MBUNGE wa Karatu Dk Willibrod Slaa, ameichanachana bajeti ya Waziri Mkuu akisema kuwa kusema si lolote katika kuwasaidia Watanzania.
Akizungumza muda mfupi baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuomba bunge limuidhinishie zaidi ya Sh2.9 trilioni kwa matumizi ya mwaka 2010/11, Dk Slaa alisema bajeti hiyo, imejaa ghiliba nyingi.
Dk Slaa jana alikuja na staili mpya katika uchangiaji, pale alipoanza kwa kusema ameamua kuichana bajeti hiyo ambayo ni ya tano kuombwa na serikali ya awamu ya nne kwa kuwa katika kipindi chote hicho, serikali hiyo haijafanya kitu zaidi ya kuwarudisha nyuma watanzania.
Katika hotuba yake, Dk Slaa alionyesha kuchukizwa na kitendo cha kupunguza misamaha ya kodi ya madini huku ikiongeza ushuru kwa wapanda pikipiki.
“Serikali isiyoweka vipaumbele kwa wananchi ni dhahiri kuwa itakuwa haiwatendei haki na haiwajali kabisa. Mfano mzuri ni hii misamaha ya kodi ya kampuni kubwa za madini.
"Wakati inawatoza wananchi wake, waendesha pikipiki (Bodaboda) ambao wanafanya biashara tu ya kujitafutia chakula huku kukitolewa misamaha mikubwa ya zaidi ya Sh700 bilioni,” alisema Slaa.
Dk Slaa alieleza kuwa hata kitendo cha serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupunguza kodi kwa wafanyakazi wake kwa asilimia moja ni cha aibu, kisichopaswa kuigwa na serikali nyingine yoyote duniani.
“Mheshimiwa Spika hoja ya kwamba serikali haiwezi kuongeza mishahara sio ya kweli kwani kama serikali ingelipanga vizuri vipaumbele vyake, mishahara ingeweza kuongezwa bila shida.”
Kwa mujibu wa Dk Slaa, mzigo mkubwa wa kodi unabebwa na idadi ndogo sana ya Watanzania ambao aliosema kuwa ni wa siku nyingi na kuigwa kila mwaka.
Awali katika hotuba yake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema serikali imetenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini nchini ili wafanye shughuli zao kwa uhakika na usalama zaidi.
Aidha Pinda alisema kuwa serikali imetenga Sh1 bilioni kwa ajili ya kianzio cha mfuko wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuanzisha kitengo maalumu cha kuwaendeleza wachimbaji hao.
Kuhusu suala la kukabiliana na upungufu wa walimu, Waziri Mkuu Pinda alisema serikali imeandaa utaratibu wa kuajili walimu 14,800 wa shule za msingi na walimu 11,140 wa shule za sekondari katika mwaka huu wa fedha.
Waziri Mkuu aliomba bunge liidhinishe Sh2,973,221,260,000. Kati ya fedha hizo, Sh 2,107,701,783,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 865,519,477,000 kugharamia miradi ya maendeleo.
Akizungumza jana kuhusu makadirio na matumizi ya fedha ya Ofisi hiyo, Dk Slaa alisema tangu ofisi hiyo ilipoanzishwa imekuwa ikitoa taarifa kuhusu matumizi mabaya ya fedha, lakini hazifanyiwi kazi.
"Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kama rasilimali za Taifa hili zingesimamiwa na kudhibitiwa inavyotakiwa leo hali yetu ya uchumi isingekuwa tofauti na Malaysia au Singapore ambapo wakati wa uhuru walikuwa na hali ya uchumi kama ya kwetu, Watanzania lazima wajiulize kuna nini, rasilimali nyingi sana, ardhi kubwa sana, maji mengi sana, lakini watanzania Maskini wa kutupwa. Serikali lazima itupe jibu," alisema Dk Slaa na kuongeza,
"Tulitegemea kuwa Serikali, kwa maana ya Hazina, Tamisemi, na Wakurugenzi husika wangechukua hatua mara moja kuhusu maeneo yaliyobainishwa kuwa na Ubadhirifu, hali imekuwa kimya, Kamati za Bunge zimezunguka takriban mikoa yote gharama lakini matokeo yamekuwa kama hakuna lililotokea"
Alisema Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) imefika kwenye maeneo na kukuta hakuna nyumba ya mwalimu iliyojengwa lakini vitabu vya halmashauri vinaonyesha mradi umekamilika asilimia 100.
"Miradi hiyo ambayo matumizi yake au hayakuridhisha kabisa, au miradi haipo lakini fedha imetumika ni pamoja na miradi ya Shule ya Msingi Mlongo Kisiwani Mafia, Stendi ya Basi Manispaa ya Songea, stendi ambayo haipo kabisa lakini fedha zimetumika, Zahanati ya Ndagoni ambapo ujenzi umesimama na fedha kuliwa" alisema Dk Slaa
Alifafanua kuwa mradi mwingine ni wa ujenzi wa Nangaramo (Nanyumbu) ambapo mradi umejengwa, lakini hautumiki pamoja na mradi mkubwa wa maji wa Newala uliogharimu Sh172 milioni, lakini hauwezi kutumika kwa miaka mingi ijayo kutokana na ukosefu wa umeme.
Aliongeza kuwa halmashauri nchini hazijajibu hoja mbalimbali za ukaguzi, zenye thamani ya Sh91,101, 051, 978.40, wakati Kamati ya LAAC ilikwisha kutoa taarifa Bungeni kuwa japo ni kweli fedha hizo si lazima ziwe zimeibiwa, lakini kinachotokea ni kuwa Wakiisha kupita wakaguzi, wahusika wanaenda kununua risiti bandia mitaani, na kuwaita tena wakaguzi kufanya ukaguzi upya.
Mwananchi News Paper
Dira Ya Dunia
1 hour ago
0 comments:
Post a Comment