MHE. KABWE ZUBERI ZITTO Aliuliza:-
Serikali katika Bunge la tisa ilitangaza kuwalipa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira na kuuchukua mgodi huo ili kuumiliki na kuzalisha umeme.
a) Je, kwa nini Serikali haijawalipa wafanyakazi hao mpaka sasa?
b) Kwa kuwa Shirika NSSF limeleta kwa maandishi Serikalini nia ya kununua madeni yote ya mgodi wa Kiwira.Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya suala hili?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto,Mbunge wa Kigoma Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:
a) Mheshimiwa Spika, suala la mgodi wa Kiwira ni suala ambalo Serikali imekuwa ikilitolea maelezo kila mara hapa Bungeni,hususan,suala la wafanyakazi wa mgodi huo. Aidha, ni kweli Serikali ilitangaza kupitia Bunge la tisa kuwa italipa wafanyakazi wa mgodi huo mishahara yao.
Baada ya tangazo hilo Serikali imefanya malipo ya malimbikizo ya mishahara yao ya miezi 15 kwa awamu mbili kama ifuatavyo:
1. Awamu ya kwanza ilifanyika katika kituo cha Kiwira kwa madai yanayoishia mwezi Julai,2010; na
2. Awamu ya pili imefanyika mwezi wa Januari 2011 kwa madai ya malimbikizo ya kuanzia mwezi Agosti, 2010 hadi Januari 2011.
Malipo yamelipwa hadi kufikia Januari kwa mategemeo kuwa baada ya hapo wahusika watakuwa wanalipwa kwa utaratibu wa kawaida kwa sababu tumeshawaingiza katika bajeti yetu inayoendelea sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba, 2010 mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliwasilisha maombi Serikalini kwa ajili ya kuendeleza mgodi huo. Kufuatia maombi hayo,Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Uchumi na Shirika la Consolidated Holding Corporation ambalo lipo chini ya Wizara ya Fedha,tumeanza mchakato wa awali kutathmini ombi hilo,ili kujiridhisha kama NSSF wanaweza kuendesha shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme kabla ya kutoa mgodi huo kawo. Hivyo,baada ya mchakato (tathmini) hiyo kukamilika,Serikali itaweka bayana suala hili na endapo atakuwa amekidhi masharti atamilikishwa mgodi huo.
MHE. KABWE Z. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Serikali ilitangaza hapa Bungeni kwamba itachukua mgodi wa Kiwra na kuumiliki, lakini mpaka tunavyozungumza hivi sasa, haijafanyika tathmini yeyote ya mali na amdeni ya mgodi kwa ajili ya Serikali kuweza kuuchua. Na tayari mmoja wa wakopeshaji kupitia benki ya CRDB wametangaza kuufilisi mgodi na hivyo kuhatarisha mali na uwekezaji mkubwa ambao Serikali uliufanya katika mgodi huu, Serikali haioni haja ya kuharakisha zoezi na kuumiliki mgodi huu na kuupa kwa taasisi ya NSSF ambayo tayari wameonyesha nia ya kuweza kuhakikisha kwamba wanalipa madeni yote ambayo ni ya mgodi huu ili waweze kuzalisha umeme?
Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kusubiri mchakato uendelee Wizara ya Fedha hayaonyeshi udharura, uharaka au upo mkakati wa mgodi wa Kiwira katika kumaliza tatizo la umeme nchini, na jana takriban masaa mawili nchi nzima ilikuwa haina umeme na TANESCO wametangaza zaidi ya megawati 230 zimeondoka katika gridi ya Taifa. Waziri wa Nishati na Madini analiambia nini Taifa kuhusu Taifa hili? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu Mheshimiwa Spika na Watanzania kwa ujumla kwamba dhamira ya Serikali ya kufanikisha uendelezaji wa mgodi wa Kiwira iko pale pale na kinachoendelea sasa hivi tangu tutangaze hapa Bungeni ni masuala ya kiutalaam ambayo ni lazima tuyafanye kwa utaratibu unaoeleweka ili kuhakikisha kwamba tunapokwenda kuwekeza na kuendeleza mradi ule pasiwe na mashaka yoyote katika mradi huo.
Kwa hiyo muda wote Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya kazi yake kwa utaratibu na umakini kuhakikisha kwamba mradi ule unaendelezwa. Kwa hiyo mchakato unaendelea ni kwa taratibu za kawaida na ndiyo maana vikao kadhaa tumekuwa tukishiriki ambavyo nina hakika Mheshimiwa Zitto anafahamu pia kwa sababu kwa kiasi kikubwa taasisi ambazo zinashirikishwa katika eneo hili ikiwemo NSSF yenyewe ni taasisi ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha. Mikutano inaendelea vizuri na masuala yanayojadiliwa ni kwa maslahi ya Taifa.
0 comments:
Post a Comment