Showing posts with label Shairi. Show all posts
Showing posts with label Shairi. Show all posts

Tuesday, October 12, 2010

Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Tumempata mwanana, mpambanaji hodari
Mzalendo pia mwana , mafisadi kukabiri
Utani kwake hakuna, kweli yeye dakitari
Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Tumpe kura kwa wingi, uchumi kuukomboa
Tumpeni nyingi kingi, nchi kuisimamia,
Avuke vyote vigingi, mtandao kuubomoa
Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Siku ile ikifika , kura tumpe Slaa
Yeye ndiye msifika , mafisadi kwao balaa
Wezi watetemeka, walisikiapo ‘Slaa’
Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Anahaha makamba , kama anakata kamba
Mafuriko yamkumba, anenayo yote pumba
Chama chake kinayumba, sasa kutumia ndumba
Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Pipozi pawa ni sasa, kona zote yasikika
Ukombozi ndiyo sasa, ccm kuizika
Nchi yetu kutakasa, wakati ndo umefika
Siku ile ikifika, Kura zetu kwa Slaa

Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki amesema, kwa hakika hazitaki,
Mbona mna muandama, kwa kisa kile na hiki,
Kikwete mtu mzima, na wala msihamaki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Pendo kitu cha hiari, hakina lazima katu,
Ni vema kujihadhari, msizidi kuthubutu,
Si kwa kero nazo shari, mumwache mwana wa watu,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mapenzi kweli maua, huweza ota popote,
Bali huhitaji nia, kuyahudumia yote,
Bila maji kumwagia, Hunyauka kwa vyovyote,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Wafanyakazi hataki, mwataka nini zaidi?
Msitumie mikiki, hali mu watu weledi,
Binadamu ana haki, kupima na kukaidi,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mbona hamna simile, huria kumuachia,
Mmeng'ang'ana na lile, hamtaki kusikia,
M-bembeleze milele, hataki kawaambia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Mmejawa na hiana, kwa jibu alilotoa,
Kawaeleza bayana, wazi amewaambia,
Mwalitafuta laana, msilolitarajia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Kwa uvumba na ubani, kesha sema hazitaki,
Zaidi mwataka nini, awaeleze rafiki?
Tulia mkae chini, muwaze na kuhakiki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki kakataa, kura zenu kasusia,
Japo mlete gitaa, na nyimbo kumuimbia,
Mumtembeze mitaa, kwa manoti mia mia,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Hazitaki si ajabu, kura zisizo na soko,
Msiitafute tabu, kujipendekeza mwiko,
Bure mwajipa aibu, kwa kumpa mialiko,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.


Kaditamati shairi, kura zenu hazitaki,
Kila kitu ni hiari, shuruti haina haki,
Kuchagua ni fahari, lazima haipendeki,
Wazi amewaambia, kura zenu hazitaki.

Thursday, October 7, 2010

Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Nimelala nimekesha, jambo nimefikira
Bongo nimezichemsha, sipati jibu sawia
Hivi kweli Umekwisha Uzalendo Tanzania?
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Ona walivyoziuza, rasilimali za mtanzania
Kwa kweli inashangaza, mikataba waloingia
Kisha tukiwauliza, hawana la kutwambia
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Rushwa imekuwa ngao, kumdhulumu raia
Ubinafsi kwao nguo, vazi la kujivunia
Hizi ndizo sera zao, katu hawajui njia
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Wananchi amkeni, haki kujitafutia
Mtalala mpaka lini?, saa imeishawadia
Uwongo ukataeni Waache kuwatania
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Mkipiga kura zenu, chagueni mwenye nia
Waonesheni wanenu, muelekeo na njia
Fanyeni vitu vyenu, tuiokoe Tanzania.
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania

Mchagueni Slaa, kiboko cha Mafisadi
Huyu bwana hana njaa, atatwanga wakaidi
Ni kiongozi shujaa, si mtumwa wa itikadi
Mchagueni Slaa, tuiponye Tanzania