Na. M. M. Mwanakijiji
Njia ya Dr. Slaa kuingia Ikulu inapitia moja kwa moja katika migongo na mabega ya Zitto Kabwe na Freeman Mbowe. Na pamoja nayo inapitia katika pembetatu ya watu hawa watatu kuongoza shambulizi la mwisho katika wiki hizi mbili zilizosalia kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010.
Kama kuna kiongozi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema anayeamini kuwa ipo nafasi nyingine ya kugombania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushinda nje ya nafasi hii ya 2010 basi mtu huyo anajidanganya. Kama wapo wanachama na mashabiki ambao wanaamini kuwa wakati wa kugombea Urais na kushinda siyo sasa na hivyo wasubiri hadi 2015 au 2010 watu hao vile vile wanajizuga wao wenyewe. Endapo viongozi, wanachama na mashabiki wa Chama hicho maarufu cha upinzani nchini hawatafanya yote wanayopaswa na wanayoweza kufanya katika wiki hizi mbili za mwisho za kampeni basi ndoto ya kuupata Urais itatoweka kama umande wa alfajiri.
Nalazimika kuandika hili kama kuwatia shime wale wote ambao wanataka kweli mabadiliko nchini kupitia chama hicho kuondoa vizuizi vyote vya kihisia na kiakili na kutumia nafasi hii ya kihistoria kuweza kuigombania ipasavyo nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano.
Mkakati wowote wa kutaka kupata wabunge wengi zaidi na siyo kupata Urais wa Jamhuri ya Muungano ni mkakati uliokubali nafasi ya kudumu ya upinzani. Kama viongozi na mashabiki wa Chadema wanapita na kuhamisha watu wawachague wabunge ili kuwe na wabunge zaidi Bungeni ili kwa kufanya hivyo waanze kusikilizwa zaidi na CCM basi watu hao wanakuwa wamekubali nafasi ya upinzani na hawako tayari kuwa watawala. Mkakati wa kupata wabunge wengi ni mkakati mzuri isipokuwa pale tu unapoendana na lengo zima la kutaka nafasi ya urais vile vile.
Ninasema hili kwa sababu kuwa na wabunge wengi wenye kuzungumza zaidi na wenye kufumua mambo mengi Bungeni wakati bado Rais ni wa chama tawala ni kuongeza kelele zaidi Bungeni na “wapiganaji” zaidi lakini ikiangaliwa kwa ukaribu itaonekana ni kujaribu kuwa na miaka mitano iliyopita tena Bungeni. Namna pekee ya kuwa na wabunge wengi bila ya kuwa na Rais inaweza kufaa kama lengo ni kuwa na wingi zaidi ya wabunge kuliko CCM au chama kingine chochote na hivyo kuwa katika uwezekano wa kumtoa Waziri Mkuu, japo siyo lazima kwani kunaweza kuwa na mbunge mwingine anayeonekana kuungwa mkono na wabunge wengi.
Lakini kama lengo ni kuwa na wabunge wengi tu ili kuongeza idadi na hivyo kuwa na “sauti zaidi” basi lengo hili ni zuri kwa kiasi fulani tu na ni kiasi kile kwamba wingi mkubwa wa wabunge wa CCM (super majority) ukiondolewa basi CCM haitoweza tena kubadili Katiba kama ipendavyo au kupitisha mijadala kirahisi rahisi. Katika mazingira hayo vyama vilivyoko Bungeni vitalazimika kujadiliana na kukubaliana na kujifunza kuachiliana vile vile ili mambo yaende. Hili likifanikiwa basi ni jambo kubwa na jema.
Hata hivyo, chama cha siasa chenye kuona tuzo wanayostahili kwa kazi ngumu ni Bunge zaidi na Ikulu wako tayari mwingine aendelee kuishikilia kinajiwekea kizuizi kisicho cha lazima. Chama cha siasa lengo lake ni kuchukua Bunge na Urais ili kwa kufanya hivyo kiweze chenyewe kutekeleza ajenda zake na ilani yake ya uchaguzi. CCM inapopita kuomba kura na kupiga kampeni hakimpigii kampeni Rais tu bali pamoja na wabunge na madiwani wake. Ni katika kutambua hili CCM inaweza kuwa na uhakika wa kutekeleza sera zake na ilani yake. Vivyo hivyo Chadema kama kinajiamini kuwa kimekomaa na kiko tayari kushika madaraka ya juu kabisa ya utawala ni lazima viongozi wake wote, wanachama na mashabiki wake wawe na lengo hilo wazi kabisa katika fikra zao yaani ni lazima wagombea wa ubunge wa Chadema wachaguliwe, wagombea wa Udiwani nao wachaguliwe na yule wa Urais naye achaguliwe. Kusisitiza kuchagua wabunge na madiwani tu bila kusisitiza kuchaguliwa kwa Rais ili chama kiunde serikali siyo mkakati mzuri.
Katika kufikia lengo hilo kwa upande wa Chadema ninaamin nafasi ya watu hawa wawili haiwezi kukwepeka. Mgombea wa Chadema na mbunge maarufu Bw. Zitto Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu ana nafasi ya pekee kumletea Dr. Slaa ushindi. Ukiondoa tofauti zao za ndani ya chama na migongano ambayo kama nilivyowahi kusema huko nyuma ni muhimu kwa afya ya Chama Zitto amekomaa zaidi kisiasa na kwa yeyote ambaye amemfuatilia kwenye kampeni zake na za kuwanadi wagombea wengine kwa hakika amevutiwa na utayari wake. Hata hivyo, bado Zitto hajajionesha kuwa anampigia Dr. Slaa debe ili achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zitto ni lazima atoke na aseme wazi na pasipo utata kuwa anamuunga mkono Dr. Slaa na anamuombea kura katika kila mikutano yake. Asionekane kusita hata kidogo.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema Bw. Freeman Mbowe naye ana nafasi ya pekee katika kumletea ushindi wa kihistoria Dr. Slaa. Hadi hivi sasa ameshafanya makosa makubwa mawili ya kimkakati na ninaamini historia itamhukumu vibaya kama atafanya kosa la tatu na la nne. Kosa la kwanza ni kuamua kugombea Hai tena kitu ambacho kimemlazimu kutumia muda mrefu jimboni humo na kama nilivyosema kwenye Chadema: Kutoka Hapa mpaka Kule CCM wataweka msukumo mkubwa Hai ili kuhakikisha Mbowe arudi Dar au haingii kwenye kampeni za Kitaifa za kumnadi Dr. Slaa. Hili hadi hivi sasa limefanikiwa na asipoweza kujinasua basi atakigharimu sana chama chake kitaifa. Kosa la pili linatokana na hilo la kwanza, kama habari kuwa “Mbowe ana wakati mgumu Hai” zina ukweli kutokana na vyanzo vyangu mbalimbali ninaamini wakati huu “mgumu” hautaisha hadi siku ya kura. Hivyo, Mbowe imemlazimu kufuatilia sana kampeni yake yeye mwenyewe kule Hai na kutokuwa msaada mkubwa kwenye kampeni ya kitaifa na CCM wataendelea kuweka presha zaidi Hai ili kuhakikisha kuwa wanamuangusha. Kumuangusha mtu anayejinadi kuwa ni Kamanda kwenye uwanja wake wa nyumbani itakuwa ni pigo kubwa la binafsi kwa Mbowe.
Lakini pamoja na ukweli wa hali halisi inayoendelea huko Hai ambako katika kampeni za CCM kumetazamwa kama “special case” Mbowe ni lazima anasuke. Ni lazima awe tayari kuitoa kafara Hai ili Dr. Slaa ashinde. Yeye naye anahitajika kuonekana katika mikutano nje ya Hai na sehemu nyingine (kama anvyofanya Zitto sasa) kuanza kuwapigia debe wagombea wengine wa Ubunge na Udiwani pamoja na Dr. Slaa. Hili ni kweli kwani kama kabla ya wiki mbili za uchaguzi Mbowe hana uhakika wa ushindi Hai basi ushindi kwake utakuwa ni mgumu mno. Kamanda mzuri vitani ni yule anayejua ni kita kipi cha kupigana na kipi cha kukiacha. Hivyo, kuna wakati wa vita basi majemedari huamua kupigana katika maeneo mbalimbali lakini maadui zao wakati mwingine hutengeneza kita mahali ili kuwavuta wapiganaji huko huku wao wenyewe wanaendeleza mapambano kwingine. CCM ilijua Mbowe atagombea Hai na walihakikisha kuwa akija hata pingamizi lolote hawaweki lakini watahakikisha wanamtoa katika mtandao wa kampeni ya Dr. Slaa. Bahati mbaya Mbowe ameingia kwenye mtego huu na ni vigumu kujinasua bila kwanza kuwa tayari kutoa kafara Jimbo la Hai. Mimi ninaamini kabisa Mbowe jimbo la Hai atashinda bila hata ya kutumia nguvu nyingi kwani anachokiona kuwa ni presha ya CCM si lolote zaidi ya kile kinachoitwa “drawing the enemy” yaani “kumvuta adui aje”. Mbowe apumzike siasa za Hai na mara moja aende maeneo mengine ya nchi kuwauza wagombea wa Chadema na kumwombea Dr. Slaa kura zaidi.
Ndugu zangu, ushindi wa uchaguzi mkubwa wa kisiasa kwenye nchi mara nyingi hauamuliwi siku ya kwanza ya kujiandikisha kupiga kura au wiki za mwanzo za kampeni. Utafiki wa kisayansi ya siasa unaonesha kuwa wapiga kura wengi hufanya uamuzi wao wiki mbili za mwisho za uchaguzi. Hadi hivi sasa matokeo yote ya kura za maoni yatakuwa na nguvu katika wiki hizi mbili zijazo na siyo yale ya Septemba au Machi. Wiki hizi mbili za mwisho ndizo zitaamua nani anashinda. Ni kutokana na ukweli huo ninaamini kile ambacho Chadema watafanya wiki hizi mbili ndicho hasa kitaamua kama wanaanguka au wanasimama.
Nimesema kuwa kile ambacho “chadema watafanya”. Maanake ni kwamba, ushindi wa Dr. Slaa na wagombea ubunge na udiwani wa Chadema hautaletwa na CCM, TLP au CUF. Hautaletwa na vyombo vya habari na hautaletwa na watu wanaokuja kuwashangilia kwenye mikutano; utaletwa na Chadema wenyewe. Ushindi hautaletwa kama zawadi bali unatakiwa kutafutwa, kupatikana na kuchukuliwa kama lulu iliyopotea. Na ushindi huo hautazuiliwa na CCM.
Kwa uhakika mkubwa naweza kusema kwamba hakuna jambo lolote ambalo CCM na makada wake na hata serikali yake wanaweza kufanya ambalo litaamua kama Chadema inashinda au la. Siamini kabisa kabisa kama Rais Kikwete, Bw. Kinana na Bw. Makamba wanaweza kufanya lolote kuzuia ushindi wa Chadema kama Chadema wanautaka na wanaenda kuuchukua. Kitu pekee CCM inaweza kufanya ni kupunguza makali yake.
Hii ina maana ya kwamba kushindwa au kushinda kwa Chadema kumo mikononi mwao wao peke yao kwa asilimia 1000. Mengine yote yatafuata yenyewe. Lakini ushindi huo utategemea moja kwa moja Pembetatu ya Ushindi (Triangle of Victory) yaani Dr.
Slaa, Freeman Mbowe na Zitto Kabwe. Hawa watatu katika mabega yao wamejibebesha mzigo wa kuiletea Chadema ushindi; naam ule “ushindi wa heshima” kama anavyoita Bw. Kabwe.
Hadi hivi sasa nikiri kuwa Dr. Slaa amefanya zaidi ya vile ambavyo wengi tulitarajia. Kwa kila kipimo Dr. Slaa amejionesha kuwa ni mwanasiasa aliyekomaa na ambaye anaweza kuhimili mikiki ya uchaguzi. Binafsi nikiri kuwa kwa mwanasiasa ambaye ameshambuliwa hadharani maisha yake binafsi (kuacha upadre), maisha yake ya chumbani (kuwa na Bi. Josephine) na kuhimili maumivu ya mkono uliovunjika na kukampeni na vijana wengi akihutubia mikutano mingi kila siku ni wazi kuwa Dr. Slaa ameshajiweka kwenye kaliba nyingine kabisa na kama mgombea sidhani kama wangeweza kumwomba afanye lolote zaidi. Katika wiki hizi mbili za mwisho ni hawa wengine ndio sasa wanaitwa na historia pamoja na wagombea wengine ambao bado wametingwa katika majimbo yao kufanya kile ambacho Umsolopagas alikiita ni “pigo takatifu”.
Ndugu zangu, kama ingekuwa ni ulingoni basi hii ni raundi ya kumi katika pambano la raundi kumi na mbili. Tayari tumeona CCM ikirusha masumbwi yake na Chadema wakirudisha. Hadi hivi sasa watazamaji wanaamini Chadema imeshenda kwa pointi. Na watu wanaamini kuwa ikiendelea hivi hivi katika raundi zilizobakia basi watashinda kwa pointi nyingi tu. Na kama viongozi wa Chadema wataendelea na mbinu zile zile na hotuba zile zile wakiamini kuwa zitawapa ushindi wajiandae kwa mshangao.
Katika mapambano ya ngumi usimdharau bondia mzoefu. CCM ni chama cha siasa na kinajua jinsi ya kufanya siasa (how to do politics). Chadema ni chama cha siasa lakini bado hakijamudu sana jinsi ya kufanya siasa. Ninaamini sasa hivi CCM inachofanya ni kumkumbatia tu huyu bondia mwingine huku ikimvuta muda kumfikisha raundi ya mwisho ambapo itaangusha ngumi kama mvua ili kuhakikisha inamtoa kwa KO. Hivyo, hata kama mnaiona CCM imeshikilia kamba inahema au inaruka ruka kwa mbali msidhani imeshashindwa. CCM bado ni chama chenye nguvu na chenye mbinu za hali ya juu za kisiasa. Yeyote anayewadharau ati kwa vile Chadema inaonekana kushinda asije kujikuta anapigwa na butwaa. Kwani ni mara ngapi tumewahi kuwaona mabondia wanaoongoza mapambano lakini dakika za mwisho wanajikuta hawana ubavu hata wa kurusha ngumi ya ushindi?
Chadema, mashabiki wake na wagombea wake wote wanazo wiki mbili kufikiria ni ngumi ipi na ilenge wapi ili kuhakikisha kuwa CCM ikinyukwa inapata kizunguzungu na kuanza kuona nyota za fedha za EPA zikiyeyuka hewani! Lakini kujiamini kuwa ati Chadema itashinda kwa vile watu wanaishangilia ni kutokujua siasa. Ni matumaini yangu Chadema na viongozi wake watabadilisha mbinu zao za vita, watamshangaza adui na zaidi sana watafanya kile ambacho CCM hata kuwaza kuwa Chadema inaweza kufanya haijawaza. Lakini wakiendelea na mtindo ule ule na mbinu zile zile ambazo CCM inazijua kwa muda mrefu, tusije kujikuta tunashangazwa na kuaza kulia “CCM wameiba kura”. CCM haina haja ya kuiba kura ili ishinde, CCM inahitaji kuchezea wapiga kura kisiasa tu ili ishinde, na nani atawalaumu hiyo ndiyo “siasa”. Chadema wajifunze kujua jinsi ya kufanya siasa dakika hizi za mwisho vinginevyo wasije kujikuta dakika za mwisho wanapatwa kwikwi.
Tayari wana ujumbe wenye kuungwa mkono na watu wengi, tayari wana wagombea viongozi wenye kukubalika na tayari wameshachochea nyoyo za Watanzania kutamani kitu tofauti nje ya CCM. Ndani ya miaka mitano wameikuta ardhi kavu, wameilowesha, wamepende mbegu, mazao yamekua na sasa wakati wa mavuno, Chadema ihakikishe inavuna kiuhakika. Isiionee huruma CCM, viongozi wake wasimuonee huruma Kikwete na CCM bali watoe na wawe tayari kutumia mbinu zote za kisiasa kwenda kupata ushindi. Isije baadaye watu wakaanza kusema “kwanini hamkufanya vile au hivi” na wao wakaanza kutafuta visingizio vya kuhalalisha kushindwa kwao, visingizio ambavyo vitakuwa ni vile vya nje ya chama. Ninaamini kuna mambo kama matatu au manne ambayo Chadema wakiamua kweli kuyafanya siyo tu kwamba watashika hatamu ya uongozi lakini wataonekana kwa haki kabisa wamestahili kufanya hivyo na hakuna mtu atakayeweza kuamua vinginevyo.
Ninachosema ni kuwa Chadema ushindi ni wao kupoteza na Urais ni wao kuukosa. CCM inaombea tu Chadema wasifanye wanachopaswa. Hata ningekuwa mimi, ningeombea Chadema wasipigane kama mashujaa siku ya ushindi. Kwani harufu ya “siku ya ushindi” inanukia kwa mbali. Chadema watafanya kweli? Tuna wiki mbili kuona kwani wananchi wanaweza kufanya yote wanayotakiwa kufanya lakini mwisho wa siku Pembetatu ya Ushindi itasimama pamoja majukwaani?
Naamini tunapoanza kuelekea katika malango ya CCM kuyatikisha na hata kuyafungua kwa nguvu ili hewa mpya ya mabadiliko ipite, hakuna njia nyingine isipokuwa kuona makamanda wa mapambano haya wakinyanyua bendera juu na wakipiga yowe la “ushindi” bila kuona huruma, woga, haya au kusita. Nje ya hapo ushindi wa CCM hautaepukika.
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
South Africa: South Africa Film Earns Oscar Nomination
43 minutes ago
0 comments:
Post a Comment