Tamko la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Juu ya Mauaji ya Wananchi wakati wa Maandamano ya Amani yaliyofanyika Arusha tarehe 5 Jan, 2011
UTANGULIZI
Tumekutana hapa leo hii kwa huzuni kubwa. Tumekutana hapa leo hii kwa sababu watoto wa familia mbili wamepoteza baba zao na mama wa familia hizo wamepoteza waume na wenzi wao wa maisha. Tumekutana hapa leo kwa sababu wazazi wa familia mbili wamepotelewa na watoto wao wa kiume. Tumekutana hapa leo kwa sababu kuna familia nyingine – kwa sababu taarifa zetu za awali zinaonyesha watu wengine zaidi wameuawa - zimepotelewa na wapendwa wao vile vile.
Tumekutana hapa leo kwa sababu mamia ya wananchi wa Jiji hili wameumizwa kwa kupigwa risasi za moto, kupigwa mabomu ya machozi na/au kupigwa kwa virungu na mabuti ya Jeshi la Polisi la Tanzania. Tumekutana hapa leo kwa sababu wote waliokufa na tunaowaomboleza leo na wote walioumizwa na/au kuharibiwa mali zao hawakufikwa na mauti na/au majanga hayo kwa ajali ya barabarani au tetemeko la ardhi. Tumekutana hapa kwa sababu wote waliofikwa na mauti wameuawa na wote walioumia wameumizwa na Jeshi la Polisi la Tanzania.
Tumekutana hapa leo kwa sababu Jeshi la Polisi la Tanzania halipaswi, na halikupaswa, kuua wananchi wasiokuwa na hatia yoyote na ambao walikuwa wanatumia haki yao ya kufanya maandamano ya amani inayotambuliwa na Katiba na sheria za nchi yetu. Na tumekutana hapa leo ili kulinda na kutetea haki hiyo na kuzuia nchi yetu kuwa dola ya kipolisi inayoendeshwa kwa amri za kijeshi na za watawala na sio kwa matakwa ya wananchi.
Lakini, ndugu wananchi wa Arusha, tumekutana hapa ili kuomboleza kwa pamoja na tunahitaji kuomboleza kwa amani. Kwenye msiba watu hawapigani na tunawaomba tusipigane kwenye msiba huu. Kwenye msiba watu hawafanyi fujo na tunawaomba tusifanye fujo kwenye msiba huu. Tunawaomba tuomboleze kwa amani ili tusiwape wale walioua ndugu zetu sababu ya kusema kwamba sisi tunapenda fujo na uvunjifu wa amani.
SIKU YA KIHISTORIA
Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Jiji la Arusha. Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo haitasahaulika katika historia ya Tanzania. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania – ambalo limepewa wajibu wa kisheria wa ‘kulinda amani, sheria na utulivu, kugundua na kuzuia uhalifu, kukamata na kudhibiti wahalifu na kulinda mali za wananchi – liliamua kwa makusudi kuacha kutimiza wajibu wake kisheria na kujipa wajibu mwingine wa kuwa ni Jeshi la kuvunja amani, kukiuka sheria, kuvuruga utulivu, kufanya uhalifu na kuharibu mali za wananchi. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania – ambalo limejipachika kauli mbiu ya ‘Ulinzi wa Raia na Mali Zao’ – liliamua kwa makusudi kubadili kauli mbiu yake kuwa ni ‘Mauaji ya Raia na uharibifu wa mali zao’!
Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo wananchi wa Jiji la Arusha walivamiwa kwa makusudi, waliuawa kikatili na kupigwa na kuumizwa bila kosa au sababu yoyote ya msingi. Ni siku ambayo Jeshi la Polisi la Tanzania lilitumia silaha kubwa kubwa – risasi za moto, mabomu ya machozi na magari ya maji ya kuwasha – dhidi ya raia waliokuwa na vitambaa vyeupe vyenye kuashiria amani. Tarehe 5 Januari 2011 ni siku ambayo – kama ilivyokuwa tarehe 26 na 27 Januari 2001 – Jeshi la Polisi la Tanzania lilitukumbusha tena kwamba liko tayari kumwaga damu ya Watanzania wasiokuwa na hatia ili kulinda wizi wa kura na unyongaji wa demokrasia unaofanywa na watawala wa Chama cha Mapinduzi.
Kama ilivyokuwa Zanzibar miaka kumi iliyopita ndivyo ambavyo imekuwa Arusha mwaka huu: tumeanza Mwaka Mpya kwa umwagaji wa damu na maombolezo badala ya sherehe na kutakiana heri! Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa Zanzibar baada ya mauaji ya Januari 2001, CHADEMA haitakubali kununuliwa au kunyamazishwa kwa kuvikwa vilemba vya ukoka na/au kupewa vipande thelathini vya fedha ili kunyamazia mauaji ya wananchi wetu: Mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia hayatazuia jitihada za kujikomboa kutoka kwenye makucha ya utawala wa CCM. Mti wa haki uliorutubishwa kwa damu isiyokuwa na hatia ya wananchi wa Arusha utaendelea kukua na kuenea Tanzania nzima. Tarehe 5 Januari 2011 itakuwa siku itakayokumbukwa katika historia ya nchi yetu kama ni siku ambayo jitihada za ukombozi wa nchi yetu zilipata msukumo mkubwa.
MAANDAMANO HALALI
Jeshi la Polisi lilijua kwamba kutakuwa na maandamano ya amani ambayo yangefuatiwa na mkutano wa hadhara. Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu njia na/au barabara za Jiji la Arusha ambazo maandano hayo ya amani yangepitia hadi kufika kwenye eneo la Viwanja vya NMC ambako mkutano wa hadhara ungefanyika. Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu muda wa kuanza maandamano hayo ya amani na muda wa kumalizika kwa mkutano wa hadhara.
Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linafahamu yote hayo sio kwa sababu ya ‘taarifa za kiintelijensia’ ambayo ndio imekuwa kisingizio cha Jeshi la Polisi la Tanzania kukanyaga haki za kikatiba za wananchi wa Tanzania kupinga serikali ya CCM kwa njia za amani kwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Jeshi la Polisi la Tanzania lilifahamu yote hayo kwa sababu Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilifuata taratibu zote za kisheria za kufanya maandamano na mikutano ya hadhara. Tarehe 3 Januari 2011 CHADEMA ilitoa taarifa ya maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kuhusu nia yake ya kufanya maandano ya amani yatakayofuatiwa na mkutano wa hadhara ili kupinga kitendo cha watawala wa CCM kuwalazimishia wananchi wa Jiji la Arusha Meya ya Jiji kwa njia za kiharamia.
Tarehe hiyo hiyo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha alifanya kikao na viongozi wa CHADEMA kwa lengo la kukubaliana njia na/au barabara zitakazotumiwa na waandamanaji hadi kufikia Viwanja vya NMC. Baada ya hapo, pamoja na kwamba hakuwa na haja ya kisheria ya kufanya hivyo, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha aliifahamisha CHADEMA kwa maandishi kwamba maandamano yetu ya amani na mkutano wa hadhara yalikuwa yameruhusiwa na Jeshi la Polisi la Tanzania. Hatua zote tulizozichukua na ambazo tumezitaja hapa zilifanyika kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na vile vile kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Lakini hata kabla ya hapo, Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linajua kwamba CHADEMA ingefanya maandamano ya amani kushinikiza utekelezaji wa madai yetu tuliyoyatoa kwa maandishi kwa serikali na nakala yake kupatiwa Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema mnamo tarehe 23 Desemba 2010. Katika barua yake, CHADEMA ilidai kwamba uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ufutwe na kurudiwa; Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Jiji afukuzwe kazi kwa kushiriki katika ukiukwaji wa sheria za uchaguzi wa viongozi wa halmashauri za serikali za mitaa; na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha avuliwe madaraka yake kwa kushiriki kumpiga Mbunge wetu wa Jimbo la Arusha Mjini aliyekuwa anajaribu kutetea sheria za nchi yetu za uchaguzi wa viongozi wa halmashauri za serikali za mitaa.
CHADEMA ilitoa nafasi ya wiki mbili kwa serikali kutekeleza madai hayo la sivyo ingeandaa maandamano ya amani ya wananchi wa Arusha. Ni wazi, kwa hiyo, kwamba CHADEMA haikukimbilia kuandaa maandamano hata kama haikuwa kosa dhidi ya sheria za Tanzania kufanya hivyo. Kabla ya matukio ya maandamano ya tarehe 5 Januari, CHADEMA ilishaweka wazi utayari wake wa kumaliza mgogoro wa Arusha kwa njia za mazungumzo. Barua yetu ya tarehe 23 Desemba 2010 kwa serikali na kwa Jeshi la Polisi la Tanzania haijajibiwa hadi leo hii!
JESHI LA WAHALIFU!
Baada ya taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA kutolewa kwa mujibu wa sheria zilizotajwa, njia pekee halali ya kusitisha maandamano na mkutano uliopangwa ilikuwa ni kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha kutoa amri ya kusitisha maandamano na mkutano huo. Na Sheria ya Jeshi la Polisi inasema wazi kwamba Ofisa wa Polisi aliyepewa taarifa ya maandamano au mkutano hatatoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo ‘isipokuwa tu kama amejiridhisha kwamba maandamano au mkutano huo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma au kutumiwa kwa malengo haramu.’
Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kikishatoa taarifa ya mkutano kinaruhusiwa kufanya mkutano huo isipokuwa tu na kama kitapokea amri kutoka kwa ofisa wa polisi mwenye mamlaka ya eneo husika ikielekeza kwamba mkutano huo usifanyike kama ilivyopangwa. Na chini ya sheria hii vile vile, ofisa wa polisi aliyepewa taarifa ya mkutano haruhusiwi kutoa amri ya kuzuia au kusitisha maandamano au mkutano huo mpaka atakapojiridhisha kwamba mkutano au maandamano hayo yana lengo la kutekeleza au kutumiwa kwa malengo haramu; au kama maandamano au mkutano huo unaweza au umelenga kusababisha uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama na/au utulivu wa umma katika eneo husika. Kwa vyovyote vile kwa mujibu wa sheria hizi mbili, amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano au mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa ni lazima iwe ni ya maandishi.
Na hata kama ‘taarifa za kiintelijensia’ alizozisema Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema zilikuwa na ukweli - kwamba kulikuwa na uwezekano wa uvunjifu wa amani iwapo maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA ungeendelea kama ilivyokuwa imepangwa - bado Jeshi la Polisi la Tanzania lisingepaswa kutoa amri ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu, kuzuia na/au kusitisha maandamano sio hatua pekee inayoweza kuchukuliwa na Jeshi la Polisi la Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama ambacho kimesajiliwa ‘kina haki ya kupatiwa ulinzi na msaada wa vyombo vya ulinzi kwa malengo ya kuwezesha mikutano yenye amani na utulivu.’
Jeshi la Polisi la Tanzania lilikiuka kwa makusudi masharti haya ya sheria. Kwanza, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha ambaye ndiye ofisa anayetakiwa kupatiwa taarifa ya maandamano na mkutano wa hadhara hakuwahi kuipa CHADEMA taarifa yoyote ya maandishi ya kuzuia na/au kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara uliotolewa taarifa rasmi kwake kwa mujibu wa sheria. Taarifa na/au amri pekee tunayoisikia ya kuzuia na/au kusitisha maandamano ni ile inayosemekana ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha jioni ya tarehe 4 Januari 2011. Taarifa na/au amri hiyo – kama kweli ilikuwepo - ilikuwa ni haramu kwa sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa hana mamlaka yoyote ya kuruhusu au kukataza maandamano na/au mikutano ya vyama vya siasa. Mtu pekee mwenye mamlaka hayo chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa ni ‘ofisa polisi mwenye mamlaka ya eneo’ la mkutano, kwa maana nyingine, Mkuu wa Polisi wa Wilaya!
Aidha, tuna taarifa kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba maandamano na mkutano wa hadhara wa CHADEMA yamepigwa marufuku kutokana na kuwepo kwa ‘taarifa za kiintelijensia’ kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani wakati wa maandamano na/au mkutano huo wa hadhara. Tangazo hilo la Inspekta Jenerali wa Polisi lilikuwa haramu na ni ukiukaji wa makusudi wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa sababu Inspekta Jenerali wa Polisi hana mamlaka yoyote kisheria ya kuzuia au kuruhusu maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Vile vile utaratibu wa kutoa amri za kuzuia ama kusitisha maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa kutumia matangazo ya televisheni na/au waandishi wa habari ni utaratibu mgeni katika nchi ya Tanzania na hautambuliwi kabisa na sheria hizo!
Lakini hata kama maandamano na mkutano wetu wa hadhara yangekuwa yamepigwa marufuku kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa – kitu ambacho hakikufanyika – bado CHADEMA ilikuwa na uhalali wa kuendelea na maandamano hayo na kufanya mkutano kama ilivyopangwa. Hii ni kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kulinda uhuru wa wananchi ‘kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani….’ Hii ina maana kwamba uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara umepanuliwa sana na hauwezi kupokonywa kihalali kwa visingizio vya ‘taarifa za kiintelijensia’ vya Jeshi la Polisi la Tanzania.
Kwa hiyo wananchi wa Arusha walivamiwa na kupigwa risasi zilizowaua au kuwajeruhi sio kwa sababu walikuwa wamevunja sheria yoyote ya Tanzania. Walivamiwa na kuuawa au kujeruhiwa na mali zao kuharibiwa sio kwa sababu walifanya kosa lolote linalotambuliwa na sheria za nchi yetu. Viongozi wa CHADEMA kuanzia ngazi za juu za kitaifa hadi ngazi za chini na wanachama wetu wa kawaida walishambuliwa kwa risasi na mabomu na baadaye kujazwa kwenye mahabusu za polisi sio kwa sababu walikiuka sheria yoyote. Wananchi wa Arusha walifanyiwa uhalifu wote huo licha ya kwamba Katiba ya nchi yetu inatambua na kulinda uhuru wa wananchi wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.
MAUAJI YA KUPANGWA
Mauaji ya Arusha yalifanywa kwa makusudi na kwa kupangwa. Jeshi la Polisi la Tanzania lilipanga na kutekeleza mauaji hayo. Lakini sio Jeshi la Polisi la Tanzania pekee lenye kuhusika na mauaji ya wananchi wetu. Rais Kikwete na serikali yake na chama chake cha CCM wanahusika moja kwa moja na damu iliyomwagwa kwa makusudi Arusha. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kikwete ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama. Aidha, chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi – ambaye ni mteuliwa wa Rais – anawajibika kufuata amri na maelekezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani – mteuliwa mwingine wa Rais – kuhusiana na udhibiti wa shughuli za Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, kikatiba na kisheria, Jeshi la Polisi liko chini ya mamlaka ya Rais na wateuliwa wake kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Inspekta Jenerali wa Polisi.
Pamoja na mamlaka ya Rais juu ya Jeshi la Polisi, Kikwete mwenyewe alikwishatoa kauli na matamko hadharani ambayo yaliashiria kwamba Jeshi la Polisi la Tanzania lilikuwa linajiandaa kumwaga damu ya Watanzania ili kulinda utawala wake na wa chama chake. Kwa mfano, katika hotuba yake ya Mwaka Mpya aliyoitoa usiku wa tarehe 31 Desemba 2010, Kikwete alidai kwamba ‘… wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa … wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara…. Wao hasa wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya dola kuingilia ati waiambie jumuiya ya kimataifa jinsi Serikali yetu ilivyo katili.’ Katiba hotuba hiyo, Kikwete alizungumzia kile alichokiita wananchi ‘kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara’!
Rais aliyasema hayo wiki moja baada ya barua yetu kwa serikali yake juu ya nia ya CHADEMA kufanya maandamano ya amani iwapo serikali yake isingechukua hatua tulizodai zichukuliwe katika barua yetu ya tarehe 23 Desemba 2010. Haikupita hata wiki moja tangu Kikwete atoe kauli yake hiyo na Jeshi la Polisi la Tanzania limemwaga damu ya Watanzania Arusha. Jeshi la Polisi la Tanzania limetekeleza maagizo ya Amiri Jeshi wake mkuu, ndio maana Amiri Jeshi Mkuu huyo hajatoa kauli yoyote kwa Watanzania kuhusiana na matukio haya ya kusikitisha na wala kuchukua hatua kuwawajibisha wale waliotoa amri za kuua na kuumiza Watanzania na/au waliozitekeleza.
KISASI CHA UCHAGUZI MKUU!
Mauaji ya wananchi wetu, matumizi ya nguvu ya kutisha dhidi ya wanawake, watoto na wazee na kukamatwa kwa mamia ya viongozi, wanachama na wananchi wa kawaida wa Jiji la Arusha ilikuwa ni kulipa kisasi kwa viongozi wa CHADEMA wa ngazi zote na kwa wananchi wa Arusha kwa kudiriki kuisambaratisha CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania lilidiriki kumvamia na kumpiga Mbunge wetu wa Arusha Mjini hadi akapoteza fahamu wakati alipojaribu kulinda haki ya wananchi wa Arusha kuwa na Meya wa Jiji wanayemtaka na sio anayetakiwa na mafisadi wa nchi hii na chama chao.
Jeshi la Polisi la Tanzania limelipa kisasi kwa niaba ya CCM kwa sababu wananchi wa Arusha wamediriki kutumia haki zao za kisheria kupinga mipango ya mafisadi kuingiza Meya wa Jiji la Arusha atakayelinda maslahi ya mafisadi na chama chao. Wananchi wa Arusha wamelipiziwa kisasi na Jeshi la Polisi la Tanzania kwa sababu mafisadi wanajua wangeruhusu haki itendeke katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha CCM ingesambaratishwa kama ilivyosambaratishwa katika Uchaguzi Mkuu.
Mauaji ya Arusha sio kisasi cha CCM dhidi wananchi wa Arusha tu. Ni kisasi pia dhidi ya wananchi wa Tanzania na dhidi ya CHADEMA. Ni kisasi dhidi ya Watanzania wote kwa sababu, kwa mara kwanza tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa urudishwe mwaka 1992, Uchaguzi Mkuu wa 2010 ulionyesha wazi kwamba CCM imeanza safari yake ya mwisho kuelekea kwenye jaa la taka taka la historia. Kwa mara ya kwanza, CCM ilipoteza miji mikubwa karibu yote ya Tanzania. Licha ya uchakachuaji wa kura, rushwa na uharamia wa kutisha, CCM imepoteza Jiji la Dar es Salaam, Jiji la Mwanza, Jiji la Arusha, Jiji la Mbeya na miji mikubwa kama vile Moshi, Iringa na Musoma.
Lakini CCM na mafisadi hawakupoteza miji tu, wamepoteza pia majimbo ya vijijini. CCM imepoteza nusu ya Shinyanga, zaidi ya nusu ya Kigoma, sehemu kubwa za Manyara, Singida, Mbeya, Iringa na mikoa mingine ambayo kihistoria imekuwa inaonekana kama ngome za CCM. Na licha ya nguvu nyingi za dola na za fedha za ufisadi, Jakaya Kikwete amepunguza idadi ya kura zake kutoka kura zaidi ya milioni nane alizopata wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 hadi kura milioni tano za mwaka jana, ikiwa ni pungufu ya zaidi ya kura milioni tatu na anguko la asilimia 20!
Kuporomoka kwa CCM kumeenda sambamba na kukua na kuongezeka kwa nguvu ya CHADEMA. Licha ya uchakachuaji wa kura wa kutisha, matumizi ya vyombo vya dola na rushwa ya kutisha, nguvu na ushawishi wa CHADEMA imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ndio chama cha upinzani chenye Wabunge wengi kuliko vyama vingine vyote vya upinzani kwa pamoja. Ndio chama pekee cha upinzani kilichowahi kupata Wabunge kutoka kanda zote za Tanzania Bara na Visiwani. Ndio chama cha upinzani pekee kilichowahi kupata zaidi ya robo ya kura zote za Rais na Wabunge. Na ndio chama pekee chenye kubeba matumaini ya wananchi wa Tanzania kwamba Tanzania bila ufisadi wa CCM inawezekana. Ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania limelipizia kisasi cha CCM kwa wananchi wa Arusha na viongozi, wanachama na wapenzi wa CHADEMA.
HAKI LAZIMA ITENDEKE ARUSHA!
Damu iliyomwagwa Arusha inalilia haki. Roho za wote waliotolewa muhanga na Jeshi la Polisi la Tanzania zinahitaji haki ili ziweze kutulia na mizimu yao ipumzike. Wote walioumizwa na ujambazi wa Jeshi la Polisi la Tanzania wanalilia fidia ili waweze kuuguza maumivu yao ya kimwili, ya kiroho na ya mali zao zilizoharibiwa. Sheria za nchi yetu zilizokanyagwa chini kana kwamba hazipo zinahitaji kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa ili iwe fundisho kwa wahalifu wengine wa aina hii.
Kwa hiyo, sisi wote tuliokusanyika hapa leo, na wale wote wanaotusikiliza mahali popote nchini na hata nje ya nchi yetu, tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale ambao tunaomboleza vifo vyao hapa leo. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wale wote walioumizwa kwa risasi na mabomu na virungu na mabuti ya Jeshi la Polisi la Tanzania. Tuna jukumu la kuhakikisha wale wote ambao waliharibiwa mali zao kwa sababu ya uhalifu huu wa Jeshi la Polisi la Tanzania wanafidiwa kwa kiasi chote cha hasara waliyoipata. Tuna jukumu la kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi la Tanzania halirudii tena ujambazi wa aina hii dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia yoyote kwa kuwawajibisha wale wote walioshiriki katika ujambazi huu kwa kutoa amri za kuua au kuumiza wananchi na/au kwa kuzitekeleza.
Ili tutimize majukumu yote haya, tunahitaji kuhakikisha kwamba mambo yafuatayo yanafanyika:
- Serikali hii iwajibike kwa wananchi kama ilivyotamkwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Waziri wa Mambo ya Nchi Shamsa Vuai Nahodha na Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema wajiuzulu mara moja ili kuwawajibisha kama viongozi na wasimamizi wa juu kabisa wa Jeshi la Polisi la Tanzania. Aidha, kujiuzulu kwao kutapisha uchunguzi huru na wa kina wa matukio yote yaliyosababisha wananchi wetu kuuawa, mamia kujeruhiwa na mamia mengine kukamatwa bila sababu yoyote na kuwekwa rumande na baadaye kufunguliwa mashtaka ya uongo ya jinai;
- Inspekta Jenerali wa Polisi Saidi Mwema, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Andengenye na wale wote walioamuru au kutekeleza amri ya kuvunja maandamano na mkutano halali wafunguliwe mashtaka ya jinai kwa matumizi mabaya ya madaraka na kwa kusababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia;
- Fidia stahili ilipwe kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na/au jamaa wa wale wote waliouawa kutokana na vitendo vya Jeshi la Polisi la Tanzania na kwa wale wote walioumizwa kwa namna yoyote ile na/au kuharibiwa mali zao kutokana na vitendo hivyo;
- Mashtaka ya uongo ya jinai yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa ngazi zote wa CHADEMA, wanachama, wafuasi na wananchi wengine wote waliokumbwa na kumba kumba ya Jeshi la Polisi la Tanzania yafutwe bila masharti yoyote kwa sababu maandamano na mkutano wa hadhara uliozuiliwa yalikuwa halali kwa mujibu wa sheria husika za nchi yetu. Tunasisitiza katika jambo hili kwamba viongozi, wanachama na wafuasi wetu wote waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka haya hawatahudhuria mahakamani tena kuhusiana kesi iliyofunguliwa dhidi yao hata kama kwa kufanya hivyo kutafanya wakamatwe na kurudishwa tena gerezani;
- Kwa vile uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ndio chanzo cha mauaji ya wananchi na kwa kufahamu utaratibu haramu uliotumika kumpata Meya wa Jiji hilo, matokeo ya uchaguzi huo yafutiliwe mbali na uchaguzi mpya uitishwe haraka iwezekanavyo kwa kufuata sheria husika za nchi yetu;
- Haki ya vyama vya siasa na wananchi kufanya maandamano ya amani kama inavyotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iheshimiwe na kutiliwa nguvu zaidi kwa kufuta vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi nay a Vyama vya Siasa vinavyoruhusu Jeshi la Polisi la Tanzania kuzuia na/au kusitisha maandamano ya amani. Badala yake, sheria ziweke wazi wajibu wa Jeshi la Polisi la Tanzania kulinda maandamano ya amani na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na/au ya wananchi;
- Tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoundwa na majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania iundwe ili kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa matukio yote yaliyopelekea Inspekta Jenerali wa Polisi na/au Jeshi la Polisi la Tanzania kupiga marufuku maandamano ya amani na mkutano wa hadhara na baadaye Jeshi la Polisi la Tanzania kufanya vurugu zilizosababisha mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia. Tunapenda kusisitiza kuundwa kwa tume huru ya kimahakama kwa sababu historia ya tume nyingine ambazo zimeundwa kwa utaratibu wa Rais kuteua watu anaowataka inaonyesha kwamba zimefanya kazi zao za uchunguzi mafichoni bila kushirikisha wadau wengine na bila wananchi kufahamu kitu kinachoendelea. Matokeo ya tume nyingi za namna hiyo ni kwamba ripoti zake mara nyingi zimepuuzwa na/au kufichwa na watawala. Tume ya uchunguzi ya kimahakama hufanya kazi zake kwa uwazi na huruhusu wananchi kuhudhuria na/au kushiriki moja kwa moja katika kazi za tume kama mashahidi na/au kwa kuhoji mashahidi wengine wanaotoa taarifa kwenye tume hiyo;
Katika kuhakikisha kwamba madai yetu yanatekelezwa, CHADEMA inaelekeza viongozi, wanachama na wafuasi wetu mikoani na Wilayani kuandaa maandamano ya amani nchi nzima ili kulaani mauaji ya wananchi wa Arusha na kudai utekelezaji wa madai haya. CHADEMA Makao Makuu itatuma maafisa wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo Wabunge na Wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kushiriki katika maandamano hayo kwa ngazi za mikoa na wilaya ili kuyaongezea nguvu na hamasa.
MAUAJI YA ARUSHA NA UMUHIMU WA KATIBA MPYA
Mauaji ya wananchi wa Arusha yanadhihirisha wazi umuhimu wa kuwa na Katiba mpya kwa ajili ya nchi yetu. Hii ni kwa sababu, Katiba viraka inayotumika sasa hivi haiheshimiwi hasa na watawala wenyewe kama tulivyoonyesha kuhusiana na uhuru wa kufanya maandamano ya amani na mikutano ya hadhara. Aidha, Katiba yetu na sheria nyingine kama vile Sheria ya Jeshi la Polisi na ya Vyama vya Siasa zimetoa mamlaka makubwa mno kwa watendaji kama vile mapolisi kuingilia na kuvuruga haki za wananchi. Mamlaka haya ya kisheria hayana udhibiti wowote wa maana ndio maana Jeshi la Polisi la Tanzania linajiona kama liko juu ya sheria na haliwajibiki kwa makosa yoyote yanayofanywa na Jeshi hilo dhidi ya wananchi.
Aidha, matukio yaliyopelekea Mauaji ya Arusha yanaonyesha kwamba mfumo mzima wa kisheria na kitaasisi wa kuendesha chaguzi katika nchi yetu unahitaji mabadiliko makubwa. Matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini – kama ilivyokuwa kwa majimbo mengine walikoshinda wagombea wa upinzani - yalitolewa baada ya shinikizo kubwa la nguvu ya umma na sio kwa sababu ya utashi na/au uadilifu wa wasimamizi wa uchaguzi. Na kilichotuleta hapa leo ni matokeo ya uchakachuaji wa uchaguzi wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na viongozi wengine wa Halmashauri hiyo.
Sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba tunapata Katiba mpya itakayohakikisha kwamba vyombo vya ulinzi wa wananchi vinakuwa chini ya udhibiti halisi wa wananchi na/au vyombo vyao vya uwakilishi. Sasa ni muda muafaka kuhakikisha kwamba tunapata Katiba mpya itakayohakikisha kwamba mfumo wetu wa uchaguzi ni huru na wa haki kwa watu na vyama vyote. Sasa ni muda muafaka kuhakikisha tunakuwa na Katiba mpya itakayohakikisha kwamba siku za huzuni kama ya leo zinabaki katika kumbu kumbu za kihistoria tu. Na kwenye suala hili la Katiba mpya tunaujulisha umma wa Watanzania kwamba hatukubaliani hata kidogo na utaratibu uliopendekezwa na Rais Kikwete wa kuunda Tume ya Kupitia Katiba. Utaratibu uliopendekezwa ni ule ule uliotufikisha hapa tulipo. Ni utaratibu wa kubadili Katiba wa watu wale wale unaoendeshwa na/au kusimamiwa na watu wale wale kwa manufaa ya watu wale wale.
Utaratibu ambao CHADEMA itauunga mkono na kushiriki kikamilifu ni ule utakaowezesha kufanyika kwa Mkutano wa Kitaifa wa Katiba ambao utawakilisha makundi yote ya kijamii katika uundaji wa Katiba mpya. Utaratibu wa kusubiri fadhila za Kikwete za kuteua wajumbe wa Tume ya Katiba haukubaliki tena na CHADEMA haitaubariki kwa kushiriki. Aidha, CHADEMA itatumia uwezo wake wote kuhamasisha wananchi nchi nzima ili kupinga utaratibu unaopendekezwa na Kikwete na kuunga mkono utaratibu wa kidemokrasia wa kupata Katiba mpya kwa kupitia Mkutano wa Kitaifa wa Katiba.
Mh. Freeman Mbowe (Mb)
Mwenyekiti Taifa
12 Januari, 2011
0 comments:
Post a Comment