Showing posts with label Matamko. Show all posts
Showing posts with label Matamko. Show all posts

Monday, February 28, 2011

Uthibitisho wa Mhe. Lema kuhusu Pinda kuongea uongo Bungeni

Maelezo ya uthibitisho ya Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema (mbunge) juu ya kauli ya uwongo iliyotolewa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo P.K. Pinda (mbunge) wakati akijibu maswali kwa Waziri Mkuu katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tarehe 10 Februari, 2011

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, nilikuomba “kupata ufafanuzi kwamba Mbunge anaweza akachukua hatua gani kama anaona mtu mwenye nafasi kubwa katika nchi kama Waziri Mkuu analidanganya taifa na kulidanganya Bunge.” Badala ya kunipatia ufafanuzi niliouomba, Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ifuatayo, kwa mujibu wa Hansard hiyo: “Mheshimiwa Mbunge, Bunge hili lazima liwe na adabu inayostahili. Kwa hiyo kama tutafanya Bunge letu hili ikawa ni mahali, sasa unataka kusema Waziri Mkuu kwa ahadi aliyoweka ndani ya Bunge hili anadanganya? Kama anadanganya naomba ukaiandike vizuri kabisa kuhusu kudanganya kwake, halafu nitakuambia tufanye nini.”

Mheshimiwa Spika,

Baada ya maelekezo hayo ya awali, ulitoa maelekezo ya ziada kwamba “nampa mpaka tarehe 14 asubuhi alete maandiko ya kuthibitisha maneno aliyoyasema…. Kwa hiyo tarehe 14 kipindi cha asubuhi atoe maelezo ya kwamba Waziri Mkuu amesema uongo. Maana yake alichosema kwamba Waziri Mkuu amesema uongo sasa anataka tumpe Mwongozo wa namna ya kufanya na akasema aandike. Sasa kifungu hiki cha 64 kinamdai alete maelezo hayo mpaka tarehe 14.”

Mheshimiwa Spika,

Maneno yote ya Hansard niliyoyanukuu hapo juu yanathibitisha kwamba mimi sikusema Waziri Mkuu amesema uongo, bali niliomba mwongozo wa Spika kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Mbunge endapo kiongozi wa ngazi za juu kama Waziri Mkuu atasema uongo au kulidanganya Bunge. Hata hivyo, kwa vile umenielekeza nitoe maelezo uthibitisho kwamba Waziri Mkuu alisema uongo au kulidanganya Bunge, na kwa kutimiza maelekezo yako, naomba sasa nithibitishe kwamba kauli ya Waziri Mkuu kuhusu matukio yaliyopelekea mauaji ya wananchi wa Arusha na Mbarali yalikuwa ya uongo na kwamba Waziri Mkuu alilidanganya Bunge.

1. UONGO WA KWANZA

Mheshimiwa Spika,

Waziri Mkuu amenukuliwa kwenye Hansard ya tarehe 10 Februari 2011 akidai kwamba “… tumepoteza maisha ya Watanzania watatu bila sababu.” Huu ni uongo wa kwanza wa Waziri Mkuu Bungeni. Ukweli ni kwamba waliopoteza maisha ni Watanzania wawili – Dennis Michael Shirima na Ismail Omari – na Mkenya mmoja aliyejulikana kwa jina la Paul Njuguna.

2. UONGO WA PILI

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Hansard ya tarehe 10 Februari 2011, Waziri Mkuu alitamka maneno yafuatayo kuhusu suala la maandamano ya Arusha: “Mliomba wenyewe mfanye maandamano, hatukukataa, mkakaa na askari pale mkaelewana vizuri. Mkakubaliana kwamba sisi tunafikiri ili tuweze kuwadhibiti vizuri na kuwalinda vizuri, tutumie route moja tu. Wenzangu nyie mkakataa.” Kauli mbili za mwisho kwamba zina maana kwamba Jeshi la Polisi lilipendekeza kwamba njia moja ya maandamano ndiyo itumike na kwamba viongozi wa CHADEMA walikataa pendekezo hilo. Kauli hiyo, Mheshimiwa Spika, ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kulidanganya Bunge.

Mheshimiwa Spika,

Ukweli wa jambo hili ni kwamba tarehe 31 Desemba 2010, Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini alitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20/10 yenye kichwa cha habari: “TAARIFA YA MAANDAMANO NA MKUTANO WA HADHARA TAREHE 5 JANUARI 2011.” Sehemu ya barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwamba “… CHADEMA (Wilaya ya Arusha Mjini) tutakuwa na maandamano ya amani tarehe 5 Januari 2011 yatakayohitimishwa na mkutano wa hadhara katika viwanja wa NMC – unga Ltd.” Aidha, barua hiyo ilipendekeza njia ifuatayo ya maandamano hayo: “Maandamano hayo yataanzia maeneo ya Phillips saa NNE asubuhi, kuelekea Sanawari, Mianzini, Stand Kuu kuelekea Mnara wa Azimio, kupitia Polisi – Manispaa – Clock Tower kushukia Sokoine Road, kasha Friends’ Corner na kuingia viwanja vya NMC.” Nakala ya taarifa hiyo ya CHADEMA kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha Mjini imeambatanishwa katika maelezo haya kama Kielelezo ‘A.’

Mheshimiwa Spika,

Mnamo tarehe 2 Januari 2011, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini alimwandikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha Mjini barua nyingine yenye kumb. Na. CDM/AR/W/20.1/11 ambapo alimjulisha kwamba “msafara wetu utabaki kama tulivyoainisha kwenye barua (ya tarehe 31 Desemba 2010.)” Vile vile barua hiyo ilimjulisha Mkuu wa Polisi wa Wilaya juu ya “… vituo maalumu vya wananchi kukutana ili baada ya hapo waweze kujiunga na maandamano (msafara mkuu).” Nakala ya barua ya tarehe 2 Januari 2011 nayo imeambatanishwa kama Kielelezo ‘B’ kwenye maelezo haya.

Kwa ushahidi huu wa maandishi, ni wazi kwa hiyo kwamba kauli ya Waziri Mkuu kwamba Jeshi la Polisi la Wilaya ya Arusha Mjini ndio waliopendekeza njia ya maandamano ilikuwa ni ya uongo na/au ililenga kulidanganya Bunge.

Mheshimiwa Spika,

Mnamo tarehe 3 Januari 2011 viongozi wa CHADEMA wa Wilaya ya Arusha Mjini walikutana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha ili kujadili masuala mbali mbali yanayohusu maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 5 Januari. Moja ya mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ndani ya Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa ilikuwa ni kuchagua njia muafaka zaidi ya maandamano hayo. Kufuatia mazungumzo hayo, mnamo tarehe 4 Januari 2011 Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha SSP Zuberi Mwombeji alimwandikia Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini kumjulisha kwamba “kimsingi mmekubaliwa kufanya maandamano na mkutano wenu wa hadhara tarehe 5 Januari 2011….”

Katika barua hiyo, Mkuu wa Polisi aliitaka CHADEMA ichague moja kati ya njia mbili za maandamano ambazo zilijadiliwa na kukubaliwa katika mkutano wa tarehe 3 Januari, yaani njia ya “kuanzia Phillips, Sanawari Mataa, kushuka na barabara ya AICC, Goliondoi, Sokoine Road, Friends Corner na kuingia uwanja wa NMC”; au “kuanzia Phillips, sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stand, CRDB Bank, Friends’ Corner hadi uwanja wa NMC.” Nakala ya barua ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya yenye kumb. Na. AR/B.5/VOL.II/63 imeambatanishwa kama Kielelezo ‘C’ kwenye maelezo haya. Siku hiyo hiyo ya tarehe 4 Januari 2011 Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya alimtaarifu Mkuu wa Polisi Wilaya kwamba maandamano yangepitia njia ya Phillips, Sanawari Mataa, Mianzini Mataa, Florida Annex, Stendi Kuu ya Mabasi, CRDB Bank, Friends’ Corner na kuingia viwanja wa NMC – Unga Ltd.

Kufuatana na mtiririko huu wa matukio, sio kweli kwamba Polisi ndio waliopendekeza njia ya maandamano na wala sio kweli kwamba CHADEMA walikataa njia hiyo iliyopendekezwa na Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkuu Bungeni kwamba Polisi walipendekeza njia ya maandamano na CHADEMA wakaikataa ilikuwa ni kauli ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge.

3. UONGO WA TATU

Mheshimiwa Spika,

Aya ya tatu ya kauli ya Waziri Mkuu inadai kwamba Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA kihalali lakini CHADEMA wakaamua “… kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe.” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo na ilikuwa na lengo la kudanganya Bunge. Kwanza kabisa, utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga marufuku maandamano ulikuwa ni ukiukaji wa sheria husika za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi, mara baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya, njia pekee halali ya kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Sheria hiyo inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano wa hadhara hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo “isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.”

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika,

Kwa vyovyote vile, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa ni lazima itolewe na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na ni lazima iwe ni ya maandishi. CHADEMA haijawahi kupokea wala kuonyeshwa amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ya kupiga marufuku maandamano ambayo Mkuu huyo huyo wa Polisi wa Wilaya alikuwa ameyaruhusu kwa maandishi! Aidha, tumeona taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011 ambayo imedai kwamba CHADEMA iliandikiwa barua yenye kumb. Na. ARR/B.5/1/VOL.VIII/24 ya tarehe 4 Januari 2011 iliyoandikwa na “Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa mujibu wa sheria … kusitisha maandamano hayo ya CHADEMA….” Madai hayo hayana ukweli wala msingi wowote kisheria kwa sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote kisheria ya kusitisha au kupiga marufuku maandamano au mikutano ya hadhara. Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni ‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!

Aidha, tuna taarifa kwamba jioni ya tarehe 4 Januari 2011 Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na hautambuliwi kabisa na sheria hizo!

Mheshimiwa Spika,

Hata kama ‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza kuchukuliwa kisheria na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye amani na utulivu.’ Swali la kumuuliza Waziri Mkuu hapa ni kwamba kama kweli kulikuwa na ‘taarifa za kiintelijensia’ za uwezekano wa uvunjifu wa amani, kwa nini Jeshi la Polisi lililokuwa na taarifa hizo halikutoa ulinzi wa kutosha kwa waandamanaji?

Mheshimiwa Spika,

Hata kama maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Aidha, kwa mujibu ibara ya 64(5) ya Katiba, “… Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka mashrti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.” Hii ina maana kwamba hata kama Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa inaruhusu Jeshi la Polisi kukataza na/au kusitisha maandamano, Sheria hizo zitakuwa ni batili kwa kiasi cha ukiukwaji wao wa masharti ya ibara ya 20(1) ya Katiba inayotoa uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.

4. UONGO WA NNE

Mheshimiwa Spika,

Uongo wa nne aliousema Waziri Mkuu unahusu sababu ya kusitishwa kwa maandamano ya amani ya tarehe 5 Januari 2011. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka: “Sasa mkaamua kufanya maandamano yale bila kujali kabisa kwamba utaratibu uliokuwa wamekubaliana mmeukiuka wenyewe. Mheshimiwa Spika, sasa kilichotokea pale ni namna ya kuzuia hayo maandamano....” Kauli hii ya Waziri Mkuu ni ya uongo kwa sababu inapingana moja kwa moja na taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi tarehe 13 Januari 2011.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Jeshi la Polisi lilichukua hatua ya kuwaamuru waandamanaji kusitisha maandamano hayo mara moja baada ya kuona kwamba yataleta uvunjifu wa amani kutokana na jazba ya waandamanaji hao.” Wakati Waziri Mkuu – ambaye hakuwepo Arusha - anadai Bungeni kwamba maandamano yalisitishwa kwa sababu yalikiuka utaratibu, Jeshi la Polisi – lililokuwa na mamia ya askari polisi kwenye eneo la tukio – linasema kwenye taarifa rasmi kwamba maandamano hayo yalisitishwa kwa sababu ya jazba ya waandamanaji!. Taarifa ya IGP kama kielelezo “D”

5. UONGO WA TANO

Mheshimiwa Spika,

Uongo wa tano wa Waziri Mkuu unahusu kauli yake juu ya umbali kati ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha na mahali walipouawa waandamanaji watatu na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa mujibu wa Hansard, Waziri Mkuu alitamka yafuatayo kuhusu jambo hili: “Mpaka mmekaribia mita 50 muweze kuingia kituo cha Polisi. Police was left with no option kwa kujua tu kwamba kama mkiingia hatujui litakalotokea ni kitu gani. Katika purukushani ile, masikini wale marehemu wale watatu wakapoteza maisha.”

Kwa mara nyingine tena kauli ya Waziri Mkuu Bungeni inapingana na kauli ya Jeshi la Polisi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi hilo, “walipokaribia kituo Kikuu cha Polisi cha Kati umbali wa kama mita 50 huku wakirusha mawe, chupa, fimbo, nondo, mapanga na visu, amri halali na tahadhari za msingi zilizotolewa kuwataka watawanyike mara moja. Wafuasi hao walikaidi amri na kuzidi kukaribia kituo kwa lengo la kutimiza azma yao ya kukivamia.” Hapa maana ni kwamba waandamanaji walishapita huo umbali wa mita 50! Baada ya hapo, kufuatana na taarifa ya Jeshi la Polisi, hatua zifuatazo zilichukuliwa:
(i) Hatua ya kwanza, yalipigwa mabomu ya machozi, onyo ambalo lilipuuzwa na wakaendelea kusonga mbele;
(ii) Hatua ya pili, zilitumika risasi za baridi na mabomu ya vishindo bado walikaidi na kuzidi kukaribia kituo cha Polisi;
(iii) Hatua ya tatu, zilipigwa risasi juu za onyo bado wakaendelea kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya hatua zote hizo kushindikana kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, “kilichofuatia ni mapambano ya ana kwa ana kati ya askari na waandamanaji waliokuwa wakisonga mbele kuvamia kituo. Katika mazingira hayo risasi za moto ililazimika kutumika. Matokeo ya tafrani hiyo, watu 14 walijeruhiwa na kufikishwa hospitalini ambapo watatu kati yao walifariki dunia wakipatiwa matibabu.”

Mheshimiwa Spika,

Kama ni kweli hatua zote zilizoelezwa hapo juu zilichukuliwa na Jeshi la Polisi basi ni wazi kwamba watu waliouawa au kujeruhiwa waliuawa au kujeruhiwa kwenye uzio au mlango wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha! Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa kauli ya Waziri Mkuu, taarifa ya Jeshi la Polisi vile vile ni ya uongo mtupu. Kwa ushahidi wa picha za video tulio nao, marehemu mmoja aliuawa kwenye eneo la Mianzini ambalo liko zaidi ya kilometa tatu kutoka Kituo Kikuu cha Polisi cha Arusha. Aidha, marehemu wa pili alipigiwa risasi katika eneo la Kaloleni ambalo nalo liko zaidi ya kilometa moja kutoka kituo hicho. Ushahidi wa video unaungwa mkono na ushahidi wa watu walioshuhudia mauaji hayo wenyewe.

6. UONGO WA SITA

Mheshimiwa Spika,

Uongo wa sita wa Waziri Mkuu unatokana na kauli yake kwamba “... kama Mheshimiwa Mbowe na chama chako mngeliamua kushirikiana na Serikali hii mkafanya ule mkutano kama tulivyokubaliana haya yote yasingetokea.” Ukweli ni kwamba mkutano wenyewe uliohutubiwa na Dr. Wilbrod Slaa na Mheshimiwa Philemon Ndesamburo ulishambuliwa kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwashawasha na kutawanywa kabla ya makundi ya watu kurudi kwenye mkutano na Dr. Slaa na Mheshimiwa Ndesamburo kuendelea kuhutubia!

Aidha, ushahidi wa maandishi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha unaonyesha wazi kwamba CHADEMA walikubaliana na matakwa ya Jeshi la Polisi kwa kuchagua njia moja ya maandamano. Hata viongozi waliokamatwa wakati wa maandamano hayo walikamatiwa kati ya eneo la Sanawari na Mianzini wakiandamana kwa kutumia moja ya njia zilizopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya! Na gari iliyokuwa imewabeba Mheshimiwa Lucy Owenya na mke wa Dr. Slaa ilishambuliwa na kuvunjwa vioo na Mheshimiwa Owenya na Mama Slaa kuumizwa na askari polisi katika eneo la Sanawari Mataa wakati wakiwa katika njia ya maandamano iliyopendekezwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba, waliovunja makubaliano juu ya maandamano na mkutano wa hadhara walikuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ACP Thobias Andengenye na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema walioamua kuingilia maamuzi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha na kuyapiga marufuku maandamano hayo.

7. UONGO WA SABA

Mheshimiwa Spika,

Katika jibu lake kwa swali la Mheshimiwa Martha Umbulla, Waziri Mkuu alidai kwamba mkutano wa Baraza la Madiwani wa kumchagua Meya, Naibu Meya na Wenyeviti wa Kamati ulianza “wajumbe wote 31 wakiwepo....” Hii ni kauli ya uongo. Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Mikutano na Shughuli za Halmashauri ya Manispaa ya Arusha za 2003, “kila mjumbe anayehudhuria mkutano wa Halmashauri au Kamati yoyote ya Halmashauri ambamo yeye ni mjumbe ataweka sahihi yake kwenye Rejesta ya mahudhurio inayotunzwa na Mkurugenzi kwa ajili hiyo.” Kwa kufuatana na orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 17 Desemba, walikuwepo madiwani 16 wote wakiwa madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM)!

Kwa Waziri Mkuu kusimama na kuliambia Bunge kwamba wajumbe wote 31 wa Halmashauri ya Jiji la Arusha walikuwepo tarehe 17 Desemba 2010 wakati Rejesta ya mahudhurio inaonyesha kwamba ni wajumbe 16 tu ndio walioweka sahihi zao kwenye Rejesta hiyo ni uongo wa wazi. Angalia Kielelezo “E”

Mheshimiwa Spika,

Waziri Mkuu alitoa kauli ya uongo tena pale aliposema kwamba mgombea wa CCM alishinda kura za meya “walikuwa wanashindana mmoja wa CHADEMA, mmoja wa CCM.” Kwa mujibu wa orodha ya mahudhurio ya mkutano wa tarehe 18 Desemba 2010 uliomchagua Meya, waliokuwepo ni madiwani 17 ambao kati yao, 16 walikuwa wa CCM na mmoja alitoka chama cha TLP. Hakukuwepo na mjumbe hata mmoja wa CHADEMA. Na hii haishangazi kwa sababu ratiba ya mkutano huo inaonyesha kwamba siku ya tarehe 18 Desemba 2010 ilitakiwa kuwa siku ya mafunzo ya Madiwani yaliyokuwa yafanyike Olasiti Garden. Madiwani wa CHADEMA ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa tarehe 17 Desemba wasingeweza kujua kwamba ratiba ya mafunzo ilikuwa imebadilishwa na kuwa ratiba ya uchaguzi wa Meya! Ratiba ya shughuli za tarehe 18.12.2010 kielelezo “F”

8. UONGO WA NANE

Mheshimiwa Spika,

Uongo wa nane wa Waziri Mkuu ni kauli yake kwamba “... utaratibu uliofuatwa ulikuwa sahihi kabisa, haukukosewa kitu chochote. Meya ni halali kabisa, alipatikana kihalali kabisa.” Huu ni uongo mtupu. Chini ya kanuni ya 8(3) ya Kanuni za Halmashauri, “akidi katika mkutano wa kawaida wa mwaka na mkutano wa kwanza wa Halmashauri itakuwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri.” Kwa kusoma kanuni ya 8(3) pamoja na kanuni ya 9, ni wazi kwamba Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri wanatakiwa kuchaguliwa na mkutano wa kwanza wa Halmashauri. Ili kukidhi matakwa ya kanuni hizi, mkutano wa uchaguzi wa Meya na Makamu Meya wa Arusha ulipaswa kuwa si chini ya wajumbe 21 ambao ni theluthi mbili ya wajumbe wote wa Halmashauri hiyo. Kwa maana hiyo, mkutano wa tarehe 18 Desemba haukuwa mkutano halali na viongozi wa Halmashauri waliochaguliwa na mkutano huo hawawezi kuwa halali!

9. UONGO WA TISA

Mheshimiwa Spika,

Uongo wa tisa aliousema Waziri Mkuu Bungeni uko kwenye kauli ifuatayo: “Mheshimiwa Spika, yaani hata kwa hesabu tu za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza hakuna namna ambavyo kwa hali ilivyokuwa kwamba mna CHADEMA wajumbe 14, una CCM 16 utashindaje?” Hapa Waziri Mkuu alitaka kuaminisha Bunge kwamba hata kama wajumbe wa CHADEMA wangehudhuria kwenye mkutano huo bado wasingeshinda kwa sababu wajumbe wa CCM walikuwa wengi zaidi ya wajumbe wa CHADEMA. Lakini kwenye hotuba hiyo hiyo Waziri Mkuu alitoa kauli ifuatayo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri hiyo ya Arusha: “Wakaingia awamu ya pili ya kumtafuta Naibu Meya, wakapiga kura, Mjumbe wa kutoka TLP akashinda, CCM alishindwa hakupata kura hata moja, CHADEMA hawakupata kura hata moja...”!

Mheshimiwa Spika,

Kwa akili za kawaida za mtoto wa darasa la kwanza kama iliwezekana kwa mgombea wa TLP ambaye yuko peke yake katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kupata kura za wajumbe wote wa CCM na kumshinda mgombea wa CCM ambaye – kwa kauli ya Waziri Mkuu – hakupata kura hata moja, je, ingeshindikanaje kwa mgombea wa CHADEMA yenye wajumbe 14 kushinda? Swali ni muhimu hasa hasa kwa vile chini ya kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha inasema kwamba kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wake itakuwa ni ya siri! Na kama inavyofahamika, katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ni mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeshinda pamoja na kwamba CCM ina wajumbe wengi zaidi katika Halmashauri hiyo!

10. UONGO WA KUMI

Mheshimiwa Spika,

Waziri Mkuu aliulizwa swali la nyongeza na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kama Serikali iko tayari kuunda tume ya uchunguzi ya kimahakama kutafuta ukweli wa matukio ya Arusha na “... vile vile kuchukua hatua kwa wale wanaohusika.” Swali hilo liliulizwa pia na Mheshimiwa Martha J. Umbulla aliyetaka kujua kama Serikali itachukua hatua kuwaadhibu CHADEMA kwa kile alichokiita kuhusika na vurugu za Arusha “... ili tukio kama hilo lisirudie katika chaguzi za nchi yetu?” Waziri Mkuu alijibu: “Mimi nadhani hili ... wala si suala pengine la kusema ichukue hatua dhidi ya CHADEMA hapana.” Waziri Mkuu alitilia mkazo kwamba Serikali haina mpango wa kuwachukulia hatua CHADEMA kwa kusema: “Nataka niwaombe sana, hili hatuwezi kama Serikali tukasema tutaichukulia hatua CHADEMA....”. Angalia hansard ya tarehe 10-02-2011 kielelezo “G”

Mheshimiwa Spika,

Watanzania wawili na raia wa nchi jirani na yenye uhusiano mzuri na nchi yetu waliuawa wakati wa vurugu za Arusha. Watu wengine wengi walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, mabomu, virungu na mabuti ya polisi. Kama taarifa za Jeshi la Polisi na kauli ya Waziri Mkuu ni za kweli, vurugu hizo zilihusisha pia mashambulizi na uharibifu wa mali za Serikali kama vile vituo vya Polisi na mali za watu binafsi na za vyama vya siasa hususan CCM. Aidha, kama kauli ya Jeshi la Polisi nay a Waziri Mkuu ni za kuaminiwa, madhara yote haya yalitokana na uchochezi uliofanywa na viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA na ambao wametajwa kwa majina.

Mheshimiwa Spika,

Kama yote haya ni ya kweli na sio porojo za kisiasa, Watanzania wanapaswa kuambiwa ni kwa nini Serikali hii haiko tayari kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika na matukio haya? Kwa nini Serikali imeamua kwamba ni busara kuwafungulia mashtaka ya kosa dogo la kufanya maandamano kinyume cha sheria badala ya kuwashtaki kwa makosa makubwa kama kusababisha mauaji, au uchochezi, au kujaribu kuchoma majengo moto au makosa ya aina hiyo ambayo yana adhabu kubwa zaidi ya kosa waliloshtakiwa nalo? Kukataa kuchukua hatua stahili kuna tafsiri moja tu: CHADEMA hawakuhusika katika vurugu za Arusha na kwa hiyo kauli ya Waziri Mkuu Bungeni ni ya uongo na yenye lengo la kulidanganya Bunge!

HITIMISHO

Mheshimiwa Spika,

Kanuni ya 63(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, inasema “… ni marufuku kabisa kusema uongo Bungeni na kwa sababu hiyo, Mbunge yeyote anapokuwa akisema Bungeni ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni la kweli na siyo jambo la kubuni au la kubahatisha tu.” Hii pia ni msingi wa kanuni ya 64(1)(a) ya Kanuni za Bunge.

Kama nilivyothibitisha katika maelezo haya, Waziri Mkuu amesema uongo na/au kutoa taarifa ambazo hazina ukweli Bungeni. Kanuni ya 63(5) inaelekeza cha kufanya inapothibitika kuwa Mbunge amesema uongo Bungeni: “Spika au Mbunge mwingine yeyote, baada ya kutoa maelezo mafupi ya ushahidi unaotilia mashaka ya dhahiri kuhusu ukweli wa kauli au usemi au maelezo juu ya jambo au suala ambalo Mbunge amelisema Bungeni, anaweza kumdai Mbunge huyo atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo.” Naomba kuchukua nafasi hii kumtaka Waziri Mkuu atoe uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake Bungeni siku ya tarehe 10 Februari 2011 na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi au maelezo yake hayo na kutubu kwa Mungu!

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha!


Godbless Jonathan Lema

Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini

Thursday, February 17, 2011

Tamko la CHADEMA kuhusu Mabomu ya Gongo la Mboto

MAAFA YA GONGO LA MBOTO: WAZIRI WA ULINZI NA MKUU WA MAJESHI WAJIBIKE!

TAARIFA KWA UMMA
DODOMA, FEBRUARI 17, 2011

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) imeeleza kushtushwa na kusikitishwa na taarifa za
milipuko ya mabomu katika Ghala la Kuhifadhi Silaha la Kambi ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam
jana jioni.

Aidha, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewapa pole ndugu, jamaa, marafiki
na wananchi wote wa Tanzania kwa sababu ya maafa haya. Pia Kambi hiyo
imezitaka mamlaka zote za umma zinazohusika kuchukua hatua za haraka
kuhakikisha wananchi wote walioathirika na maafa haya wanapatiwa huduma zote
wanazohitaji katika kipindi hiki cha msiba huu. Hii ni pamoja na kuwapatia
huduma za maziko wale wote waliofariki, matibabu kwa waliojeruhiwa na
hifadhi kwa wale waliopoteza makazi yao. Aidha, ni muhimu kwa vyombo vya
usalama kuhakikisha ulinzi wa mali za wananchi katika maeneo yote
yaliyoathirika na ambazo zitakuwa hazina ulinzi baada ya wananchi kukimbia
maeneo yao.

Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeeleza kwamba tukio hili ni la
kushtusha na kusikitisha hasa kwa kuzingatia kwamba haijapita miaka miwili
tangu tukio la aina hiyo hiyo litokee katika Ghala ya Silaha ya Kambi
nyingine ya JWTZ katika eneo la Mbagala, Dar es Salaam, ambalo lilisababisha
vifo vya zaidi ya watu thelathini na uharibifu mkubwa wa mali za umma na za
wananchi binafsi. Aidha, milipuko ya Mbagala ilipelekea Serikali kutumia
mabilioni ya fedha za umma kwa ajili ya malipo ya fidia kutokana na vifo,
majeruhi na uharibifu wa mali binafsi za wananchi.

Akielezea tukio la milipuko ya Gongo la Mboto, Msemaji wa Ulinzi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Joseph Selasini alisema: “Milipuko ya Gongo
la Mboto inaonyesha dhahiri kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) haijajifunza lolote kutokana na maafa yaliyotokea Mbagala
mwaka juzi. Maana kama Serikali ingejifunza kutokana na maafa hayo
ingeshachukua hatua za dharura na za haraka kuhakikisha kwamba maafa ya aina
hii hayatokei tena.” Mh. Selasini alizitaja baadhi ya hatua hizo kama ni
pamoja na kuhamisha maghala yote ya silaha na mabomu yaliyo karibu na maeneo
wanayoishi raia na kuyapeleka katika Kambi za JWTZ zilizoko mbali kabisa na
maeneo ya raia. “Haiwezekani kwa Serikali kuendelea kuweka maghala ya silaha
katika Kambi za Jeshi zilizo karibu na wananchi na hivyo kuhatarisha maisha
yao namna hii”, alisema Mh. Selasini.

Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewataka Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa Dr. Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali
Davis Mwamunyange kujiuzulu mara moja ili kuwajibika kisiasa kutokana na
maafa ya Gongo la Mboto na ili kupisha uchunguzi huru na wa kina wa chanzo
na/au sababu za milipuko hiyo. Mh. Selasini alisema: “Dr. Hussein Mwinyi
alikuwa Waziri wa Ulinzi wakati wa maafa ya Mbagala; na Jenerali Mwamunyange
alikuwa Mkuu wa Majeshi. Maafa ya Mbagala yalitokea chini ya dhamana na/au
usimamizi wao. Na mara baada ya maafa hayo, Waziri Mwinyi na Jenerali
Mwamunyange waliliahidi taifa kwamba maafa ya aina hii hayatatokea tena.
Sasa yametokea. Inaelekea, kwa hiyo, kwamba ahadi yao ilikuwa sio ya kweli
na/au hawakuhakikisha kwamba inafanyiwa kazi ili iwe ya kweli. Viongozi hawa
hawana budi kuwajibika kwa hiari yao wenyewe au kuwajibishwa kama
itahitajika.”

Mh. Selasini aliongeza kusema kwamba hadi leo hakuna taarifa yoyote rasmi
iliyowahi kutolewa hadharani kwa wananchi na/au kwa wawakilishi wao Bungeni
ya chanzo na/au sababu za maafa hayo. “Hadi leo hii wananchi na/au
wawakilishi wao Bungeni hawajaambiwa kama kulikuwa na makosa ya makusudi
na/au ya uzembe na/au kama hatua zozote za kinidhamu na/au za kisheria
zilizochukuliwa dhidi ya mtu yeyote kutokana na kusababisha na/au kuwajibika
kwa maafa hayo. Jana maafa mengine ya aina hiyo hiyo yametokea tena na kwa
kadri ya taarifa rasmi ya Serikali watu wengi wameuawa na wengi wengine
kujeruhiwa na mali nyingi kuharibiwa. Kwa sababu hizo, huu ni wakati muafaka
kwa Dr. Mwinyi na Jenerali Mwamunyange kuonyesha uadilifu wao kwa kujiuzulu
nafasi zao ili kuwajibika kwa maafa haya.”

Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imependekeza iundwe Tume Huru ya
Uchunguzi na/au Kamati Teule ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili
kuchunguza kwa kina chanzo, sababu na madhara yote yaliyosababishwa na
milipuko ya Gongo la Mboto. “Kwa kuzingatia historia ya uchunguzi wa
milipuko iliyotokea Mbagala mwezi Aprili 2009, Tume Huru na/au Kamati Teule
ya Bunge lazima itoe taarifa yake hadharani kwa kupitia Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania”, alishauri Mh. Selasini.

Tuesday, February 1, 2011

TAMKO LA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHADEMA KUHUSU HALI YA TAIFA

TAMKO LA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HALI YA TAIFA.

Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika tarehe 29-30 Januari 2011 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe (Mb), pamoja na mambo mengine, imepokea, kujadili na kutolea maazimio Taarifa ya Hali ya Siasa na Taifa kwa ujumla. Maazimio haya yapo katika maeneo matano yafuatayo.

1. Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya.

Kamati Kuu imezingatia na kupongeza juhudi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wadau mbalimbali wa demokrasia nchini za kudai Katiba Mpya. Aidha, Kamati Kuu imejadili na kutafakari kwa kina maoni ya wadau mbalimbali juu ya mchakato unaofaa katika kupata Katiba Mpya, na kuzingatia kuwa njia sahihi ni ile itakayowashirikisha wananchi kikamilifu na kwa dhati bila kujali tofaui zao za kisiasa, dini, umri, elimu, kabila wala jinsia zao. Kamati Kuu imezingatia pia kwamba Tume ya Rais sio njia sahihi itakayowezesha upatikanaji wa Katiba Mpya yenye kuzingatia utashi, matakwa na mahitaji ya wananchi wa Tanzania. Hivyo basi:
  1. Kamati Kuu imepinga utaratibu wa kuunda Tume ya Rais katika uundaji wa Katiba Mpya
  2. Kamati Kuu imeunga mkono utaratibu wa kutumia Bunge katika kutengeneza na kusimamia mchakato utakaoletekeza upatikanaji wa Katiba Mpya
  3. Kamati Kuu imeipongeza Sekretariati yake kwa kumwagiza Mheshimiwa John Mnyika kuandaa na kuwakilisha Hoja Binafsi inayolitaka Bunge kuandaa sheria itakayoweka utaratibu na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya
  4. Kamati Kuu imewahimiza na kuwaomba wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunga mkono Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mnyika kwa maslahi ya Taifa.

2. Mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Jijini Arusha

Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya wananchi watatu wasio na hatia kwa kupigwa Risasi na askari wa Jeshi la Polisi kufuatia vurugu zilizosababishwa na Jeshi hilo katika harakati zao za kuzuia maandamano halali na yenye Baraka zote za Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilayani Arusha. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na uvurugwaji wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha kulikofanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa maelekezo ya Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Katika maazimio yake:
  1. Kamati Kuu imewapa pole ndugu wa wafiwa wa vurugu za Arusha pamoja na wananchi wa Arusha na watanzania kwa ujumla
  2. Kamati Kuu imewapongeza Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mhe Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willibrod Peter Slaa, Mbunge wa Arusha Mjini Mhe Godbless Lema na viongozi wengine wa CHADEMA kwa juhudi zao kubwa za kuepusha shari na kutoa uongozi wa kisiasa pale ambapo wananchi wa Arusha walitelekezwa na viongozi wa Serikali ya CCM katika kipindi chote cha matatizo ya Arusha
  3. Kamati Kuu imeiagiza sekretariati ya CHADEMA kuendelea na harakati za kudai haki za wananchi wa Jiji la Arusha kwa njia za kisiasa.
  4. Kamati Kuu imewaagiza madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuingia katika vikao vya Baraza la Halmahauri hiyo na kuwawakilisha wananchi waliowachagua kikamilifu na wahakikishe kuwa wanatumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa Meya.

3. Matatizo ya Nishati ya Umeme na Gesi na Malipo kwa Kampuni Hewa ya Dowans

Kamati Kuu imesikitishwa na kupanda holela kwa bei za nishati muhimu za umeme na gesi, pamoja na kushindwa kwa serikali ya CCM katika kuwekeza kikamilifu katika sekta ya nishati hapa nchini. Aidha, Kamati Kuu imesikitishwa na kufadhaishwa sana na uamuzi wa CCM na serikali yake kuridhia kuilipa Kampuni hewa ya Dowans fedha za walipa kodi wa Tanzania zipatazo Shilingi bilioni 94, pamoja na kwamba Kampuni hii ilikwishaharamishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi.

Kamati Kuu imetambua kuwa sakata la Dowans ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi ndani ya CCM na serikali yake ambavyo vimeligharimu taifa hili kwa miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:
  1. Kamati Kuu imewahimiza wana CHADEMA, wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kupinga kwa nguvu zote malipo ya Dowans
  2. Kamati Kuu imewaelekeza viongozi pamoja na wabunge wa CHADEMA kuendelea kuwahamasisha wananchi kupinga kwa njia mbalimbali za kisiasa na kisheria malipo ya Dowans na ufisadi mwingine hapa nchini
  3. Kamati Kuu imewapongeza na kuwashukuru wanaharakati wa taasisi za kiraia kwa ujasiri na moyo wao wa kizalendo kwa uamuzi wao wa kufungua kesi mahakamani ya kupinga malipo ya Dowans
  4. Kamati Kuu imeiasa Serikali ya CCM kutokuona aibu kutekeleza sera za CHADEMA zilizofanyiwa utafiti kuhusu namna ya kujenga na kuimarisha sekta ya nishati ya umeme na gesi hapa nchini ili nchi yetu iondokane na tatizo la kudumu la umeme.
  5. Kamati Kuu imeiagiza Secretariat yake kuanza maandalizi ya maandamano ya nchi nzima ya kupinga ongezeko la bei ya umeme, gesi na kuilipa Dowans. Na tarehe 24/02/2011 itakuwa siku ya kuanza maandamano kwenye Jiji la Mwanza na miji mingine kadiri ratiba itakavyotolewa.

4. Matokeo ya Kidato cha Nne

Kamati Kuu imeyapokea kwa masikitiko makubwa matokeo ya Kidato cha Nne yanayoonyesha kuwa nusu ya watahaniwa wote wamefeli Mtihani huo. Aidha, Kamati Kuu imezingatia na kusikitishwa na taarifa kuwa ni
asilimia 11.5 tu ya watahiniwa ndio waliopata daraja la I hadi la III. Ndio kusema kuwa karibu asilimia 90 ya vijana wote waliomaliza kidato cha nne mwaka 2010 hawawezi kuendelea na elimu yeyote ya juu na itakuwa ni vigumu sana kwa vijana hawa kupata aina yeyote ya ajira ya uhakika.

Aidha, Kamati Kuu imezingatia kuwa matokeo mabaya ya Kidato cha Nne yamesababishwa na sera dhaifu za serikali ya CCM zenye kulenga kughilibu wananchi kwa ajili ya mafanikio ya kisiasa kwa kukazania wingi wa majengo ya shule badala ya ubora wa walimu na ubora wa shule. Kutokana na hali hii:
  1. Kamati Kuu imeyatangaza matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2010 kuwa ni Janga la Kitaifa
  2. Kamati Kuu imeitaka Serikali ya CCM isione aibu kutekeleza sera za elimu za CHADEMA zilizoanishwa katika ilani yake ya mwaka 2010, ikiwemo sera ya kutoa elimu bure na kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya walimu ambazo zilielezwa na wataalamu wa elimu kwamba ndio sera sahihi za kufufua ubora wa elimu ya nchi yetu
  3. Kamati Kuu imeunda timu maalumu ya wataalamu wa elimu kwa ajili ya kutafiti kwa kina sababu za matokeo mabaya ya Kidato cha Nne na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu katika kikao chake kitakachofanyika kabla ya Mwezi Mei 2011.

5. Kuhusu propaganda za udini hapa nchini

Kamati Kuu imesikitishwa na propaganda zinaendelezwa na viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi, hususani Rais Kikwete, kuhusu kuwepo kwa mfarakano wa kidini hapa nchini. Kamati Kuu imezingatia kuwa wananchi wa Tanzania wameendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano mkubwa bila kujali tofauti zao za kidini. Kamati Kuu imezingatia kuwa Viongozi wa juu wa CCM, na hasa Rais Kikwete, ameamua kuficha udhaifu wake wa kiuongozi chini ya zulia la udini ili wananchi waache kujadili mambo ya msingi ya Taifa hili, ikiwemo kushindwa kwa CCM kutekeleza ahadi ambazo imekuwa ikizitoa katika miongo mitano iliyopita. Hivyo basi:
  1. Kamati Kuu imewahimiza wananchi wa dini zote hapa nchini kuendelea kuishi kwa amani na mshikamano na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii bila kujali tofauti zao za dini, ukabila wala itikadi ya siasa
  2. Kamati Kuu imewataka viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete kuacha kuchochea mgawanyiko wa dini hapa nchini kama njia ya kuficha udhaifu wake wa uongozi
  3. Kamati Kuu imewahimiza viongozi wa dini zote hapa nchini kuendelea kukemea maovu yeyote katika jamii bila woga wala upendeleo kwani hilo ni jukumu lao la msingi.

6. Kuhusu Ushirikiano wa Vyama vya Siasa vya Upinzani

Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa
Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja Kitaifa Zanzibar, na kwa kuwa Sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za Muungano, na kwa kuwa vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge wamo katika ushirikiano na CUF, Kamati Kuu imeona kuwa CHADEMA haiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo. Hivyo basi Kamati Kuu imemwagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kuunda Baraza la Kivuli kwa kuhusisha wabunge wa CHADEMA pekee.




7. Kuhusu mpango mkakati wa chama 2011-2016.

Kamati Kuu ilijadili na kupitisha mapendekezo ya mpango kazi wa chama kwenye Baraza kuu la chama .Pia ilijadili na kupitisha mpango kazi wa mwaka 2011-2012.

Tamko hili limetolewa leo tarehe 31/01/2011.

Dk Willibrod Peter Slaa
Katibu Mkuu

Monday, January 24, 2011

TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO CHADEMA MKOA WA DODOMA KULAANI MATUMIZI MABAYA YA NGUVU ZA POLISI MKOANI ARUSHA

TAMKO LA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
CHADEMA MKOA WA DODOMA KULAANI MATUMIZI MABAYA YA NGUVU ZA POLISI MKOANI ARUSHA NA KUSABABISHA MAUAJI YA RAIA WASIO NA HATIA.

UTANGULIZI.
Ndugu Mgeni rasmi, awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema na uzima anaozidi kutujalia. Tumekusanyika hapa leo hii kwa Amani, ili kuweza kuunga mkono Tamko la CHADEMA Taifa juu ya mauaji ya Raia watatu (1) Denis M. Shirima (2) Ismail Omari (3) Paulo Njuguna (Mkenya) wasiokuwa na hatia yaliyofanywa na Serikali dhalimu kupitia Jeshi la Polisi Mkoani Arusha. Lakini pia tunawapa pole wale wote waliofikwa na maafa mbalimbali yaliyosababishwa na vurugu zilizoanzishwa na Jeshi la Polisi

TUSIMAME KWA DAKIKA 1 KUWAKUMBUKA MASHUJAA HAO WATATU WALIOPOTEZA MAISHA.

MSIMAMO WA CHADEMA DODOMA JUU YA MAUAJI YA RAIA ARUSHA.

Ndugu Mgeni rasmi, CHADEMA (Mkoani Dodoma) tunaamini kabisa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 20 (1) na Tamko la haki za binadamu la umoja wa Mataifa ya mwaka 1948, (yaani Universal Declaration of Human Rights) kuwa ni haki ya msingi ya kila Raia kuandamana kwa Amani ndani ya Nchi yake. Na Jeshi la Polisi kuwa kama nyenzo ya kulinda Amani na si kuvuruga Amani. Hii ni haki ya kikatiba ya wananchi wa Tanzania.

Ndugu Mgeni rasmi, imekuwa tabia ya CCM na Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuwapora Raia wa Tanzania haki zao za msingi na za Kikatiba kwa kisingizio cha kuvurugika kwa Amani,jambo ambalo halivumiliki na halikubaliki. Watanzania wamejua na wanaamini kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwalinda wao (Wananchi) na mali zao. Jeshi la Polisi kwa sasa limekuwa chombo cha kuvuruga Amani na kupora mali za Watanzania kwa kisingizio cha maono ya “kiintelijensia”. Je Intelejensia” hiyo haiwezi kutumika kwa kutazama madhara ya kuzuia maandamano hayo ya Amani? Maandamano ya mazishi ya wahanga wa mauaji ya Arusha ni ushahidi tosha kuwa dhana ya inteligensia ni fikra potofu na hupikwa na kikundi kidogo cha watu kwa ajili ya maslahi yao.



Ndugu Mgeni rasmi, CHADEMA Dodoma, Tunawapa pole Ndugu na jamaa za mashujaa waliopoteza maisha katika harakati za kudai haki zao na za Watanzania wote kwa ujumla. Vilevile tunawapa pole majeruhi wote walioumizwa na Jeshi la Polisi linalotaka kuingiza Tanzania katika machafuko makubwa. Tunawaombea majeruhi wote wapone haraka na kuwataka wasikate tamaa badala yake waendeleze mapambano mpaka kufikia lengo.

Ndugu Mgeni rasmi, Tunawapa pole na pongezi za dhati Viongozi wetu makini wa chama kitaifa Mwenyekiti Freeman Aikaeli Mbowe, na Katibu Mkuu Dr Wilbrod Peter Slaa, (Katibu Mkuu Taifa), na Wabunge wa majimbo na wa viti maalumu wa CHADEMA walioongoza mapambano dhidi ya Serikali dhalimu inayotumia nguvu nyingi na kodi za Watanzania waliopigika kupora haki zao.

Ndugu Mgeni rasmi, CHADEMA DODOMA tunalaani nguvu za kivita zilizotumiwa na Jeshi la Polisi Mkoani Arusha KUPAMBANA NA RAIA WASIO NA SILAHA WALIOBEBA MAJANI NA VITAMBAA VYEUPE, jambo lililopelekea mauaji ya watu watatu wasiokuwa na hatia na kupelekea wengine wengi kubaki vilema na majeraha yasiyokuwa ya lazima. Tunaungana na Viongozi wetu wa CHADEMA Kitaifa kulitaka Jeshi la Polisi kwanza kuwaomba radhi Watanzania kwa kusababisha majonzi makubwa yaliyogharimu maisha ya Ndugu zao, pili kuwataka wahusika wakuu waliosababisha vurugu hizo kuwajibika wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nchi Ndugu

Shamshi Vuai Nahodha, akifuatiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema au Bwana “Intelijensia” na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha (RPC) Thobias Andengenye.

Ndugu Mgeni rasmi, Tunalitaka Jeshi la Polisi nchini kutoendeleza tabia ya kuwanyanyasa Wana wa nchi hii (Watanzania) kwa sababu ya maslahi ya watu wachache hasa Viongozi wa CCM, kinyume na hapo wao watakuwa wa kwanza kuhukumiwa kwa tabia hiyo, kwani Watanzania watashindwa kuvumilia. Tunalisihi Jeshi la Polisi kutoa Ulinzi na kuhakikisha usalama wa Watanzania hasa pale wanapotaka kupaza sauti zao kwa njia ya maandamano ya Amani. Polisi kamwe hawajapata mamlaka ya kisheria ya kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano bali kuweka ulinzi na kuhakikisha sauti za watanzania zinafika mahali husika. Kupitia hadhara hii tunatangaza kusimamia haki zetu.

Sisi kama Watanzania tunaliagiza Jeshi la Polisi kuacha mara moja tabia ya kukurupuka na kutumia silaha nzito kwa Watanzania

wasiokuwa na hatia (vurugu) pindi wanapodai haki zao. Maandamano kama yale ya Arusha na ya wanavyuo mfano Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yalikuwa ya amani na hayakustahili kukambiliana na mashambulizi ya kivita! Tunawapa pole watanzania wote waliokumbana na mikikimikiki kutoka kwa Jeshi la Polisi.
NINI CHANZO CHA JEURI YA JESHI LA POLISI.
Ndugu mgeni rasmi , CHADEMA DODOMA tunaamini kabisa kuwa jeuri ya jeshi hili la polisi linatokana na mambo makuu matatu:-
· Kwanza ni kutokuwa na katiba inayoeleza wazi zile haki za msingi za mtanzania na nguvu zake katika kutetea haki hizo.
· Pili ni kutokuwa na viongozi makini na wenye uwezo wa kuthubutu kuheshimu haki za watanzania, wakiongozwa na viongozi wa CCM .
· Tatu ni dharau na ukatili wa viongozi wa jeshi hilo waliokengeuka na kujengeka kifikra kwamba vyeo au madaraka wanayoyapata yametokana na uswahiba wao na viongozi wakuu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi!

Ndugu mgeni rasmi , sababu hizo, msingi wake hasa ni ubovu wa katiba yetu inayotoa mwanya kwa viongozi wa serikali na jeshi la polisi kutokuheshimu UMMA wa watanzania kwa kuwa katiba hiyo ilitungwa na watu wachache, kwa maslahi ya watu hao wachache na si watanzania wote.

Hivyo basi tunaisihi Serikali na kuitaka kuanzisha mara moja mchakato wa katiba mpya ( siyo marekebisho ) itakayotoa fursa kwa kila mwana wa nchi hii kueleza wazi hasa wanahitaji katiba ya aina gani kwa mstakabali wa Taifa hili.



Ndugu mgeni rasmi, tunapenda kutoa angalizo kwa Serikali kuwa, kutowashirikisha watanzania katika maamuzi juu ya katiba mpya kunaweza kulifikisha Taifa hili katika historia chafu ambayo haijawahi kutokea. Dalili za uchafu huu wa historia zimeanza kuonekana kwa kuwa ni tabia ya Serikali ya CCM kuwapuuza watanzania. Tunasisitiza hili “ Maamuzi ya watanzania yaheshimiwe”.

Ndugu mgeni rasmi , CHADEMA DODOMA tunaungana na Viongozi wetu kitaifa kuwasihi na kuwahamasisha watanzania kudai katiba mpya itakayoweka bayana ni Taifa gani wanalolihitaji watanzania. Tunaungana na umma wa watanzania wote kudai uandikwaji wa katiba utakaoongozwa na BARAZA LA KATIBA na kupinga tume inayotaka kuundwa na Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete. Tunasisitiza kuwa zoezi hili lianze mara moja ili kuzuia uwezekano wa uharibifu wa maendeleo na ustawi wa jamii kuendelea kujitokeza. Haya ni maangamizi kwa taifa. Ndugu mgeni rasmi, ni dhahiri kuwa katiba hii tuliyonayo sasa hivi ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya Taifa letu!

Ndugu mgeni rasmi. Tunaomba watanzania waendelee kuwa imara pasipo kutetereka katika kudai haki zao za msingi na kuendelea

kuwakumbuka Ndugu zetu mashujaa walioandika historia katika nchi hii kwa kufa kishujaa walipokuwa wakitetea haki zao na za watanzania wote kwa ujumla. Tunaomba watanzania wote kuendelea


kudumisha amani tuliyonayo ijapokuwa Serikali na jeshi lake la polisi wanataka na wameanza kuvuruga Amani hiyo.

Ndugu mgeni rasmi, tunalisihi jeshi la polisi kuelekeza nguvu zake na silaha zake nzito nzito kupambana na wahalifu wanaosumbua nchi hii kama majambazi na mafisadi yanayofilisi nchi na siyo kuwa warahisi wa kuwapiga mabomu watanzania waliokuwa huru ndani ya nchi yao kwa kipindi kirefu.

Pia tunaliomba jeshi la polisi kuelekeza nguvu zake za “Kiintelijensia” katika kutabiri na kugundua madhara na athari za mikataba inayoingiwa na Serikali (hilo ndilo la msingi kwa watanzania). Kama vile Dowans, Meremeta, Kagoda kwa kutaja machache tu.

Tunalitaka jeshi la polisi lijenge utamaduni wa kusema ukweli na kuondokana na utamaduni wa kuwabambikia raia kesi mbalimbali ambazo haziwahusu. Mfano wa hili ni mbinu chafu ambazo zinaendelea chini ya jeshi la polisi kuhariri na kurusha kwenye runinga picha zinazoonyesha kuwa CHADEMA ndio chanzo cha vurugu za Arusha! Umma mzima umeshuhudia kuwa maandamano yalikuwa ya amani kwa urefu wa kilomita mbili hadi pale polisi kwa makusudi walipoamua kuanzisha vurugu kwa kuwashambulia waandamanaji kwa

mabomu na risasi za moto. Mkanda huu lakini haukuonyesha polisi walivyodhalilisha na kunyanyasa raia waliowapiga, kuvunja vioo vya

magari, na kupora mali za raia. Tunamtaka kamanda Paul Chagonja kwa niaba ya polisi kuuomba radhi umma wa watanzania kwa juhudi zake za makusudi za kupotosha ukweli na kutetea uovu mkubwa uliofanywa na jeshi la polisi. Tunasisitiza kuwe na tume huru ya kuchunguza mauaji haya. Pia tunasisitiza kuwa viongozi wa CHADEMA na watu wote waliobambikiwa shauri hili wafutiwe kesi, na waachiwe huru bila ya masharti yoyote.

Tunamtaka pia Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda atamke rasmi tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi halali wa Meya wa Jiji la Arusha. Tunamtaka Mh. Pinda atumie wepesi ule ule alioutumia kusimamisha uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Kigoma baada ya kulalamikiwa na Chama Cha Mapinduzi. Katika tukio hili Mh. Pinda aliweza hata kupora uhuru wa mahakama na kusimamisha uchaguzi. Maendeleo ya wananchi ni zaidi ya vyeo vinavyong’ang’aniwa na Chama Cha Mapinduzi.

CHADEMA inatoa rai kwa raia wote wa Tanzania kusimama kidete kwa ajili ya haki na maendeleo ya taifa lao. Watanzania wa kada mbalimbali wake kwa waume, wazee kwa vijana, wawe wanasiasa, wasomi, wafanyabiashara, wanafunzi, wakulima na wafanyakazi kuungana mkono na kuhakikisha ustawi wa nchi yetu hauwekwi rehani kwa maslahi ya watu wachache. Tunapaswa kuulinda na kuutetea ustawi wa nchi yetu kwa maslahi ya kizazi hiki na kile kijacho.



Ndugu mgeni rasmi, tunamalizia kwa kusema “Jeshi la polisi litambue kuwa kwa kupitia kodi za raia wa Tanzania, ndipo mishahara yao na posho zinalipwa, pia zana za kazi zao zinanunuliwa. Jeshi la polisi
liwaheshimu watanzania kwani lipo kwa ajili ya kuwalinda wao na mali zao na sio kuwatia ulemavu na kuwapotezea maisha.

Tanzania bila ubabe inawezekana!

Ndugu mgeni rasmi; tunaomba kuwasilisha hoja
MUNGU IBARIKI CHADEMA
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA

“Mungu warehemu mashujaa wetu hawa ISMAL OMAR, DENIS MICHAEL na PAULO NJUGUNA (Mkenya ) wapumzike kwa amani.
TUNAJIVUNIA NGUVU YA UMMA.
PEOPLE’S POWER
__________________________
Steven E. Masawe
KATIBU MKOA
CHADEMA.

Thursday, January 13, 2011

Juu ya Mauaji ya Wananchi wakati wa Maandamano ya Amani yaliyofanyika Arusha

Tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Juu ya Mauaji ya Wananchi wakati wa Maandamano ya Amani yaliyofanyika Arusha tarehe 5 Jan, 2011

UTANGULIZI

Tumekutana hapa leo hii kwa huzuni kubwa. Tumekutana hapa leo hii kwa sababu watoto wa familia mbili wamepoteza baba zao na mama wa familia hizo wamepoteza waume na wenzi wao wa maisha. Tumekutana hapa leo kwa sababu wazazi wa familia mbili wamepotelewa na watoto wao wa kiume. Tumekutana hapa leo kwa sababu kuna familia nyingine – kwa sababu taarifa zetu za awali zinaonyesha watu wengine zaidi wameuawa - zimepotelewa na wapendwa wao vile vile.

Tumekutana hapa leo kwa sababu mamia ya wananchi wa Jiji hili wameumizwa kwa kupigwa risasi za moto, kupigwa mabomu ya machozi na/au kupigwa kwa virungu na mabuti ya Jeshi la Polisi la Tanzania. Tumekutana hapa leo kwa sababu wote waliokufa na tunaowaomboleza leo na wote walioumizwa na/au kuharibiwa mali zao hawakufikwa na mauti na/au majanga hayo kwa ajali ya barabarani au tetemeko la ardhi. Tumekutana hapa kwa sababu wote waliofikwa na mauti wameuawa na wote walioumia wameumizwa na Jeshi la Polisi la Tanzania.

Tumekutana hapa leo kwa sababu Jeshi la Polisi la Tanzania halipaswi, na halikupaswa, kuua wananchi wasiokuwa na hatia yoyote na ambao walikuwa wanatumia haki yao ya kufanya maandamano ya amani inayotambuliwa na Katiba na sheria za nchi yetu. Na tumekutana hapa leo ili kulinda na kutetea haki hiyo na kuzuia nchi yetu kuwa dola ya kipolisi inayoendeshwa kwa amri za kijeshi na za watawala na sio kwa matakwa ya wananchi.

Lakini, ndugu wananchi wa Arusha, tumekutana hapa ili kuomboleza kwa pamoja na tunahitaji kuomboleza kwa amani. Kwenye msiba watu hawapigani na tunawaomba tusipigane kwenye msiba huu. Kwenye msiba watu hawafanyi fujo na tunawaomba tusifanye fujo kwenye msiba huu. Tunawaomba tuomboleze kwa amani ili tusiwape wale walioua ndugu zetu sababu ya kusema kwamba sisi tunapenda fujo na uvunjifu wa amani.

SIKU YA KIHISTORIA

Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Jiji la Arusha. Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Tanzania. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania – ambalo limepewa wajibu wa kisheria wa ‘kulinda amani, sheria na utulivu, kugundua na kuzuia uhalifu, kukamata na kudhibiti wahalifu na kulinda mali za wananchi – liliamua kwa makusudi kuacha kutimiza wajibu wake kisheria na kujipa wajibu mwingine wa kuwa ni Jeshi la kuvunja amani, kukiuka sheria, kuvuruga utulivu, kufanya uhalifu na kuharibu mali za wananchi. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania – ambalo limejipachika kauli mbiu ya ‘Ulinzi wa Raia na Mali Zao’ – liliamua kwa makusudi kubadili kauli mbiu yake kuwa ni ‘Mauaji ya Raia na uharibifu wa mali zao’!

Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo wananchi wa Jiji la Arusha walivamiwa kwa makusudi, waliuawa kikatili na kupigwa na kuumizwa bila kosa au sababu yoyote ya msingi. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania lilitumia silaha kubwa kubwa – risasi za moto, mabomu ya machozi na magari ya maji ya kuwasha – dhidi ya raia waliokuwa na vitambaa vyeupe vyenye kuashiria amani. Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo – kama ilivyokuwa tarehe 26 na 27 Januari 2001 – Jeshi la Polisi la Tanzania lilitukumbusha tena kwamba liko tayari kumwaga damu ya Watanzania wasiokuwa na hatia ili kulinda wizi wa kura na unyongaji wa demokrasia unaofanywa na watawala wa Chama cha Mapinduzi.

Kama ilivyokuwa Zanzibar miaka kumi iliyopita ndivyo ambavyo imekuwa Arusha mwaka huu: tumeanza Mwaka Mpya kwa umwagaji wa damu na maombolezo badala ya sherehe na kutakiana heri! Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa Zanzibar baada ya mauaji ya Januari 2001, CHADEMA haitakubali kununuliwa au kunyamazishwa kwa kuvikwa vilemba vya ukoka na/au kupewa vipande thelathini vya fedha ili kunyamazia mauaji ya wananchi wetu: Mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia hayatazuia jitihada za kujikomboa kutoka kwenye makucha ya utawala wa CCM. Mti wa haki uliorutubishwa kwa damu isiyokuwa na hatia ya wananchi wa Arusha utaendelea kukua na kuenea Tanzania nzima. Tarehe 5 Januari 2011 itakuwa siku itakayokumbukwa katika historia ya nchi yetu kama ni siku ambayo jitihada za ukombozi wa nchi yetu zilipata msukumo mkubwa.

MAANDAMANO HALALI

Jeshi la Polisi lilijua kwamba kutakuwa na maandamano ya amani ambayo yangefuatiwa na mkutano wa hadhara. Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu njia na/au barabara za Jiji la Arusha ambazo maandano hayo ya amani yangepitia hadi kufika kwenye eneo la Viwanja vya NMC ambako mkutano wa hadhara ungefanyika. Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu muda wa kuanza maandamano hayo ya amani na muda wa kumalizika kwa mkutano wa hadhara.

Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu yote hayo sio kwa sababu ya ‘taarifa za kiintelijensia’ ambayo ndio imekuwa kisingizio cha Jeshi la Polisi la Tanzania kukanyaga haki za kikatiba za wananchi wa Tanzania kupinga serikali ya CCM kwa njia za amani kwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Jeshi la Polisi la Tanzania lilifahamu yote hayo kwa sababu Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilifuata taratibu zote za kisheria za kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Tarehe 3 Januari 2011 CHADEMA ilitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kuhusu nia yake ya kufanya maandano ya amani yatakayofuatiwa na mkutano wa hadhara ili kupinga kitendo cha watawala wa CCM kuwalazimishia wananchi wa Jiji la Arusha Meya ya Jiji kwa njia za kiharamia.

Tarehe hiyo hiyo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha alifanya kikao na viongozi wa CHADEMA kwa lengo la kukubaliana njia na/au barabara zitakazotumiwa na waandamanaji hadi kufikia Viwanja vya NMC. Baada ya hapo, pamoja na kwamba hakuwa na haja ya kisheria ya kufanya hivyo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha aliifahamisha CHADEMA kwa maandishi kwamba maandamano yetu ya amani na mkutano wa hadhara yalikuwa yameruhusiwa na Jeshi la Polisi la Tanzania. Hatua zote tulizozichukua na ambazo tumezitaja hapa zilifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na vile vile kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Lakini hata kabla ya hapo, Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linajua kwamba CHADEMA ingefanya maandamano ya amani kushinikiza utekelezaji wa madai yetu tuliyoyatoa kwa maandishi kwa serikali na nakala yake kupatiwa Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema mnamo tarehe 23 Desemba 2010. Katika barua yake, CHADEMA ilidai kwamba uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ufutwe na kurudiwa; Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Jiji afukuzwe kazi kwa kushiriki katika ukiukwaji wa sheria za uchaguzi wa viongozi wa halmashauri za serikali za mitaa; na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha avuliwe madaraka yake kwa kushiriki kumpiga Mbunge wetu wa Jimbo la Arusha Mjini aliyekuwa anajaribu kutetea sheria za nchi yetu za uchaguzi wa viongozi wa halmashauri za serikali za mitaa.

CHADEMA ilitoa nafasi ya wiki mbili kwa serikali kutekeleza madai hayo la sivyo ingeandaa maandamano ya amani ya wananchi wa Arusha. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba CHADEMA haikukimbilia kuandaa maandamano hata kama haikuwa kosa dhidi ya sheria za Tanzania kufanya hivyo. Kabla ya matukio ya maandamano ya tarehe 5 Januari, CHADEMA ilishaweka wazi utayari wake wa kumaliza mgogoro wa Arusha kwa njia za mazungumzo. Barua yetu ya tarehe 23 Desemba 2010 kwa serikali na kwa Jeshi la Polisi la Tanzania haijajibiwa hadi leo hii!

JESHI LA WAHALIFU!

Baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa mujibu wa sheria zilizotajwa, njia pekee halali ya kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Na Sheria ya Jeshi la Polisi inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo ‘isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.’

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma katika eneo husika. Kwa vyovyote vile kwa mujibu wa sheria hizi mbili, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa ni lazima iwe ni ya maandishi.

Na hata kama ‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza kuchukuliwa na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye amani na utulivu.’

Jeshi la Polisi la Tanzania lilikiuka kwa makusudi masharti haya ya sheria. Kwanza, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ambaye ndiye ofisa anayetakiwa kupatiwa taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara hakuwahi kuipa CHADEMA taarifa yoyote ya maandishi ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa rasmi kwake kwa mujibu wa sheria. Taarifa na/au amri pekee tunayoisikia ya kuzuia na/au kusitisha maandamano ni ile inayosemekana ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha jioni ya tarehe 4 Januari 2011. Taarifa na/au amri hiyo – kama kweli ilikuwepo - ilikuwa ni haramu kwa sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote ya kuruhusu au kukataza maandamano na/au mikutano ya vyama vya siasa. Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni ‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!

Aidha, tuna taarifa kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na hautambuliwi kabisa na sheria hizo!

Lakini hata kama maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Hii ina maana kwamba uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara umepanuliwa sana na hauwezi kupokonywa kihalali kwa visingizio vya ‘taarifa za kiintelijensia’ vya Jeshi la Polisi la Tanzania.

Kwa hiyo wananchi wa Arusha walivamiwa na kupigwa risasi zilizowaua au kuwajeruhi sio kwa sababu walikuwa wamevunja sheria yoyote ya Tanzania. Walivamiwa na kuuawa au kujeruhiwa na mali zao kuharibiwa sio kwa sababu walifanya kosa lolote linalotambuliwa na sheria za nchi yetu. Viongozi wa CHADEMA kuanzia ngazi za juu za kitaifa hadi ngazi za chini na wanachama wetu wa kawaida walishambuliwa kwa risasi na mabomu na baadaye kujazwa kwenye mahabusu za polisi sio kwa sababu walikiuka sheria yoyote. Wananchi wa Arusha walifanyiwa uhalifu wote huo licha ya kwamba Katiba ya nchi yetu inatambua na kulinda uhuru wa wananchi wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.

MAUAJI YA KUPANGWA

Mauaji ya Arusha yalifanywa kwa makusudi na kwa kupangwa. Jeshi la Polisi la Tanzania lilipanga na kutekeleza mauaji hayo. Lakini sio Jeshi la Polisi la Tanzania pekee lenye kuhusika na mauaji ya wananchi wetu. Rais Kikwete na serikali yake na chama chake cha CCM wanahusika moja kwa moja na damu iliyomwagwa kwa makusudi Arusha. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kikwete ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama. Aidha, chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi – ambaye ni mteuliwa wa Rais – anawajibika kufuata amri na maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani – mteuliwa mwingine wa Rais – kuhusiana na udhibiti wa shughuli za Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kikatiba na kisheria, Jeshi la Polisi liko chini ya mamlaka ya Rais na wateuliwa wake kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Pamoja na mamlaka ya Rais juu ya Jeshi la Polisi, Kikwete mwenyewe alikwishatoa kauli na matamko hadharani ambayo yaliashiria kwamba Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linajiandaa kumwaga damu ya Watanzania ili kulinda utawala wake na wa chama chake. Kwa mfano, katika hotuba yake ya Mwaka Mpya aliyoitoa usiku wa tarehe 31 Desemba 2010, Kikwete alidai kwamba ‘… wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa … wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara…. Wao hasa wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya dola kuingilia ati waiambie jumuiya ya kimataifa jinsi Serikali yetu ilivyo katili.’ Katiba hotuba hiyo, Kikwete alizungumzia kile alichokiita wananchi ‘kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara’!

Rais aliyasema hayo wiki moja baada ya barua yetu kwa serikali yake juu ya nia ya CHADEMA kufanya maandamano ya amani iwapo serikali yake isingechukua hatua tulizodai zichukuliwe katika barua yetu ya tarehe 23 Desemba 2010. Haikupita hata wiki moja tangu Kikwete atoe kauli yake hiyo na Jeshi la Polisi la Tanzania limemwaga damu ya Watanzania Arusha. Jeshi la Polisi la Tanzania limetekeleza maagizo ya Amiri Jeshi wake mkuu, ndio maana Amiri Jeshi Mkuu huyo hajatoa kauli yoyote kwa Watanzania kuhusiana na matukio haya ya kusikitisha na wala kuchukua hatua kuwawajibisha wale waliotoa amri za kuua na kuumiza Watanzania na/au waliozitekeleza.

KISASI CHA UCHAGUZI MKUU!

Mauaji ya wananchi wetu, matumizi ya nguvu ya kutisha dhidi ya wanawake, watoto na wazee na kukamatwa kwa mamia ya viongozi, wanachama na wananchi wa kawaida wa Jiji la Arusha ilikuwa ni kulipa kisasi kwa viongozi wa CHADEMA wa ngazi zote na kwa wananchi wa Arusha kwa kudiriki kuisambaratisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania lilidiriki kumvamia na kumpiga Mbunge wetu wa Arusha Mjini hadi akapoteza fahamu wakati alipojaribu kulinda haki ya wananchi wa Arusha kuwa na Meya wa Jiji wanayemtaka na sio anayetakiwa na mafisadi wa nchi hii na chama chao.

Jeshi la Polisi la Tanzania limelipa kisasi kwa niaba ya CCM kwa sababu wananchi wa Arusha wamediriki kutumia haki zao za kisheria kupinga mipango ya mafisadi kuingiza Meya wa Jiji la Arusha atakayelinda maslahi ya mafisadi na chama chao. Wananchi wa Arusha wamelipiziwa kisasi na Jeshi la Polisi la Tanzania kwa sababu mafisadi wanajua wangeruhusu haki itendeke katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha CCM ingesambaratishwa kama ilivyosambaratishwa katika Uchaguzi Mkuu.

Mauaji ya Arusha sio kisasi cha CCM dhidi wananchi wa Arusha tu. Ni kisasi pia dhidi ya wananchi wa Tanzania na dhidi ya CHADEMA. Ni kisasi dhidi ya Watanzania wote kwa sababu, kwa mara kwanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urudishwe mwaka 1992, Uchaguzi Mkuu wa 2010 ulionyesha wazi kwamba CCM imeanza safari yake ya mwisho kuelekea kwenye jaa la taka taka la historia. Kwa mara ya kwanza, CCM ilipoteza miji mikubwa karibu yote ya Tanzania. Licha ya uchakachuaji wa kura, rushwa na uharamia wa kutisha, CCM imepoteza Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Mwanza, Jiji la Arusha, Jiji la Mbeya na miji mikubwa kama vile Moshi, Iringa na Musoma.

Lakini CCM na mafisadi hawakupoteza miji tu, wamepoteza pia majimbo ya vijijini. CCM imepoteza nusu ya Shinyanga, zaidi ya nusu ya Kigoma, sehemu kubwa za Manyara, Singida, Mbeya, Iringa na mikoa mingine ambayo kihistoria imekuwa inaonekana kama ngome za CCM. Na licha ya nguvu nyingi za dola na za fedha za ufisadi, Jakaya Kikwete amepunguza idadi ya kura zake kutoka kura zaidi ya milioni nane alizopata wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 hadi kura milioni tano za mwaka jana, ikiwa ni pungufu ya zaidi ya kura milioni tatu na anguko la asilimia 20!

Kuporomoka kwa CCM kumeenda sambamba na kukua na kuongezeka kwa nguvu ya CHADEMA. Licha ya uchakachuaji wa kura wa kutisha, matumizi ya vyombo vya dola na rushwa ya kutisha, nguvu na ushawishi wa CHADEMA imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ndio chama cha upinzani chenye Wabunge wengi kuliko vyama vingine vyote vya upinzani kwa pamoja. Ndio chama pekee cha upinzani kilichowahi kupata Wabunge kutoka kanda zote za Tanzania Bara na Visiwani. Ndio chama cha upinzani pekee kilichowahi kupata zaidi ya robo ya kura zote za Rais na Wabunge. Na ndio chama pekee chenye kubeba matumaini ya wananchi wa Tanzania kwamba Tanzania bila ufisadi wa CCM inawezekana. Ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania limelipizia kisasi cha CCM kwa wananchi wa Arusha na viongozi, wanachama na wapenzi wa CHADEMA.

HAKI LAZIMA ITENDEKE ARUSHA!

Damu iliyomwagwa Arusha inalilia haki. Roho za wote waliotolewa muhanga na Jeshi la Polisi la Tanzania zinahitaji haki ili ziweze kutulia na mizimu yao ipumzike. Wote walioumizwa na ujambazi wa Jeshi la Polisi la Tanzania wanalilia fidia ili waweze kuuguza maumivu yao ya kimwili, ya kiroho na ya mali zao zilizoharibiwa. Sheria za nchi yetu zilizokanyagwa chini kana kwamba hazipo zinahitaji kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine wa aina hii.

Kwa hiyo, sisi wote tuliokusanyika hapa leo, na wale wote wanaotusikiliza mahali popote nchini na hata nje ya nchi yetu, tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale ambao tunaomboleza vifo vyao hapa leo. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale wote walioumizwa kwa risasi na mabomu na virungu na mabuti ya Jeshi la Polisi la Tanzania. Tuna jukumu la kuhakikisha wale wote ambao waliharibiwa mali zao kwa sababu ya uhalifu huu wa Jeshi la Polisi la Tanzania wanafidiwa kwa kiasi chote cha hasara waliyoipata. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi la Tanzania halirudii tena ujambazi wa aina hii dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia yoyote kwa kuwawajibisha wale wote walioshiriki katika ujambazi huu kwa kutoa amri za kuua au kuumiza wananchi na/au kwa kuzitekeleza.

Ili tutimize majukumu yote haya, tunahitaji kuhakikisha kwamba mambo yafuatayo yanafanyika:

  1. Serikali hii iwajibike kwa wananchi kama ilivyotamkwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Waziri wa Mambo ya Nchi Shamsa Vuai Nahodha na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema wajiuzulu mara moja ili kuwawajibisha kama viongozi na wasimamizi wa juu kabisa wa Jeshi la Polisi la Tanzania. Aidha, kujiuzulu kwao kutapisha uchunguzi huru na wa kina wa matukio yote yaliyosababisha wananchi wetu kuuawa, mamia kujeruhiwa na mamia mengine kukamatwa bila sababu yoyote na kuwekwa rumande na baadaye kufunguliwa mashtaka ya uongo ya jinai;
  2. Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Andengenye na wale wote walioamuru au kutekeleza amri ya kuvunja maandamano na mkutano halali wafunguliwe mashtaka ya jinai kwa matumizi mabaya ya madaraka na kwa kusababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia;
  3. Fidia stahili ilipwe kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na/au jamaa wa wale wote waliouawa kutokana na vitendo vya Jeshi la Polisi la Tanzania na kwa wale wote walioumizwa kwa namna yoyote ile na/au kuharibiwa mali zao kutokana na vitendo hivyo;
  4. Mashtaka ya uongo ya jinai yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa ngazi zote wa CHADEMA, wanachama, wafuasi na wananchi wengine wote waliokumbwa na kumba kumba ya Jeshi la Polisi la Tanzania yafutwe bila masharti yoyote kwa sababu maandamano na mkutano wa hadhara uliozuiliwa yalikuwa halali kwa mujibu wa sheria husika za nchi yetu. Tunasisitiza katika jambo hili kwamba viongozi, wanachama na wafuasi wetu wote waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka haya hawatahudhuria mahakamani tena kuhusiana kesi iliyofunguliwa dhidi yao hata kama kwa kufanya hivyo kutafanya wakamatwe na kurudishwa tena gerezani;
  5. Kwa vile uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ndio chanzo cha mauaji ya wananchi na kwa kufahamu utaratibu haramu uliotumika kumpata Meya wa Jiji hilo, matokeo ya uchaguzi huo yafutiliwe mbali na uchaguzi mpya uitishwe haraka iwezekanavyo kwa kufuata sheria husika za nchi yetu;
  6. Haki ya vyama vya siasa na wananchi kufanya maandamano ya amani kama inavyotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iheshimiwe na kutiliwa nguvu zaidi kwa kufuta vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi nay a Vyama vya Siasa vinavyoruhusu Jeshi la Polisi la Tanzania kuzuia na/au kusitisha maandamano ya amani. Badala yake, sheria ziweke wazi wajibu wa Jeshi la Polisi la Tanzania kulinda maandamano ya amani na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na/au ya wananchi;
  7. Tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoundwa na majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania iundwe ili kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa matukio yote yaliyopelekea Inspekta Jenerali wa Polisi na/au Jeshi la Polisi la Tanzania kupiga marufuku maandamano ya amani na mkutano wa hadhara na baadaye Jeshi la Polisi la Tanzania kufanya vurugu zilizosababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia. Tunapenda kusisitiza kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa sababu historia ya tume nyingine ambazo zimeundwa kwa utaratibu wa Rais kuteua watu anaowataka inaonyesha kwamba zimefanya kazi zao za uchunguzi mafichoni bila kushirikisha wadau wengine na bila wananchi kufahamu kitu kinachoendelea. Matokeo ya tume nyingi za namna hiyo ni kwamba ripoti zake mara nyingi zimepuuzwa na/au kufichwa na watawala. Tume ya uchunguzi ya kimahakama hufanya kazi zake kwa uwazi na huruhusu wananchi kuhudhuria na/au kushiriki moja kwa moja katika kazi za tume kama mashahidi na/au kwa kuhoji mashahidi wengine wanaotoa taarifa kwenye tume hiyo;

Katika kuhakikisha kwamba madai yetu yanatekelezwa, CHADEMA inaelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wetu mikoani na Wilayani kuandaa maandamano ya amani nchi nzima ili kulaani mauaji ya wananchi wa Arusha na kudai utekelezaji wa madai haya. CHADEMA Makao Makuu itatuma maafisa wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo Wabunge na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kushiriki katika maandamano hayo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuyaongezea nguvu na hamasa.

MAUAJI YA ARUSHA NA UMUHIMU WA KATIBA MPYA

Mauaji ya wananchi wa Arusha yanadhihirisha wazi umuhimu wa kuwa na Katiba mpya kwa ajili ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu, Katiba viraka inayotumika sasa hivi haiheshimiwi hasa na watawala wenyewe kama tulivyoonyesha kuhusiana na uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara. Aidha, Katiba yetu na sheria nyingine kama vile Sheria ya Jeshi la Polisi na ya Vyama vya Siasa zimetoa mamlaka makubwa mno kwa watendaji kama vile mapolisi kuingilia na kuvuruga haki za wananchi. Mamlaka haya ya kisheria hayana udhibiti wowote wa maana ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania linajiona kama liko juu ya sheria na haliwajibiki kwa makosa yoyote yanayofanywa na Jeshi hilo dhidi ya wananchi.

Aidha, matukio yaliyopelekea Mauaji ya Arusha yanaonyesha kwamba mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi wa kuendesha chaguzi katika nchi yetu unahitaji mabadiliko makubwa. Matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini – kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine walikoshinda wagombea wa upinzani - yalitolewa baada ya shinikizo kubwa la nguvu ya umma na sio kwa sababu ya utashi na/au uadilifu wa wasimamizi wa uchaguzi. Na kilichotuleta hapa leo ni matokeo ya uchakachuaji wa uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na viongozi wengine wa Halmashauri hiyo.

Sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba tunapata Katiba mpya itakayohakikisha kwamba vyombo vya ulinzi wa wananchi vinakuwa chini ya udhibiti halisi wa wananchi na/au vyombo vyao vya uwakilishi. Sasa ni muda muafaka kuhakikisha kwamba tunapata Katiba mpya itakayohakikisha kwamba mfumo wetu wa uchaguzi ni huru na wa haki kwa watu na vyama vyote. Sasa ni muda muafaka kuhakikisha tunakuwa na Katiba mpya itakayohakikisha kwamba siku za huzuni kama ya leo zinabaki katika kumbu kumbu za kihistoria tu. Na kwenye suala hili la Katiba mpya tunaujulisha umma wa Watanzania kwamba hatukubaliani hata kidogo na utaratibu uliopendekezwa na Rais Kikwete wa kuunda Tume ya Kupitia Katiba. Utaratibu uliopendekezwa ni ule ule uliotufikisha hapa tulipo. Ni utaratibu wa kubadili Katiba wa watu wale wale unaoendeshwa na/au kusimamiwa na watu wale wale kwa manufaa ya watu wale wale.

Utaratibu ambao CHADEMA itauunga mkono na kushiriki kikamilifu ni ule utakaowezesha kufanyika kwa Mkutano wa Kitaifa wa Katiba ambao utawakilisha makundi yote ya kijamii katika uundaji wa Katiba mpya. Utaratibu wa kusubiri fadhila za Kikwete za kuteua wajumbe wa Tume ya Katiba haukubaliki tena na CHADEMA haitaubariki kwa kushiriki. Aidha, CHADEMA itatumia uwezo wake wote kuhamasisha wananchi nchi nzima ili kupinga utaratibu unaopendekezwa na Kikwete na kuunga mkono utaratibu wa kidemokrasia wa kupata Katiba mpya kwa kupitia Mkutano wa Kitaifa wa Katiba.

Mh. Freeman Mbowe (Mb)

Mwenyekiti Taifa

12 Januari, 2011

Tamko limetolewa wakati wa heshima za mwisho za marehemu katika Uwanja wa NMC Arusha

Kauli ya Mbunge Mnyika kuhusu Kikwete na Katiba Mpya

3 Januari 2011

Kauli ya Mbunge Mnyika kuhusu Kikwete na Katiba Mpya

Mara baada ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya tarehe 31 Disemba 2010 nikiwa safarini nimepokea simu na ujumbe wa simu pamoja na barua pepe toka kwa vyombo mbalimbali, baadhi ya viongozi wa kada anuai na wananchi kadhaa wakitaka kujua msimamo wangu kuhusu kauli ya Rais Kikwete kukubali hoja ya kuandikwa kwa katiba mpya na kutangaza kuunda Tume ya mchakato husika.

Aidha baadhi ya simu na barua hizo zimetaka kujua hatma ya hoja binafsi ambayo nilipanga kuiwasilisha kwenye Mkutano wa Bunge wa Mwezi Februari kuhusu mchakato husika; hoja ambayo nimeshawasilisha taarifa yake ya hoja kwa Katibu wa Bunge.

Katika simu hizo na barua pepe wako baadhi ya watu ambao wamekwenda mbele zaidi kwa kutoa maoni wengine wakitaka bado hoja binafsi iwasilishwe bungeni na wengine wakishauri kwamba sasa nguvu zielekezwe katika Tume iliyotangazwa kuundwa na Rais kuhusu mchakato husika.

Katika muktadha huo nimeona ni vyema nitoe kauli rasmi kuhusu suala husika ili msimamo na maoni yangu kuhusu suala husika ufahamike wa wananchi wa Ubungo na Watanzania wenzangu kwa ujumla kuhusu suala hili nyeti linalogusa mustakabali wa taifa letu.

Natambua tofauti aliyoionyesha Rais Kikwete kwenye jambo hili kwa kutambua haja ya katiba mpya kinyume na kauli za watendaji wake ndani ya serikali za hivi karibuni ( Waziri Kombani, Waziri Mkuu Pinda na baadaye Mwanasheria Mkuu Werema) ambao wote walitaka marekebisho ya katiba kwa kuwekwa viraka mbalimbali.

Aidha natambua kuwa kauli ya Rais Kikwete kukubali kuandikwa kwa katiba mpya inaashiria mabadiliko ya kimtazamo kwa upande wake pia ukilinganisha na kauli zake mbalimbali katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 mpaka mwaka 2010 kuhusu suala la mabadiliko ya mfumo wa utawala katika taifa hali inayoashiria kwamba ametambua kuwa hitaji la katiba mpya ni la watanzania waliowengi ambalo limetolewa kauli na wadau mbalimbali.

Pamoja na kukubali kuandikwa kwa katiba mpya bado watanzania wanahitaji kujadili kwa kina na kwa haraka kuhusu mchakato uliopendekezwa ili taifa liende katika mkondo sahihi wa kuanza kutoa maoni.

Ni muhimu kwa wadau wote kutaka kufahamu muundo wa Tume pamoja na hadidu rejea kwa kina ili kuepuka taifa kuanza mchakato kwa njia isiyo kamili; kinyume na hapo watanzania tunaweza ‘kuuziwa mbuzi kwenye gunia’.

Suala hili ni la msingi kwa kuwa Historia ya Taifa letu inaonyesha kwamba Tume zilizoundwa na Marais na kushughulika na masuala yanayogusa Katiba hazikuweza kukidhi matakwa ya wananchi kwa sababu mbalimbali.

Mathalani, taifa linajadili sasa kuhusu mabadiliko ya katiba kutokana na kasoro katika hatua za awali za kuandikwa kwa Katiba ya Kudumu ya Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndiyo tunayoitumia hivi sasa pamoja na marekebisho yake.

Mchakato uliotumiwa na Rais wa wakati huo, Hayati Julius Nyerere ndio ambao unajitokeza sasa kwenye Hotuba ya Rais Kikwete kwa kueleza kwamba Rais anaunda tume na baadaye mapendekezo ya tume yanakwenda moja kwa moja kwenye vyombo vya kikatiba bila kwanza kuwa na .

Matokeo ya utaratibu huu ni wananchi kutoshirikishwa kwa ukamilifu wake katika maamuzi yanayohusu katiba. Tume ya Rais ya wakati huo iliyokuwa chini ya Thabiti Kombo ilifanya kazi ya kukusanya kwa muda mfupi, matokeo yake yakaenda kujadiliwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama tawala wa siku moja, na hatimaye yakapelekwa bungeni na kupitishwa baada ya majadiliano ya muda mfupi sana (kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwa saa tatu tu).

Matokeo ya mfumo huo ni kuandikwa kwa katiba isiyokubalika na umma kwa uwingi wake na kusababisha mpaka sasa marekebisho (viraka) mara kumi na nne na bado kuna mapungufu mengi kwa kiwango cha sasa kukubaliana kuandika katiba mpya.

Natambua kwamba Rais Kikwete amesema kwamba Tume itakwenda kukusanya maoni kwa umma, lakini jambo la muhimu sio kupatikana kwa maoni tu, suala la msingi na maamuzi kuhusu ni maoni ambayo ndiyo yanatumika kama msingi wa katiba mpya na makubaliano ya pamoja kuhusu misingi muhimu ya katiba mpya.

Katika mazingira hayo, ndipo panapojitokeza umuhimu wa kuwa na Mkutano Mkuu wa Taifa Katiba kabla ya mapendekezo ya katiba kupelekwa kwenye mamlaka za kikatiba ambazo kwa mujibu wa katiba ya sasa ibara ya 98 ni Bunge pekee. Kauli ya Rais Kikwete inaashiria kwamba wananchi hawatahusishwa moja kwa moja kwenye kuamua katiba badala yake tume itachukua maoni yake na baadaye maamuzi yatafanywa na bunge kwa niaba yao kama ilivyo kwenye marekebisho ya kawaida ya katiba kwa mujibu wa ibara ya 98 ya katiba.

Izingatiwe kuwa kwa sasa Tanzania haifanyi marekebisho ya Katiba bali tunakwenda kufanya mapitio (review) na hatimaye kuwa na katiba mpya; hivyo suala la ushirikishwaji wa umma sio katika kutoa maoni tu bali kuamua misingi muhimu ya katiba ni suala lenye umuhimu wa pekee ili tuwe na katiba inayokubalika na umma mpana isije yakajirudia tena yaliyojitokeza kwenye kuandikwa kwa katiba ya mwaka 1977.

Kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye Katiba hii tunayotumia sasa kwenye ibara ya 98 ambapo haijaweka bayana mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya bali mabadiliko ya katiba, ni muhimu kutumia mamlaka ya ibara hiyo ya katiba kifungu cha pili kuwezesha Bunge kutunga sheria itayosimamia na kuwezesha mchakato wa mapitio (review) ya katiba ili kupata katiba mpya.

Sheria hiyo itawezesha kuwekwa utaratibu wa Kongamano/Mkutano wa Taifa, Tume ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na hata kutafakari uwezekano wa kufanya kura ya maoni (referendum) katika masuala nyeti kama Muungano.

Kutokana na kujitokeza bayana kwa mahitaji ya kisheria kuhusu mchakato inaonekana bayana kwamba bado iko haja ya suala hili la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Katika mazingira hayo nasubiri kwanza ufafanuzi wa serikali kuhusu mchakato husika ikiwemo kujua kwa kina muundo wa tume, hadidu rejea na kama serikali itapeleka bungeni mapendekezo kuhusu mchakato kabla ya kutoa kauli kuhusu hatma ya hoja binafsi ambayo nilitoa taarifa kuwa nitaiwasilisha bungeni katika mkutano wa mwezi Februari.

Na katika kipindi ambacho nasubiria ufafanuzi wa serikali ambao inapaswa kuuweka hadharani nitaendelea na hatua ambazo nilizitangaza nilipokwenda kuwasilisha taarifa ya hoja tarehe 27 Disemba 2010.

Hata hivyo, kutokana na kauli ya Rais Kikwete na hatua za ziada ambazo natarajia kutoka kwa serikali nitatumia wiki ya kwanza ya mwezi Januari kukutana ana kwa ana na baadhi ya viongozi wa asasi za kiraia, taasisi za dini na vyama vya siasa ikiwemo CHADEMA kuweza kushauriana hatua za ziada za kuchukua.

Kimsingi, kama nilivyoeleza awali, hoja hiyo pamoja na kuwa inaitwa hoja binafsi kwa kanuni za bunge ni mimi ni mwakilishi lakini hoja ya umma kutokana na kuwa katiba mpya ni hitaji la wananchi hivyo maamuzi kuhusu hatma ya hoja husika yatafanywa kwa kushauriana na wananchi na wadau wengine baada ya kupata ufafanuzi wa serikali.

Aidha kabla ya wananchi kuanza kutoa maoni kuhusu maudhui (nini kiwemo ndani ya katiba mpya) natoa mwito kwa wadau wote kujadili kwa kina mchakato (taratibu gani zifuatwe) wa katiba mpya; kwa kuwa mchakato usipokuwa sahihi hata maoni mazuri yakitolewa yanaweza yasifikie hatua ya kufanyiwa kazi kwa ukamilifu na hatimaye tukakosa tija ambayo tunaikusudia kwa kuandikwa kwa katiba mpya miaka 50 baada ya uhuru.

Tukumbuke kwamba mwaka 1991 Rais wakati huo Ali Hassan Mwinyi aliunda tume ya kuhusu mfumo wa vyama Tanzania (maarufu kama Tume ya Nyalali) na kwamba tume hiyo ilikuja na mapendekezo mengi ikiwemo la kutaka kuandikwa kwa katiba mpya, lakini serikali ilichukua machache ikiwemo la kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Mchakato tunaotaka kuuanza sasa ungeshakamilika miaka mingi kama mapendekezo ya wakati ule yangetekelezwa kwa ukamilifu wake.

Kadhalika tukumbuke kwamba mwaka 1998 Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa aliunda Tume ya marekebisho ya Katiba (Maarufu kama Tume ya Kisanga aliyoratibu maoni kwa kutumia White Paper), hata hivyo sehemu kubwa ya mapendekezo ya Tume hayakutekelezwa. Na Rais wa wakati huo aliikataa hadharani sehemu kubwa ya taarifa yao na kutangaza kuwa tume imefanya kazi kinyume na hadidu rejea. Wakati huo tume ilielezwa kuwa ilikwenda kinyume na maoni ya wananchi lakini kimsingi ni kwamba mapendekezo ya tume yalikwenda tofauti na misimamo ya serikali ambayo ilianishwa bayana kwenye White Paper. Suala hili lilijitokeza kwa kuwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 37 Rais katika kufanya kazi zake halazimiki kufuata ushauri wa mtu yoyote; hivyo suala la kuwa na mfumo ambao mapendekezo yake yatakubalika na kuheshimika ni la muhimu sana kabla ya kuanza kutoa maoni ya kuingizwa kwenye katiba mpya.

Ndio, maana ni muhimu kwa mchakato wa sasa kufanyika kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na kuwekewa utaratibu bayana ikiwemo kuitaka tume yoyote itayoundwa kutumia mfumo wa Green Paper ili wananchi wenyewe kuanza kutoa maoni yao kuhusu masuala wanayoyaona kipaumbele badala ya kuathiriwa kimsimamo na serikali au tume yenyewe.

Natambua kwamba Rais Kikwete amedokeza kuwa Tume anayotaka kuiunda itahusisha wadau hata hivyo ni muhimu tume ikaundwa katika mfumo ambao ni shirikishi, sio tu wajumbe kuteuliwa kutoka sekta au kada Fulani bali pia kuwe na mashauriano (consultation) kati ya kada au sekta husika kabla ya uteuzi ili kuwe na uwakilishi badala ya wahusika kujiwakilisha wenyewe au kumwakilisha aliyewateua. Ndio maana katika mazingira hayo, tume inayoundwa kwa sheria ya bunge ingekuwa na uzito zaidi na kazi yake kupata kuungwa mkono. Jambo hili ni muhimu kwa kurejea yaliyojiri katika mchakato wa kuundwa kwa Kamati ya Rais ya kupitia upya mikataba ya madini (maarufu kama Kamati ya Bomani); hali hiyo haipaswi kujitokeza sasa katika mchakato wa kuunda Tume ambayo inashughulika na suala tata na tete la katiba mpya ambalo kukubalika kwa mchakato na chombo kinachoratibu ni hatua ya msingi sana katika kuwa na katiba inayokubalika na umma.

Pamoja na njia ya kibunge ambayo niliidokeza wakati naeleza kusudio la hoja binafsi, Rais Kikwete na serikali yake kwa dhamira ya kuhusisha umma katika kuandika katiba mpya kuanzia katika hatua za awali ingeweza kuitisha Kongamano la Kitaifa (National Congress) kujadili tunu za taifa kitaifa, misingi ya kikatiba, muundo/majukumu ya tume ya katiba, kutoa mwongozo wa bunge la katiba na namna ya kufanya kura ya maoni (referendum). Hivyo, kama serikali haitatoa maelezo yanayokidhi haja na hoja bado Bunge litawajibika kutimiza wajibu wake wa kikatiba kwa niaba ya wananchi kwa kurejea ibara ya 63(2) na (3) ili kuweka mchakato muafaka zaidi wa katiba mpya kama sehemu ya kuisimamia na kuishauri serikali inayoongozwa na Rais Kikwete katika hatua hii muhimu ya kuandika katiba mpya- ambayo ni sheria mama na mkataba kati ya wananchi na serikali.


John Mnyika

Mbunge wa Ubungo