HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUDHAMINIWA FOMU YA KUGOMBEA URAIS KWA TIKETI YA CCM, OFISI YA CCM DODOMA
TAREHE 21 JUNI, 2010
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Muda mchache uliopita nimechukua fomu ya kuomba kuteuliwa tena na Chama chetu kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mambo matatu yamenipa moyo wa kufanya uamuzi huu. Kwanza, ushawishi wa Watanzania wenzangu wengi: wana-CCM na wasiokuwa wana-CCM, wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee wa Mikoa yetu na Wilaya zetu zote kwa kunitaka nigombee tena. Pili, nimeridhika kwamba katika miaka mitano hii, pamoja na kukabiliana na changamoto nyingi, Serikali chini ya uongozi wangu imefanya kazi nzuri ya kusukuma maendeleo ya taifa letu na kuimarisha umoja, amani na utulivu katika nchi yetu. Na tatu, Katiba inaniruhusu, kwani naweza kuwa Rais kwa vipindi viwili mfululizo. Nimemaliza kimoja, hivyo naweza kuomba kupata kipind kingine cha pili.
Nawashukuru sana wana-CCM wenzangu hususan wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa imani kubwa waliyonipa mwaka 2005 ya kubeba bendera ya Chama chetu katika uchaguzi wa mwaka ule. Nimejitokeza tena safari hii kuwaomba mnipe ridhaa nyingine. Nilitembea nchi nzima kunadi Ilani ya uchaguzi na Sera za Chama cha Mapinduzi na kwa ushirikiano na wagombea wenzangu wa nafasi za Ubunge na Udiwani tukiongozwa pamoja na viongozi wa Chama wa ngazi zote tangu Taifa hadi Shina na kuungwa mkono na wana-CCM wenzetu na wananchi tulipata ushindi mkubwa. Naahidi kuwa mkiniteua tena safari hii nitafanya hivyo hivyo na naamini kwa dhati kabisa na hasa kama wana-CCM tutaendelea kushikamana na kukipigania Chama chetu kama tulivyofanya mwaka 2005 tutapata ushindi mkubwa kama ule au hata kuzidi ule.
Niliahidi, wakati ule kwamba katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi mliyonikabidhi kuinadi kwa Watanzania, tutatengeneza mipango na programu mbalimbali za utekelezaji wa shabaha na malengo ya Ilani hiyo. Wana-CCM wenzangu wote na Watanzania wote ni mashahidi kwa kiasi gani nilikuwa muaminifu kwa ahadi hiyo. Tumeitekeleza Ilani kwa umakini mkubwa na matokeo yake yanaonekana pembe zote. Takriban mambo yote tuliyoahidi tumetekeleza na pale ambapo yapo ambayo hatujatekeleza, ambayo kwa kweli si mengi, ni kwa sababu za msingi. Hata hivyo, yale ambayo hatukujaaliwa kuyatekeleza safari hii tutayakamilisha tukipewa heshima ya kuliongoza taifa letu katika awamu ijayo.
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Baada ya kuchaguliwa niliahidi kuwa nitatumia vipaji vyangu vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuitumikia nchi yangu na watu wake. Ninyi ni mashahidi kwa kiasi gani nimefanya kazi kwa kujituma usiku na mchana, ndani na nje ya nchi yetu kwa ajili hiyo.
Katika miaka mitano hii, hakuna Wilaya au Jimbo la Uchaguzi katika nchi yetu ambalo sikufika. Nimetembea vijiji, vitongoji na maeneo mengi sana kuona mengi. Nimekutana na kuzungumza na wananchi na kujua raha zao, mafanikio yao na karaha zao. Yapo masuala mengi yanayowatatiza wananchi ambayo yameweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia hiyo. Nimeiacha wazi simu yangu kwa wananchi kuwasiliana nami na nimeambiwa mengi ya ushauri na yanayotaka kuchukuliwa hatua. Nimesikiliza na kuchukua hatua muafaka. Hata waliokuwa na shida binafsi niliwasikiliza na kuwasaidia kwa kile nilichoweza. Katika kipindi cha miaka mitano hii tumeshuhudia demokrasia nchini ikizidi kustawi na taasisi za kidemodrasia na utoaji wa haki kama vile Bunge, Mahakama na vyombo vya habari vikiimarika. Watu wamekuwa huru zaidi kutoa maoni yao na uhuru wa kuabudu umeendelea kuheshimiwa. Vyombo vya ulinzi na usalama vimeendelea kuimarishwa na mapambano dhidi ya uhalifu na maovu mengine katika jamii ikiwemo rushwa yaliendelea kwa uthabiti zaidi.
Na kwa kweli tumepata mafanikio makubwa katika kutimiza yale tuliyowaahidi Watanzania. Kote ninakotembea katika nchi yetu, napata faraja kuwasikia wananchi wenzangu wengi wakiyazungumzia, wakiyafurahia na wakinufaika na mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hiki cha uongozi wangu. Hata mimi mwenyewe ninapotazama na kuona tuliyoweza kufanya katika kipindi hiki nashangaa. Hakika pamoja na juhudi zetu kuna baraka za Mwenyezi Mungu. Naamini Mungu asipotuacha mkono kipindi kijacho tutafanya makubwa zaidi.
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Upo msemo kwamba kama unavuka mto ukiwa umepanda farasi sio busara kushuka na kubadili farasi katikati ya mto, hasa kama farasi huyo amehimili mawimbi.
Katika miaka mitano iliyopita, tumehimili mawimbi makubwa yaliyotishia umoja wa nchi yetu. Tanzania yetu leo hii bado ni ile ile nchi yenye amani na utulivu tunayoijua sote na ambayo dunia inaijua hivyo. Tumejifunza mengi, na tumepikwa katika tanuru la moto na tumeiva kama chuma cha pua. Na tumefaulu mtihani na changamoto za uongozi wa Taifa letu. Na tumedhihirisha kwamba tunao uwezo wa kuivusha nchi yetu kuelekea kwenye neema.
Leo hii kuna shule nyingi zaidi za msingi na sekondari na vijana wengi zaidi wanaingia shule za msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu kuliko 2005 na kuna walimu wengi zaidi. Huduma ya afya ni bora zaidi na zipo hospitali, vituo vya afya na zahanati nyingi zaidi na upatikanaji wa dawa umeboreka zaidi. Afya za Watanzania zinaimarika na watu wachache zaidi wanakufa kwa malaria, Ukimwi, TB na maradhi mengine ambayo huko nyuma yalikuwa yanauwa watu wengi. Barabara nyingi zaidi vijijini na mijini zimejengwa na kuimarishwa na kufanya maeneo mengi zaidi kufikika na kupitika mwaka mzima. Barabara za lami na changarawe zimeongezeka na madaraja mengi zaidi yametengenezwa. Kuna visima vingi, mabwawa mengi yaliyochimbwa na miradi mingi ya maji ya bomba imejengwa na kuimarishwa. Idadi ya watu wanaopata maji safi na salama imeongezeka zaidi mijini na vijijini kuliko mwaka 2005. Umeme umeendelea kusambazwa na kufika kwenye wilaya nyingi zaidi nchini kuliko mwaka 2005.
Mfuko wa ruzuku ya mbolea na pembejeo nyingine kwa wakulima na wafugaji umeongezewa sana pesa. Matokeo yake wakulima wengi wameongeza matumizi ya mbolea, mbegu bora, madawa ya kuulia wadudu na wafugaji wanapata dawa za kinga na tiba ya mifugo yao. Mfumo wa ununuzi wa mazao ya wakulima umeboreshwa na kufanya wakulima wa mazao yetu makuu kupata masoko ya uhakika na bei nzuri.
Uchumi wa taifa, pato la taifa na pato la Mtanzania limeendelea kuongezeka na kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2005 na idadi ya Watanzania wanaoishi katika umaskini uliokithiri imepungua, ingawa sio kwa kasi tuliyotarajia. Bajeti ya Serikali nayo imeongezeka sana kutoka shilingi trilioni 4.8 mwaka 2005/2006 hadi shilingi trilioni 11.1 mwaka 2010/2011. Tumezidi kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje katika bajeti yetu. Mafanikio ni mengi sana, na itakapofika wakati wa kampeni tutayaeleza yote kwa kina.
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Naomba niwashukuru wanachama wa CCM wote walionishawishi kuchukua fomu pamoja na ninyi mliofika hapa kunidhamini. Nimefarijika sana kuona kwamba ninyi, pamoja na wana-CCM wenzangu wengine wengi nchini, mmeniamini kwamba ninafaa kuendelea kuliongoza Taifa letu kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Hayo yote ndiyo yaliyonishawishi nami kushawishika kujitokeza kuomba tena kupewa nafasi ya kuliongoza taifa letu. Safari ile nilisema mkinichagua nitafanya kazi kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na kasi Mpya na matokeo yake tumeyaona. Safari hii nasema mkinichagua nitawatumikiwa Watanzania kwa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi katika dhamira yetu ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Kwa pamoja tuzidi kusonga mbele.
Ndugu Wana-CCM,
Napenda kuwashukuru wanachama wote wa CCM walionichangia fedha za kuchukua fomu hii. Nawashukuru sana. Wamejinyima ili kunichangia. Nauthamini sana mchango wenu.
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kuwaahidi kwamba, mkinipa nafasi ya kuwa mgombea wa Chama chetu, sitawaangusha. Nitatumia bidii yangu yote kufanya kampeni ya kukipigania Chama chetu kipate ushindi mkubwa.
Na, mara tutakapofanikiwa, vipaumbele vya Serikali ijayo vitasukumwa na misingi kumi na moja ifuatayo:
1. Kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa na umoja, amani na usalama, na Muungano wetu unaendelea kuimarika.
2. Kujenga misingi ya uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea kwa kuchukua hatua madhubuti za kuharakisha zaidi mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda. Nataka tuanze safari ya kuelekea kuwa taifa la uchumi wa kati, ambalo viwanda ndio mhimili mkuu.
3. Kuongeza jitihada na mipango zaidi ya kuwawezesha kiuchumi wananchi hasa wa hali ya chini, ili waweze kushiriki na kunufaika na uchumi wetu unaokua. Lakini vilevile tutaweka mkazo katika kulitambua na kuliwezesha kwa namna yake kundi la wajasiriamali wa tabaka la kati ili waweze kushiriki katika uwekezaji mkubwa katika nchi yetu.
4. Kutumia fursa ya kijiografia ya nchi ya nchi yetu kwa kuifanya lango kuu la biashara na usafirishaji kwa nchi za Afrika ya Mashariki, Kusini na Kati, hasa kwa kuimarisha ufanisi wa reli na bandari zetu.
5. Kuongeza jitihada za kuhakikisha Taifa letu linanufaika zaidi na rasilimali za asili za nchi yetu, kuanzia madini, misitu, wanyamapori hadi vivutio mbalimbali vya utalii.
6. Kuweka mkazo sasa kwenye kuboresha elimu ya msingi na sekondari, na kupanua elimu ya ufundi na elimu ya juu, hasa katika masomo ya sayansi.
7. Kuongeza jitihada za kupanua na kuboresha huduma muhimu za kijamii hasa huduma za afya na maji, na huduma za kiuchumi hasa umeme, miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano na huduma ya fedha.
8. Kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria, na demokrasia nchini, hasa kwa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, na ubadhirifu wa mali ya umma; na kuendelea kuviwezesha kirasilimali, kitaasisi/kimuundo na kisheria vyombo vya kutoa na kusimamia haki nchini;
9. Kuipa dola na vyombo vyake husika uwezo mkubwa zaidi wa kupanga mipango ya uchumi na kusimamia uchumi wa nchi kwa ufanisi, bila kuingilia sekta binafsi, ili kulinda maslahi ya nchi yetu na watu wake.
10. Kulinda mafanikio tuliyoyapata katika nyanja zote tangu uhuru wa nchi yetu, ikiwemo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kukamilisha yale tuliyoyaahidi mwaka 2005 ambayo, kwa sababu moja au nyingine, hatukuweza kuyakamilisha katika miaka hii mitano.
11. Kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi yetu na majirani zetu, na mataifa mengine duniani, pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa, na kuendelea kutafuta marafiki wapya kwa manufaa ya nchi yetu.
Ndugu Wana-CCM wenzangu,
Haya ni mambo ya msingi kwa maendeleo ya Taifa letu. Nitahakikisha kwamba Ilani ya Uchaguzi tutakayoitengeza na mipango ya Serikali baada ya hapo inayabeba yote haya.
Naomba nimalize tena kwa kuwashukuru kwa mara nyingine kwa kujitokeza kushuhudia tukio hili. Nawashukuru kwa imani mliyoionyesha kwangu. Ninayo nguvu, ari na dhamira ya kuitumikia nchi yangu. Na niko tayari kuendelea kuwa mtumishi wenu. Pamoja, Tuzidi Kusonga Mbele!
Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Dira Ya Dunia
1 hour ago
0 comments:
Post a Comment