Saturday, 11 September 2010 20:59
0diggsdigg
Salim Said, Mwanza
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete na kumtaka awaombe radhi watanzania kwa kumtangaza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Lawrence Masha kuwa mgombea pekee wa ubunge jimbo la Nyamagana kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutoa uamuzi wa pingamizi alilowekewa.
Dk Slaa alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kiwanja cha Milongo, kunadi sera za chama hicho na kuwaombea kura wabunge wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, kauli ya Kikwete kwamba Masha amepita bila kupingwa kuwa Mbunge wa Nyamagana, imewapotosha Watanzania na kuwakatisha tamaa ya kumchagua kipenzi wao, mgombea wa Chadema.
"Tunamwomba Kikwete awaombe radhi watanzania kwa kuwakatisha tamaa ya kumchagua kipenzi chao Wenje baada ya kumtangaza Masha kwamba ni mgombea asiye na mpinzani," alisema Dk Slaa.
Alisema kauli hiyo ya mgombea wa CCM sio tu imewakatisha tamaa Watanzania, bali pia inaonyesha kuwa mgombea huyo haheshimu mamlaka zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa alidai kuwa Kikwete hana sera mpya zaidi ya kutumia sera za Chadema kujinadi.
Dk Slaa alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla haanza maandalizi ya kikao cha ndani cha chama hicho kilichotarajiwa kuanza jana usiku kutathmini ufanisi wa kampeni zake na mambo mengine kitakachohudhuriwa na viongozi wote wa juu wa chama akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Alisema Chadema ilikuwa ya kwanza kulitambua tatizo la kiwanda cha sukari Mtibwa mkoani Morogoro na kuwaambia Watanzania kuwa ingemaliza tatizo hilo ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani.
"Baada ya kutusikia, Kikwete akaenda kutoa siku tatu kumaliza tatizo hilo. Kumbe inawezekana kwa serikali kumaliza matatizo ya Watanzania lakini mpaka Dk Slaa atoe maagizo ndiyo itekeleze,” alisema Dk Slaa.
Alidai zaidi: “Dk Slaa alitoa agizo la kufukuzwa kwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT) Daudi Balali, kukamatwa na kushitakiwa kwa kina Basil Mramba na Daniel Yona, Richmond na wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) lakini, yote yakatekelezwa na serikali ya Kikwete."
Alisema alipokuwa Mbunge wa Karatu, alifanikisha jimbo hilo kuwa la kwanza kupunguza kodi za manyanyaso na kisha kujenga shule na zahanati za kata.
“Wakati Karatu tunazungumzia shule na zahanati za kijiji, ndio wenzetu bado wako katika shule na zahanati za kata. Haya yote ni maagizo ya Dk Slaa,” alisema.
Awali akihutubia wakazi wa Geita, Dk Slaa alisema inasikitisha kuona ndani ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania, wilaya ya Geita haina maji safi na salama ya kunywa na umeme wa uhakika, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini.
Alisema Watanzania wasifikiri kuwa madini na rasilimali nyingine zitakaa milele ardhini bali zinapungua kwa sababu hazizai.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za serikali mwaka 2007, Tanzania ina tani za dhahabu 2222 ambazo ni sawa na malori 20 tu ya tani 10 kila moja.
Alisema uvunaji wa dhahabu unazidi kuporomoka kadiri miaka inavyosonga mbele.
“Mwaka 2000 Tanzania ilivuna dhahabu kilogramu 15,000, 2001 kilogramu 30,000, 2002 kilogramu 43220, 2003 kilogramu 48,000, 2004 kilogramu 48,900, 2005 kilogramu 42,000, lakini mwaka 2006, uzalishaji ulianza kuporomoka,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Mwaka 2006 tulizalisha kilogramu 36,000 na 2007 kilogramu 37,600, hivyo tusipokuwa makini, tutabakishiwa mahandaki na dhahabu yote itakwenda Ulaya na Marekani”.
Alisema mwekezaji wa madini wilayani Geita ana magari 400 lakini, anaagizia matairi yote kutoka Afrika ya Kusini kwa sababu serikali ya CCM, imeua viwanda vyote.
Dk Slaa aliahidi kushughulikia tatizo la DECI ndani ya siku 100 tu baada ya kuingia Ikulu na kulipatia ufumbuzi juu ya fedha zao Sh15 bilioni walizokuwa wamepanda.
Kigogo Chadema aingia katika matatizo
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Hamad Yussuf huenda akaondolewa katika timu ya kampeni ya mgombea urais wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya kubainika kuwa hawajibiki ipasavyo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zimeeleza kuwa kiongozi huyo uamuzi huo unatokana na Chadema kumwona kuwa ni kero katika msafara wa mgombea wao.
“Leo (jana) tutakutana na jopo lote la viongozi wa Chadema Makao Makuu akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe katika mkutano wa mwisho utakaofanyika jijini Mwanza. Kutakuwa na ripoti maalumu itakayotolewa kuhusu Naibu katibu Mkuu huyo,” alidokeza kiongozi mmoja wa chama hicho aliyeomba kutotajwa gazetini.
Kiongozi huyo mwandamizi alidia: “Baadaye tutaiomba makao makuu, imwondoe katika msafara na kumrejesha nyumbani kwa sababu amekuwa kero ndani ya msafara chama”.
Katika ufunguzi wa kampeni za Chadema Agosti 28 mwaka huu, Jangwani jijini Dar es Salaam Yussuf aliisumbua CCM baada ya kumfananisha Dk Slaa na bwana harusi.
Baada ya mkutano huo wa ufunguzi wa kampeni, kiongozi huyo wa Chadema aliambatana na msafara wa Dk Slaa kuzunguka nchi nzima wakianzia mikoa ya Morogoro, Dodoma , Manyara, Singida na sasa Mwanza.
Hata hivyo, mvuto wa kiongozi huyo unadaiwa kupungua katika mkoani Singida baada ya wananchi kumkimbia jukwaani.
Mwanasheria maarufu nchini na kada wa Chadema Mabere Marando amesema anajiandaa kukilipua mabomu mengine.
Marando alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu kuhusu kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini.
Kauli hiyo ya Marando imekuja wiki mbili tangu akilipue kwa mabomu chama hicho ya kuwatuhumu makada wake kuhusika na wizi wa fedha za EPA katika uzinduzi wa kampeni za Chadema uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo Marando aliahidi kuwapiga tena mabomu viongozi wa CCM.
"Ndiyo nasema haya kwa sababu nafahamu hawawezi kunifanya chochote kwani wakithubutu nitawapeleka mahakamani," alisema Marando baada ya kuwataja vigogo hao kwa majina.
Marando alisema mabomu yake kwa CCM bado yapo, lakini kwa sasa la msingi ni kuhakikisha Chadema inashinda katika uchaguzi mkuu ujao na kwamba, mabomu yapo palepale na atayatoa wakati wowote.
"Huu ni muda wa kampeni, sasa natekeleza maagizo ya chama, ni kuhakikisha tunauza sera ya chama chetu ili kipate ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
“Hilo ndilo la msingi, lakini zaidi kuhusu kampeni zetu muulize Profesa Mwesiga Baregu au Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika watakueleza zaidi, mabomu yangu yapo nitayatoa," alisema Marando bila kutaja atayatoa lini.
Shina la Chadema lavamiwa
WATU wasiojulikana walivamia shina la ofisi ya chadema lililopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana na kungoa mlingoti wa bendera ya chama hicho na kuchana mabango ya wagombea wake wanafasi mbalimbali.
Katibu Mwenezi wa chama hicho, Jimbo la Kinondoni Moses Raymond alisema walibaini tukio hilo jana asubuhi, baada ya kufika katika ofisi hizo.
Alisema mlingoti uliongolewa ulikuwa na bendera ya chama hicho na kuchanwa mabango ya mgombea urais wa chama hicho Wallboard Slaa, wagombea ubunge wa jimbo la kinondonina ubunge Ubungo na madiwani wa kati mbalimbali zilizopo katika jimbo hilo.
Alisema tukio hilo wameshaliripoti katika kituo cha polisi cha ostabay, kwa uchunguzi na hatua zaidi.
“Hata sisi tunaendelea kufanya uchunguzi ili tukiwabaini tuwapeleke poisi,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Exuper Kachenje, Fredy Azzah na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment