Leon Bahati na Claud Mshana
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemrejeshea cheo cha Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, na kupanga mikakati ya kukabili CCM katika mikoa yote nchini.
Uamuzi huo ulifikiwa jana na Kamati Kuu ya Chadema, kwenye mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo walipanga bajeti ya kufanikisha mipango yao ya kujiimarisha mikoani.
Zitto alinyang'anywa cheo hicho Novemba mwaka jana kwa kile kilichoelezwa ni kwenda kinyume na uamuzi wa chama.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kwamba uamuzi huo ulifikiwa baada ya mjadala mzito.
Baadhi ya wajumbe walimlaumu Zitto kwamba msimamo wake wa kutangaza hadharani kupitia vyombo vya habari hakubaliani na uamuzi wa chama kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, umesababisha kukigawa chama.
Zitto alinyang'anywa cheo hicho kutokana na msimamo wake wa kutounga mkono uamuzi uliopitishwa na wabunge wa chama hicho wa kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kwa kutoka nje ya Bunge.
Zitto na wabunge wengine hakuingia bungeni siku hiyo na aliweka msimamo wake waziwazi kwenye vyombo vya habari kwamba ingawa chama kimekubaliana hivyo, yeye binafsi haungi mkono.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Zitto pamoja na kurejeshewa cheo hicho, alionywa kwa maelezo kwamba hakupaswa kutangaza msimamo wake hadharani.
Chanzo hicho kilieleza kwamba wajumbe walimuonya wakisema angeweza kukaa kimya na kubakia na msimamo wake na hali hiyo isingekiaibisha chama.
Jambo jingine lililozungumza katika kikao hicho ni mgawanyiko ndani ya chama ambao umesababisha kukosa baadhi ya majimbo kwenye uchaguzi uliopita.
Walisema mgawanyiko ndani ya chama hicho ulisababisha wakose majimbo mengi mkoani Kigoma wakati walikuwa na nguvu kubwa ya kisiasa.
Majimbo matano ambayo chama hicho ilikuwa iyachukue, walisema yalinyakuliwa na NCCR-Mageuzi na wao kuambulia moja tu.
Walitoa mfano kwa jimbo Kigoma Kusini ambalo kama sio kumumfukuza ndani ya chama, David Kafulila, wangeweza kulinyakua.
Kafulila ambaye alionyesha kuwa na ushawishi mkubwa kwenye jimbo hilo baada ya kufukuzwa Chadema alihamia NCCR na kushinda kiti hicho.
Awali katika kikao hicho, ambacho kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, Erasto Tumbo,kitajadili masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho, ikiwa ni pamoja na kujadili agenda zilizojadiliwa katika kikao kilichotangulia.
Tumbo alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, agenda kubwa ya kikao hicho, ambacho alisema watatoa tamko baada ya kumalizika, kitajadili mpango mkakati wa Chadema kwa mwaka 2011.
Katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Septemba, 2010, suala la uteuzi wa nafasi za viti maalum kwa wabunge wa chama hicho ambalo lilizua malalamiko ya kuwepo kwa upendeleo, hatua iliyofanya viongozi waandamizi wa chama hicho kwa nyakati tofauti kulitolea ufafanuzi suala hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya vigezo hivyo vya uteuzi wa wabunge iliyotolewa na Dk Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa mwenyekiti wa uteuzi huo, mgombea yeyote ambaye aliwahi kushika wadhifa wa ubunge aliwekewa alama 10 ambacho ni kigezo kimojawapo kati ya sita.
Dk Mkumbo aliongeza kuwa kigezo kingine kilichotumika ni cha uzoefu wa uongozi nje ya siasa, ambacho nacho alifafanua kuwa kilikuwa kimegawanywa katika madaraja mbalimbali.
Kwa Mujibu wa Dk Mkumbo, njia hizo zilitumika ili kuondoa malalamiko mbalimbali yaliyokuwepo, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa upendeleo wa watu wanaotoka Kanda ya Kaskazini.
Kamati kuu ya chama hicho ilikutana Septemba 25, 2010 kujadili suala hilo lakini haikuweza kufikia muafaka na hivyo kulazimika kuendelea na mkuatano huo Septemba 26.
Mkutano huo ulishindwa kumaliza ajenda zake baada ya makundi kuibuka juu ya njia ya kuwapata wabunge hao.
Makundi hayo yalidaiwa kuegemea vigogo wawili wazito ndani ya chama hicho, jambo ambalo liliipasua pia meza kuu na kuiweka katika mazingira magumu katika kuokoa jahazi.
Chama hicho hatimaye kilipitisha majina ya wabunge 105 wa viti maalum, huku kikiwaacha wanachama 42 walioshindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa.
Majina hayo hayakuwekwa hadharani na badala yake yalipelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambapo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 ambapo Chadema ilisimamisha wagombea wa majimbo 185, na kufanikiwa kutwaa majimbo 25, na kupata viti maalum 23.
0 comments:
Post a Comment