya watanzania wakawaida kwasababu ya elimu duni, CHADEMA tuliamua fedha yote ile ipelekwe kusomesha watoto bure kwa shule za sekondari. Ni kweli fedha hizi ni kiduchu sana, lakini si haba. Sio sawa na kukosa kabisa. Sasa kama Tarime fedha hizi zinasomesha watoto. Nyie wilaya ya Geita fedha hizi zinakwenda wapi? Zinaishia kwenye warsha, vikao na makongamano ya madiwani.
Yote haya ni matokeo ya utawala dhaifu na usiowajali wa Chama cha Mapinduzi-CCM. Kwa mfano, kama Serikali ya CCM ingekubali kuetekeleza mapendekezo ya Kamati ya Bomani, Badala ya wilaya zenye migodi kupewa dola 200,000. Kila wilaya yenye mgodi ingelipwa dola milioni2 kwa mwaka. Yani mara 10 zaidi ya sasa.
Tarehe 24 Mei, ukienda kupiga kura, ukichagua CCM, maana yake unakubaliana na utaratibu wa sasa wa CCM kutoa dola laki mbili kwa mwaka kwa halmashauri yako badala ya dola milioni mbili kama Kamati ya Bomani inavyotaka unufaike na madini. Kura yako ni alama! Ukienda ukampigia kura Magessa, maana yake unataka Serikali ya CCM itoe dola milioni mbili badala ya dola laki mbili kwa Halmashauri yako.
Kwaiyo unaona thamani ya kura yako ilivyo kubwa. Zaidi ya utu wako, kura yako ina thamani ya mabilioni. Lakini leo tunasikia CCM wanapita wanawahonga watu shilingi elfu mbili, tatu,nne, tano. Inajua bei za wateja wake. Ukiwa mjanja mjanja kidogo inakupa hata elfu kumi. Ukiwa hujui kitu kabisa inaweza kukupa hata shilingi mia moja. Lakini wote hawa ni wajinga, tofauti yao ni bei za ujinga wao.
Ukiuza shahada yako maana yake unahujuma maendeleo ya Taifa leko. Unahujumu maisha ya watoto wako.Lazima mjiulieze kwanini mtu akupe pesa kukuzuia usipige kura? Watoto wenu hapa wanasoma shule za kata zisizo na walimu, vitabu, wala maabara kwasababu mnakosea kupiga kura.
Kura yako ni muhimu sana. Ukipigia kura CCM maana yake unaunga mkono ufisadi. Ukipigia kura CHADEMA maana yake umeamua kuunga mkono harakati za uzalendo. CCM haijawi kuwa na huruma baada ya Mwalimu Nyerere.
Wakati kwa kipindi cha miaka 10, tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2006, Bunge la Tanzania halikuwa limepata hoja binafsi kutoka kwa mbunge yeyote, Hoja binafsi ya kwanza ilitolewa na mimi Bungeni, Hoja ya Buzwagi kupinga ufisadi katika mikataba ya madini ambapo baada ya kuwashinda kwa hoja, bunge la CCM mafisadi waliamua kunisimamisha kazi yangu ya uwakilishi. Na hoja binafsi ya pili ni hoja ya ufisadi wa benki kuu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, ambayo ilikataliwa na tukaamua kuipeleka kwa Umma septemba 15, 2007 , na mpaka leo bado inaisulubu serikali ya CCM.
Tangu sekeske la Buzwagi, Agosti 14, 2007, Hali ya taifa ni tete haijawahi kutokea tangu uhuru, na itaendelea kuwa tete mpaka hapo watanzania watakapofaidika na rasilimali za nchi yao. Na Tanzania haitafikia hali hiyo chini ya utawala wa CCM. Njia pekee ni kuondoa utawala huu uliojaa wezi, wasio na uchungu na maisha yaw ewe masikini wa Busanda.
Asiwadanganye mtu kwamba ndani ya CCM kuna kiongozi mwenye ujasiri wa kupambana na ufisadi. Mana wameanza kujitokeza baadhi ya wabunge wa CCM eti wakijifanya na wao wana uchungu na nchi hii. Eti na wao wanapambana na ufisadi. Waulizeni walikuwa wapi miaka yote hii nchi ikiuazwa? Leo baada ya CHADEMA kuhamasisha Umma kwa kupinga ufisadi, nao kwa aibu ya kuogopa kuzomewa ndio wanachukua ajenda za CHADEMA ili nao wasionekane mafisadi. Mimi nawaambia, hakuna kiongozi safi ndani ya CCM. Wabunge wote wa CCM walishinda uchaguzi Mkuu kwa takrima.
Vita dhidi ya ufisadi ni via takatifu. Haiwezi kufanywa kwa unafiki. Wala kwa hawa ninaowaita walokole wa vita dhidi ya ufisadi.. Nimeambiwa watakuja hapa akina Olesendeka, akina Dk Mwakyembe na wenzao. Mimi nawaambia wabunge wote wa CCM walipewa shilingi milioni5 ambazo ni sehemu ya fedha za ufisadi zilizochotwa benki kuu kupitia kampuni ya kifisadi ya Kagoda. Waulizeni wakija. Mana wakati walitumia fedha za ufisadi wa Kagoda, leo wanajifanya wanapinga ufisadi. Wapi na Wapi jamani?
Ndio maana nawaambia kuwa uchaguzi huu wa Busanda ni wa kihistoria. Mnayo nafasi ya kuamua kuiangusha CCM, mnayo nafasi ya kutukataa. Sisi tupo wabunge 11. Lakini kazi tuliyoifanya kwa miaka hii mitatu tunaamini, kama mnaipenda nchi yenu mtatuongezea wabunge. Tumpate mpiganaji wa 12, Ndugu yangu Finias Magesa. Mkituchagua mtakuwa mmetupa moyo, na itatusaidia kuongeza mapamabno zaidi. Lakini mkituangusha mtakuwa mnatuvunja moyo. Ni sawa na kutuambia kuwa mapambano yetu dhidi ya ulinzi wa rasilimali za madini na vita dhidi ya ufisadi ni kelele tupu.
Tumekuwa tukiwaambia watanzania. Mwenyezi Mungu hakudhmilia nchi hii iwe na watu masikini kiasi hiki. Hebu angalieni, Kanda ya ziwa imejaa dhahabu, Almasi, Nickeli na Almasi. Kanda ya Magharibi imejaa Shaba, Mafuta na madini ya fedha. Kanda ya kati ya ina madini ya uranium yanayotumika kutengenezea mabomu ya nuclear, Kanda ya Pwani imejaa gesi na mafuta. Kanda ya kusini imejaa makaa yam awe. Kila kanda Mungu ameipa utajiri. Lakini masikini wamejaa juu ya ardhi tajiri. Kwanini msichukue hatua? Mimi ninawaambia. Njia pekee ya kutoka hapa tulipo kwanza ni kuikataa CCM.Ndio maana ninarudia! Uchaguzi huu ni zaidi ya uchaguzi. Ni kipimo kama mnaridhika au hamridhiki na mwenendo wa utawala wa namna hii.
Katika uchaguzi wa 2005, CCM waliwaahidi maisha bora kwa kila mtanzania kufikia mwaka 2010. Leo ni 2009, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, Wangapi maisha bora walau yamepiga hodi kwao? . Mwaka 2005 bei ya kilo ya sukari ilikuwa shilingi 600, leo bei ya sukari shilingi 1400. bei imepanda zaidi ya mara mbili, Je mapato yenu yamepanda au yameshuka? Bei ya khanga za akina mama mwaka 2005, khanga ya India ilikuwa sh 2000. Leo naambiwa hapa Busanda khanga ileile inauzwa shilingi 3500. Mfuko wa saruji mwaka 2006 uliuzwa kwa shilingi 11,000. Leo mwaka 2009 mfuko wa saruji unauzwa shilingi 21000. Mwaka 2006 nauli kutoka kijiji chochote cha jimbo la Busanda kwenda Geita ilikuwa ni shilingi 1000 mpaka 2000 tu.
Leo mwaka 2009, nauli zimepanda hadi shilingi 3000. Lazima mjiulize kweli mapato yenu yamepanda?. Kweli haya ndio masiha bora mliyotarajia? Wakati bidhaa hizi zinapanda bei, mazao yenu ya kilimo kama pamba serikali imeshindwa kuzuia yasiporomoke bei. Wakati mwaka 2006 kilo ya pamba iliuzwa kwa shilingi 400, leo mwaka 2009, kilo ya pamba inauzwa kwa shilingi 300. Na haya ndio maisha bora mliyoahidiwa na CCM. Mapato yenu yanaporomoka, uwezo wenu wa kununua unashuka, lakini bidhaa za kununua zinaachwa zipande bei.
Tarehe 24, Mei ukienda kupiga kura , ukichagua CCM maana yake unakubaliana na gharama za maisha kupanda. Ukichagua CHADEMA na Magessa maana yake unatuma ujumbe kwa watala kwamba hakubaliani na kupanda kwa gharama za maisha.
Najua kwamba watawala hawa walioshindwa wamekuwa wakitumia nguvu za dola kukabiliana na utashi wa wananchi walioamua kufanya mabadiliko. RPC na OCD naomba mnisikilize kwa makini. Mjue kwamba chochote mlichovaa, kuanzia kiatu, magwanda ni kodi zetu wananchi. Na labda wananchi mkumbuke kuwa hawa polisi, wengi ni watoto wa masikini kama sisi. Ni mgawanyo wa kazi, wengine wanakuwa walimu, wengine madkari, wengine polisi, wengine wabunge. Sasa kwenda kwenu upolisi kusiwafanye mgeuke tatizo kwa wananchi badala ya kuwalinda.
Polisi mnapaswa kukumbuka kuwa ninyi ni watoto wa masikini kama sisi. Mkimtesa kijana wa Busanda, basi ujue kwamba na wewe kwenu mdogo wako anateswa na polisi mwenzako. Ukimtesa mama wa Busanda hapa, ujue kwamba polisi mwenzako anamtesa mama yako huko kwenu. Ukimtesa mzee wa Busanda, ujue na wewe wazee wako wanateswa na polisi wenzako huko kwenu.
Polisi wanapaswa kukumbuka ni sisi wabunge tunaojadili na kupitisha bajeti zao. Na sisi wabunge wa upinzani siku zote tumekuwa mstari wa mbele kudai maslahi bora ya polisi ili kupunguza udokozi wa polisi kwa wananchi masikini kabisa, na kuwasababishia usumbufu, na kukosa amani. Hatutaki polisi watupendelee, wala watuonee. Wakituonea tutajibu. Wakipendelea CCM tutakataa. Polisi wanapaswa kujua leo ni polisi, kesho raia. Hatutaki polisi waonee raia, ingawa hatutaki raia wavunje sheria.
Jamani polisi wa Tanzania ndio polisi wanaolipwa kidogo kuliko polisi wote katika nchi kumi na mbili za SADC. Nchi zingine kama Malawi ambazo uchumi wake unategemea tumbaku lakini polisi wake wanalipwa vizuri kuliko polisi wetu, Nchi yenye madini, ziwa, bahari, ardhi yenye rutuba, watu wenye moyo wa kufanya kazi na kila aina ya utajiri.
Polisi wanapaswa kufikiria upya kuhusu ukandamizaji wanaoufanya dhidi yetu wapinzani maana wao ni sehemu yetu. Wote tumepigika tu! Polisi ndio wanaolinda benki kuu, lakini wakati mafisadi yanaingia benki kuu, polisi wetu wanapiga ‘saluti’, mafisadi yanaingia yanachota mabilioni ya fedha, yanatoka. Polisi wanabaki ni wakukamata vibaka wanaoiba masufuria, mbuzi, kuku, na vitu vidogo vidogo. Mapapa na manyangumi yanayohujumu uchumi wetu hayaguswi.
Mimi Zitto Kabwe nawambia, sitaki kusikia mtanzania yeyote wa Busanda ananyanyaswa na polisi eti kwa sababu ya chama chake.Nikipata polisi mmoja anayenyanyasa raia kwa sababu tu ya chama chake, nitamfanyia kazi kama nilivyomfanyia Nazir Karamagi. Na nilipokuwa Tarime kwenye uchaguzi mdogo niliwaambia polisi kauli kali kwasababu ya ujinga na upumbavu wa baadhi ya polisi. Sitarajii yaliyofanywa na polisi Tarime yatajirudia Busanda. Yeyote atakaye nyanyaswa na polisi hapa atoe taarifa kwa viongozi wa CHADEMA. Ila msivunje sheria.Hatutamtetea yeyote atakaye vunja sheria. Tunataka uchaguzi wa amani, tumapate Magessa tujenge taifa hili, Kazi ambayo CCM imethibitisha kwa vitendo kuwa wameshindwa.
Tarehe 24, Mei mchague Magessa akutetee wewe mkazi wa Katoro, awatetee wakazi wa jimbo la Busanda. Awatetee wakazi wa mkoa wa Mwanza. Awatetee watanzania. Mkoa wa Mwanza una majimbo 11, yote mkaipa CCM. Kuna Kikao cha Kamati ya mashauriano ya mkoa, RCC, Nani atawatetea kwenye RCC ilhali mmejaza wabunge wa CCM humo?
Mimi nawaambia kutoka uvungu wa moyo wangu kwamba, wabunge wa CHADEMA hata tufanye kazi namna gain Dodoma, kama hamna ‘mbwa’ mkali Geita, Mwanza, mtaendelea kuibiwa tu!. Tunahitaji mbwa mkali ambaye akiona ufisadi kwenye Halmashauri, RCC na Serikali kuu aje kuwaambia. Tunahitaji mtu mwenye rekodi na tusiye na mashaka kuhusu dhamira yake ya kututumikia. Na katika wagombea hawa, hakuna Mwingine isipokuwa Magessa.
Hakuna mtu yeyote wa CCM ambaye akiwa mbunge anaweza kupinga ufisadi wa CCM ilhali wabunge wote wa CCM ni zao la ufisadi.. Labda apinge kwa unafiki wa makundi ndani ya CCM lakini sio kwa dhamira ya mapenzi ya mtanzania kwa nchi yake. Magessa amesoma sekondari Tosa Maganga, Zitto amesoma sekondari Tosamanganga. Magessa amesoma shahada ya kwanza na kufanya harakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zitto amesoma shahada ya kwanza na kufanya harakati Chuokikuu cha Dar es Salaam. Magessa amesoma shahada ya pili Ujerumani, Zitto Amesoma Shahada ya pili Ujerumani. Ninawaomba wananchi wa Busanda, mpeni nafasi kijana wenu Finias Maggessa. Ninaamini Magessa ni Zitto na Zitto ni Magessa.
Dira Ya Dunia
1 hour ago
0 comments:
Post a Comment